pg 1Sasa ni wazi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kipo kwenye hatua za mwisho za kufumuliwa na kuundwa upya.

Hatua hiyo itawezekana punde tu baada ya Rais John Magufuli, kupigiwa kura na Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliopangwa kufanyika Julai 23, mwaka huu mjini Dodoma.

Mkutano huo utashuhudia chama hicho kikiandika historia nyingine kwa Mwenyekiti wa sasa, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, kung’atuka na hivyo kumwachia Rais Magufuli.

Wakati maandalizi ya mkutano huo yakiwa yanaelekea tamati, watu walio karibu na Rais Magufuli, wanasema kiongozi huyo anatumia muda mrefu akiwa na watu anaowaamini, kubuni muundo mpya wa kuirejesha CCM kwenye ulingo wa ushindani ili iweze kukabiliana vilivyo na joto la vyama vingine vya upinzani vinavyoelekea kuwa na ushawishi mkubwa hasa kwa vijana.

Kwenye mabadiliko hayo, Rais Magufuli, anatajwa kujielekeza kwanza kwenye Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo kwa mfumo wa chama hicho ndiyo injini ya mwelekeo na mafanikio ya chama kwa jumla.

Novemba 2012, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM iliridhia mapendekezo ya Mwenyekiti Kikwete, na kuwapitisha makada saba wa chama hicho kuwa Wajumbe wa Sekretarieti.

Katibu Mkuu wa CCM ambaye kwa nafasi yake ni Mwenyekiti wa Sekretarieti, alipitishwa Abdulrahman Kinana; mtu anayetajwa kuwa ‘mkombozi’ wa CCM iliyokuwa imeshapoteza umaarufu kwa kiwango cha juu mno miongoni mwa wananchi.

Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, ilikwenda kwa Vuai Ali Vuai.

Naibu Katibu Mkuu Bara akapitishwa Lameck Nchemba; Katibu wa Oganaizesheni akawa Mohamed Seif Khatibu; Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, akawa Asha-rose Migiro; nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha ikashikwa na Zakhia Meghji; na aliyepewa dhima ya Itikadi na Uenezi ni Nape Nnauye.

Kati ya wote hao, waliobaki hadi sasa ni Kinana, Vuai, Khatibu, na Meghji.

Mwigulu alijiuzulu mwaka jana ili agombee urais. Nafasi yake ikazibwa na Rajab Luhwavi, ambaye kabla ya hapo alikuwa Mshauri wa Rais Kikwete wa masuala ya siasa. Nafasi ya Dk. Migiro ilizibwa na Kikwete, kwa kumteua Pindi Chana, ambaye ni Naibu Waziri pekee kati ya wale waliomaliza na Kikwete, aliyeachwa kwenye uteuzi wa nafasi mbalimbali uliofanywa na Rais Magufuli.

Nape aliacha nafasi hiyo na mara moja ikazibwa na aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka.

Habari za uhakika zinasema ni majaliwa tu yanayoweza kuwafanya Kinana, Vuai, Luhwavi, Meghji, Chana, Sendeka na Khatibu, kurejeshwa kwenye Sekretarieti mpya itakayoundwa mapema na Mwenyekiti mtarajiwa, Rais Magufuli.

Kinana, mtu anayeheshimika ndani na nje ya CCM kwa kukirejeshea uhai chama hicho, huenda akaamua kupumzika baada ya kazi kubwa aliyoifanya na pia kusimamia kampeni za wagombea wengi wa urais wa CCM na kufanikisha ushindi.

Watu walio karibu naye wanasema anataka akae kando kama mpango wake wa kulinda heshima aliyokwishajipatia ndani ya CCM.

“Kinana ni mfuasi mzuri wa misingi ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Anapenda ang’atuke akiwa na heshima. Ikumbukwe hata Ukatibu Mkuu alikubali mwaka 2012 baada ya kuombwa sana na wazee ndani ya chama. Hakutaka kuwa Katibu, lakini aliheshimu mwito wa wazee wastaafu walioona ndiye mtu pekee kwa wakati huo aliyekuwa na uwezo wa kukiokoa chama,” kimesema chanzo chetu.

