Kocha Mkuu wa timu ya Kagera Sugar ya Bukoba, King Abdallah Kibadeni (Mputa), amekuwa wa kwanza kuzungumzia hadharani tuhuma za rushwa katika michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, Tanzania Bara.

Kibadeni alijitoa mhanga kubainisha njia zote zinazotumiwa na baadhi ya waamuzi wa kandanda wa ligi hiyo, kuhongwa na baadhi ya timu ili wazipendelee dimbani kwa kuzisaidia kushinda nje ya sheria 17 za soka.


Siku chache baadaye, vyanzo vya habari vilidokeza kuwapo kwa mkakati wa siri unaofanywa na timu mbili kubwa za Dar es Salaam Young Africans (Yanga) na Simba Sports Club, kutaka kuihujumu Azam FC ishindwe kushika nafasi mbili za juu, kukosa kushiriki michuano ya kimataifa ya Afrika na hata Afrika Mashariki na Kati.


Mwaka jana, Azam ilishika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo msimu huu, Simba, hivyo ikafanikiwa kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).


Tangu ishiriki mashindano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) mwaka 1980 nchini Nigeria, Tanzania haijashiriki tena mashindano hayo. Suala la rushwa hasa kwa waamuzi ni moja kati ya vikwazo vinavyodumaza soka nchini. Hali hiyo imeifanya Tanzania kuwa ngazi katika mashindano ya kimataifa.


Kama alivyodokeza Kibadeni, rushwa inachangia kwa kiwango kikubwa kudumaza soka letu kwa vile viongozi hasa wa klabu kubwa badala ya kutengeneza timu imara zenye ushindani mkubwa uwanjani, wanakazania kuzungumza na waamuzi husika kupitia mlango wa nyuma.


Kibadeni amesema yupo tayari kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kukabili vitendo vya rushwa katika soka, hivyo apewe ushirikiano wa kutosha. Kibadeni amewahi kuwa mchezaji mahiri wa timu za Simba, Taifa Stars na Majimaji ya Songea, kabla ya kustaafu na kujikita katika ukocha wa kabumbu.


Kama msimamizi mkuu wa soka nchini, Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) linapaswa kumkutanisha haraka na Takukuru asaidie kufanya uchunguzi, kubaini mianya ya rushwa inayozidi kuwa janga kubwa kwa maendeleo ya soka nchini.