Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Kesi ya aliyekuwa kigogo wa Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa Umma(PSSSF),Rajabu Kinande na wenzake Ashura Kapera (36), Farida Mbonaheri (33), Mohamed Miraji (47) na Msafiri Raha walikuwa wakikabiliwa na mashitaka manne likiwemo wizi imeahirishwa tena
Chanzo cha kuhahirisha kesi hiyo ni mmoja wa washitakiwa hao kunyosha mkono na kuiomba mahakama iahirishe shauri hilo, kwa kuwa wakili wao wa utetezi yupo Mahakama Kuu kwenye shauri lingine.
Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Serikali,Michael Ng’oboko kuieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Ndipo taarifa kutoka kwa mmoja wa washitakiwa aliieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala kuwa wakili wao wa utetezi alimpigia simu, kuwa amepokea wito kutoka mahakama.kuu hivyo hatakuwepo kwenye shauri hilo.
“Wakili wetu ameoiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine Kwa kuwa alipewa wito na mahakama kuu na leo hii yupo huko,”amedai mshtakiwa huyo.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi,Fadhiri Luvinga amesema kesi hii imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara hadi sasa wamesikiliza shahidi mmoja bado wanne.
Luvinga amewataka upande wa utetezi kuhakikisha shauri lijalo wanakuwepo ili shauri hilo liweze kwenda mbele.
“Mbona kesi hii inaahirishwa inaahirishwa sana kwa wakili wenu wa utetezi yupo mmoja naipanga tarehe ya karibu ili shauri hili liweze kuisha,” amesema Luvinga.
Shauri hilo limeahirishwa Agosti Mosi,2022 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Katika kesi ya msingi ilibainika kuwa mnamo Juni 16,2020 mtaa wa Gerezani Wilaya ya Ilala washtakiwa washtakiwa kwa pamoja walivunja na kuingia kwenye duka na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh.milioni 60.8 mali ya Mohamed Soli,Anwar Hemed, Rashidi Hassan na Salehe Seleman.