Kurejeshwa kwa Vuai si jambo la kutarajiwa sana kutokana na kutajwa kuwa haivi chungu kimoja na vigogo kadhaa wa CCM Zanzibar, akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Lakini pia Vuai anatajwa kuwa mwenye makundi ambayo kwa namna fulani yamesaidia kudhoofisha nguvu ya chama hicho kwa upande wa Zanzibar.

Khatibu, naye anakabiliwa na wakati mgumu kurejeshwa kwenye nafasi hiyo ya Oganaizeshi ambayo kimsingi ndiyo injini ya Mipango ya Kiuchumi ndani ya chama.

Nafasi hiyo inahitaji kijana mwenye kasi, mbinifu na mwenye msimamo ili kukijenga chama hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Ndani mwakani. Khatibu anatajwa kuwa na kasi ndogo kwenye utekelezaji mambo mbalimbali yanayohitaji kasi. Khatibu amekuwa kiongozi kwa muda mrefu, akianzia Umoja wa Vijana.

Luhwavi, licha ya kuwa kada wa muda mrefu, staili yake ya uongozi inaweza isimvutie Mwenyekiti Magufuli. Anatajwa kuwa mtu asiye na makeke ya utendaji kazi na hivyo kujiweka kwenye mazingira ya kutokuwamo kwenye Sekretarieti mpya itakayoundwa.

Kwa upande wa Meghji, mwanasiasa huyo ni miongoni mwa wakongwe wanaoheshimika ndani na nje ya CCM. Amekuwa akishika nafasi mbalimbali ndani ya CCM na katika Serikali.

Kigezo cha umri kinaweza kutumika kumweka kando ili kupisha damu changa zinazoweza kwenda na kasi ya kuleta mabadiliko ndani ya CCM. Hata hivyo, anaweza kuendelea kwa kutumia kigezo cha kuchanganya damu mpya na ya zamani katika utendaji kazi.

Uwezekano wa Chana kuendelea kuwa kwenye Sekretarieti ni jambo ambalo haliko wazi sana. Hii inatokana na uamuzi wa Rais Magufuli, kutoeleweka msimamo wake wa moja kwa moja kwa kada huyo.

Chana ndiye Naibu Waziri pekee kwenye Baraza la Mawaziri la mwisho la Serikali ya Awamu ya Nne, ambaye Rais Magufuli, kwenye uteuzi wake alimwacha. Manaibu wenzake waliteuliwa kuwa wakuu wa mikoa.

Agrey Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Stephen Kebwe ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Afya, sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro. Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Anne Kilango ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango-Malecela; aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, kabla ya kufukuzwa wiki kadhaa baadaye kutokana na ripoti isiyo sahihi ya wafanyakazi hewa.

Chana ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; ndiye pekee kwenye kundi la manaibu waliokosa ubunge na pia wakakosa ukuu wa mkoa.

Hata hivyo, akiwa anaonekana Ofisi Ndogo za CCM, Lumumba, Mwenyekiti Kikwete, aliweza kumpachika kwenye Sekretarieti kuziba nafasi ya Dk. Migiro.

“Je, aliachwa kwenye ukuu wa mkoa kwa makusudi ili apelekwe kwenye Sekretarieti, au aliachwa kwa sababu si chaguo na mkubwa (Magufuli)? Je, alionewa huruma na Kikwete kwa kuukosa japo ukuu wa mkoa na hivyo akampachika kwenye Sekretarieti? Hapo inakuwa vigumu kuelewa, nadhani ni suala la muda tutajua,” kimesema chanzo chetu.

Sendeka, ambaye ameshika nafasi hiyo kwa makeke, kuendelea kuwapo kwake kwenye nafasi hiyo ni jambo litakalohitaji ujasiri wa Mwenyekiti mpya.

Watu walio karibu na Rais Magufuli, wanasema kwa malengo na maudhui ya muundo mpya wa chama hicho, Itikadi na Uenezi vinahitaji mtendaji aliye tofauti na aliyepita, yaani Nape.

“Aina ya Serikali iliyopita ilihitaji mtu wa kutetea makosa yaliyokuwa yakifanywa na Serikali kwa lengo la kuyafunika. Alitafutwa kijana mwenye kelele.

“Serikali ya Awamu ya Tano ni tofauti kabisa. Anahitajika mtu mtulivu, msikivu mwenye uwezo wa kujenga uhusiano kati ya chama na wananchi, chama na vyombo vya habari, na chama na serikali.

