Mahakama ya kikatiba ya Korea Kusini imefanya kikao chake cha kwanza kuamua iwapo Rais aliyesimamishwa kazi Yoon Suk Yeol aondolewe madarakani baada ya jaribio lake la kushtukiza la kutekeleza sheria ya kijeshi mwezi uliopita.

Hata hivyo kikao hicho kiliisha ndani ya dakika nne kwa sababu ya kutokuwepo kwa Yoon – mawakili wake walikuwa wamesema awali hatahudhuria kwa usalama wake, kwani kuna kibali cha kukamatwa kwake kwa mashtaka tofauti ya uasi.

Mnamo mwezi Desemba, Yoon alisimamishwa kazi baada ya wanachama wa chama chake pamoja na upinzani kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.

Hata hivyo ataondolewa rasmi afisini ikiwa tu angalau majaji sita kati ya wanane wa mahakama ya kikatiba watapiga kura kuunga mkono mashtaka hayo.

Kulingana na sheria za Korea Kusini, mahakama lazima ipange tarehe mpya ya kusikilizwa kwake kabla ya kuendelea bila ushiriki wake.

Kesi inayofuata imepangwa kufanyika Alhamisi.

Mawakili wa Yoon wameeleza kuwa atajitokeza kusikilizwa kwa “wakati mwafaka”, lakini wamepinga ‘uamuzi wa upande mmoja’ wa mahakama katika tarehe za kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Yoon hajatoa maoni yake hadharani tangu Bunge lilipopiga kura ya kumshtaki tarehe 14 Desemba na amekuwa akizungumza hasa kupitia mawakili wake.

Yoon ni rais wa kwanza wa Korea Kusini kukabiliana na mashtaka ya kukamatwa.

Jitihada za pili za kumweka kizuizini zinaweza kufanyika mapema wiki hii, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.