“Anahitajika mtu wa kutafsiri na kutekeleza ilani na sera za chama. Kwa maana hiyo huhitaji tena mtu aina ya Nape ambaye licha ya weledi na uwezo wake mkubwa kwenye kutetea, alifanya kazi hiyo ya kushambulia ili kuficha udhaifu wa Serikali.

“Ukitazama kwa kina unaona Sendeka ni aina ya Nape, anaweza asiwe na msaada ya kusukuma ajenda ya utekelezaji wa ilani.

“Anahitajika mtu kwenye a, b, c za mawasiliano ya umma kwa kina kuanzia kwenye lugha anayoitumia hadi kwenye utekelezaji,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:

“Mabadiliko ya Sekretarieti hayana budi yafanywe kwa weledi na kwa ujasiri. JPM aanze kujenga Sekretarieti yenye kuchapa kazi ili kuandaa mazingira mazuri ya uchaguzi wa mwakani.

“Ukiwa na Sekretarieti dhaifu unakuwa na viongozi dhaifu kwenye nafasi mbalimbali kama za Makatibu wa Mikoa. Kwa mfano, Dar es Salaam tumeshawahi kuwa na Katibu (anamtaja) ambaye ni dhaifu mno. Hao ndiyo aina ya watu aliowata Kikwete kutokana na staili yake ya uongozi. Utaona aina ya watu waliojitokeza kugombea mwaka 2010 na wakashinda ni aina ile ile ya viongozi waliokuwapo.

“Magufuli asifanye kosa, aunde Sekretarieti ya kumsaidia kuleta maboresho ndani ya chama kuelekea Uchaguzi wa mwaka 2017.

“Anakabidhiwa chama huku karibu asilimia 90 ya viongozi wamepata nafasi walizonazo kwa rushwa.”

 

Utegemezi fedha za uchaguzi

 Eneo jingine ambalo ‘Mwenyekiti’ Rais Magufuli, anatajwa kuanza nalo, ni suala la kuhakikisha chama kinajitegemea kwa mapato ili kisiyumbe wakati wa mikutano yake pamoja na kwenye ushiriki wa Uchaguzi Mkuu.

Suala la utegemezi linatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayomkera mno Rais Magufuli, lakini inatajwa kuwa ombaomba hiyo imetumiwa kama upenyo wa baadhi ya wanachama na viongozi ndani ya CCM kuchukua fedha kutoka kwa matajiri kwa kigezo cha kukisaidia chama kushinda uchaguzi.

“Kuna fedha nyingi sana zinakusanywa kutoka kwa wafanyabiashara -ndani na nje ya nchi- maelekezo ni kuwa zinapelekwa kukisaidia chama, lakini ukweli zinaishia mifukoni kwa wachache.

“Sasa hivi ukipita mitaani utaambiwa fulani amechangia bilioni kadhaa, fulani ametoa milioni kadhaa, lakini hizo fedha hazionekani kwa sababu hakuna mfumo wa kuzidhibiti.

“Rais Magufuli anaamini chama kikijitegemea kwa mapato kitaacha kuwa ombaomba na upenyo huo utafungwa, lakini kubwa zaidi ni kulinda hadhi na heshima ya chama ili baada ya Uchaguzi Mkuu kusiwepo wafanyabiashara wa kutaka watendewe fadhili kwa kigezo cha kukisaidia chama. Misaada itapokewa, lakini siyo yenye masharti ya kutaka rais anayeingia madarakani alipe fadhili kwa kuwasamehe kodi au kuwapendelea kwenye mambo ya zabuni na mengine,” kinasema chanzo chetu.

Lingine linaloendana na hilo, na ambalo Rais Magufuli, anatajwa kulivalia njuga ni la malipo ya mishahara kwa watumishi ndani ya CCM.

Watumishi wengi, hasa wa ngazi za chini na za kati wanalia ukata mkubwa kutokana na mishahara midogo, huku fedha nyingi zikiishia kwa vigogo ndani ya chama hicho.

Licha ya kulipwa kidogo, watumishi wengi wamekuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa malipo yao, jambo ambalo uongozi wa Kikwete unatajwa kuwa haukulipa kipaumbele.

Jambo jingine ambalo Rais Magufuli, ameliwekwa kwenye kipaumbele ni kuhakikisha chama kinaondokana na dhana ya kujiendesha kwa kutegemea ruzuku.

Hofu yake inatajwa kusababishwa na ukweli kuwa ruzuku kwa chama hicho imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka kutokana na kupungua viti vya ubunge kunakosababishwa na ushindani wa vyama vya siasa.

Kati ya mwaka 2009/2010 na mwaka 2012/2013 CCM ililipwa ruzuku Sh bilioni 50.97. Kwa kipindi hicho CHADEMA ilipata Sh bilioni 9.2; CUF (Sh bilioni 6.29), NCCR – Mageuzi (Sh. milioni 677), UDP (Sh milioni 33); TLP (Sh. milioni 217), APPT (Sh milioni 11), DP (Sh milioni 3.3) na CHAUSTA iliambulia Sh milioni 2.4.

“Inatakiwa iundwe Sekretarieti ya kukifanya chama kiondokane na utegemezi wa ruzuku. Kijitegemee kwa mapato yake. Kwa sasa kuna vitega uchumi vingi ambavyo viko mikononi mwa wafanyabiashara waliojitwalia kijanja.

“CCM ndiyo namba mbili baada ya NHC (Shirika la Nyumba la Taifa) kwa kuwa na ardhi kubwa na nzuri, kinachopaswa ni kuitumia ardhi hiyo kuingiza mapato na hivyo kuwalipa vizuri watumishi, kugharimia shughuli za chama na mambo mengine ya kimaendeleo.

“Ni aibu kwa CCM kutegemea ruzuku kujiendesha. Focus ya Sekretarieti anayotaka kuiunda anataka iwe ya kujitegemea na kuondoa dhana ya uongozi wa mazoea,” amesema mtu aliye karibu na Rais Magufuli.

 

Panga wajumbe wa NEC wa Wilaya

 Eneo jingine linalotajwa kurekebishwa mapema iwezekanavyo ni la kufuta utaratibu wa Wajumbe wa NEC Taifa wanaotoka kila wilaya nchini.

Utaratibu huo ulianzishwa mwaka 2012 kwa kupigiwa debe na Mwenyekiti Kikwete, akisema ulilenga kukirejesha chama karibu na wanachama kwenye ngazi za chini, na kutoa uwakilishi wenye uwiano.

“Huu ni utaratibu wa ovyo kuwahi kutokea CCM. Umekiumiza sana chama. Ni utaratibu uliowekwa kinyume cha matakwa ya u-NEC. NEC imekosa nguvu kwa sababu wameingia watu wa ovyo kwa ushabiki tu.

“Ile dhamira ya chama kusimamia Serikali imepotea kwa sababu hakuna wajumbe wa NEC wenye kusaidia kutekeleza hilo,” anasema.

Anatoa mfano wa kilichotokea mwaka jana katika Ukumbi wa Whitehouse, baada ya wajumbe kadhaa wa NEC kuimba “tuna imani na Lowassa’, badala ya kuimba “tuna imani na Kikwete.”

Awali, NEC ya CCM ilikuwa na wajumbe 200 hivi kutoka nchi nzima, lakini baada ya utaratibu wa kuwa na wajumbe kutoka kila wilaya, idadi hiyo imepanda hadi zaidi ya 400.

“Huwezi kuwa na wajumbe zaidi ya 400 kwenye ukumbi halafu ukajadili jambo la nchi kwa utulivu na weledi. NEC imekuwa vurugu tu,” kimesema chanzo chetu.

Kubadili mfumo huo wa upatikanaji wajumbe wa NEC kwa kurejea ule wa zamani au kubuni mfumo mwingine; ni jambo ambalo Rais Magufuli, anatajwa kulipa kipaumbele.

 

Wazee kurejeshwa CC?

CCM wanakiri kuwa uwepo wa wazee katika Kamati Kuu (CC) wakati wa mchujo wa wagombea urais mwaka jana ulikisaidia mno chama hicho kutoka kwenye hatari ya kumeguka.

Hatua hiyo inatajwa na watu walio karibu na Rais Magufuli, kuwa huenda ikamfanya aone umuhimu wa kuvunja utaratibu ulioasisiwa na Kikwete, uliowaengua kwenye CC na vikao vingine; badala yake wakaundiwa Baraza la Ushauri la Wazee ambalo halipo kikatiba.

“Tunahitaji busara ya wazee. Tulifanya makosa kuwaondoa kwenye vikao vya uamuzi. Sababu za kuwatoa hazijaleta mashiko kwa sababu kila pale chama kilipofika pagumu, wazee walisaidia. Kuna sababu za kuwarejesha CC na katika NEC. Kunatakiwa kuwepo utaratibu wa kuwashirikisha wazee moja kwa moja badala ya kuwatumia kupitia kwenye Baraza.

Baraza linaundwa na wajumbe sita ambao ni Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wastaafu Taifa wa chama hicho. Viongozi hao ni Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi (Mwenyekiti), Pius Msekwa (Katibu), Mwenyekiti na Rais mstaafu Benjamin Mkapa (Mjumbe); Makamu Mwenyekiti na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume; Makamu na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour; na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu John Malecela.  

 

Jumuiya kusukwa upya

 Eneo jingine linalotajwa kumuudhi Rais Magufuli, ni ‘kifo’ cha Jumuiya za chama hicho. CCM ina Jumuiya tatu za Umoja wa Wanawake (UWT), Jumuiya ya Wazazi na Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVT).

Kwa sasa Jumuiya pekee inayoonekana kuwa na uhai kidogo ni ya Wazazi inayoongozwa na Abdallah Bulembo.

“Jumuiya ya Vijana ni kama imekufa. Jumuiya ya Wanawake ipo ipo kwa sababu Mwenyekiti wake alishakuwa na upande-ipo kama haipo. Vijana ndiyo injini ya chama, lakini kwa sasa husikii ikitoa matamko ya kukitetea au kukikulinda chama dhidi ya mashambulizi ya vyama vya upinzani.

“Ukiwasikiliza Chadema unaona wana nguvu kwa vijana wao, lakini CCM Jumuiya imekufa kabisa. Hii inahitaji kufufuliwa upya ili itekeleze wajibu wake wa kukilinda na kukitetea Chama bilsa kusahau wajibu wake wa kuwaandaa viongozi wa baadaye,” kimesema chanzo chetu. 

 

Vita dhidi ya rushwa

 Vita dhidi ya rushwa inaweza kuwa ndiyo ajenda binafsi kuu ya Rais Magufuli, akishakabidhiwa Uenyekiti.

JAMHURI imethibitishiwa kuwa msimamo wake dhidi ya rushwa atautangaza bayana baada ya kukabidhiwa kiti, na anatajwa kuanza kuchukua hatua zinazokaribiana na zile alizoanza kuzichukua ndani ya Serikali.

“Anajua namna rushwa inavyotumika kupata uongozi. Ana uozefu wa namna alivyoombwa rushwa bila kificho wakati akipita kuomba adhaminiwe kuwania urais. Kuna sehemu hakupata mapokezi mazuri kwa sababu wanachama walijua yeye si mtoa fedha kwa hiyo walimkimbia.

“Anajua rushwa ni kansa kubwa ndani ya CCM na njia pekee ni kupambana nayo kwa nguvu zote. Anajua maskini kwa sasa hata awe na uwezo wa kuongoza mkubwa kiasi gani, hawezi kupata uongozi bila fedha.

“Rais Magufuli, ameshuhudia watu wanavyotumia fedha kununua uongozi ndani ya chama na katika Serikali. Amekusudia kuanzisha kitengo maalumu cha kukabiliana na rushwa ndani ya CCM pamoja na kuishirikisha Takukuru.

“Hilo nakuhakikishia atalitolea msimamo pale pale ukumbini Dodoma baada ya kukabidhiwa uenyekiti. Anataka chama kirejee kwenye misingi yake ya asili hata kama kwa kufanya hivyo kutapunguza ushawishi wa baadhi ya wanachama. Anaamini heri awe na wanachama wachache waadilifu ambao kwa uadilifu wao watawafurahisha Watanzania na kwa sababu hiyo watawafanya wananchi waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi na kukichagua,” kimesema chanzo chetu.

 

Historia ya CCM

CCM ilizaliwa Februari 5, 1977. Ni matokeo ya kuunganishwa kwa vyama viwili vya Tanganyika African Nationa Union (TANU) na Afro-Shiraz (ASP).

Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM ni Mwalimu Julius Nyerere, aliyefuatiwa na Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.