*Ni ya Mama Lela aliyetajwa na Rais Obama
Kesi ya mtuhumiwa mkubwa wa dawa za kulevya duniani aliyekamatwa eneo la Mbezi jijini Dar es Salaam imetajwa wiki hii.
JAMHURI ilipata taarifa kutoka Mahakama Kuu kuwa kesi hii, inahusisha watuhumiwa wanane akiwamo Mtanzania Mwanaidi R. Mfundo. Pia nchini Kenya na Marekani anafahamika kwa jina la Naima Mohamed Nyakiniywa au Naima Nyakinywa, maarufu Mama Lela huko Mbezi, jijini Dar es Salaam akiwa pamoja na Wakenya saba, imetajwa jana Mahakama Kuu.
Rais wa Marekani, Barack Obama, Mei 29, 2011 alimtangaza Naima mwenye kufahamika kwa majina yote yaliyotajwa hapo juu kuwa muuza ‘unga’ mkuu duniani, hivyo akapigwa marufuku kuingia nchini Marekani.
Rais Obama alitumia Sheria ya Kudhibiti Wauza ‘Unga’ Wakubwa ya Marekani Na. 21 ya Mwaka 1901 kumtaja Naima kuwa ni muuza ‘unga’ mkubwa na haruhusiwi kukanyaga Marekani kuanzia mwaka 2011 na kuendelea.
“Kama vile Mungu alikuwa upande wetu, mama huyu Juni 1, 2011 tulimkamata kule Mbezi Beach. Alipokamatwa akataka kutoa milioni 60 na chochote tunachotaka, tukasema ‘hapana. Tumeapa kudhibiti dawa za kulevya na hivyo tunakukamata; alijaribu kuomba dhamana, lakini kwa uaminifu mkubwa Jaji Kaduli akatoa hukumu ya kumnyima dhamana Desemba 16, 2011. Hadi sasa yuko ndani,” kilisema chanzo chetu.
Kesi hii ya Mwanaidi Mfundo sasa imetajwa mbele ya Jaji Kaduli. Chanzo cha habari kinasema kuwa Ujerumani walipopata taarifa kuwa Mfundo amekamatwa, wakaomba kupitia ubalozi wao Tanzania afutiwe kesi hapa nchini, kisha apelekwe Ujerumani katika Jimbo la Hanover, ambako ana kesi 60 zinazomkabili mama huyu kuhusiana na dawa za kulevya, lakini Mwanasheria Mwampoma wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) akakataa.
“Mwampoma alisema sheria zetu haziruhusu kumsafirisha Mtanzania kwenda nchi nyingine kushitakiwa, hivyo akasema kesi inayomkabili Mama Lela iendelee hapa hapa Tanzania, ambapo alikuwa sahihi kisheria kwani sheria zetu ziko hivyo,” kilisema chanzo chetu.
Pamoja naye, Rais Obama kwa kutumia hati ya kusafiria aliyokuwa nayo Mama Lela ikionesha kuwa ni Mkenya, alimtangaza pia Mbunge wa Kenya, John Harun Mwau, kuwa naye ni muuzaji mkubwa wa dawa za kulevya hivyo akampiga marufuku kuingia Marekani.
Wengine waliopigwa marufuku kuingia Marekani kwa tangazo hilo la Rais Obama na nchi zao kwenye mabano ni Manuel Torres Felix (Mexico), Gonzalo Inzunza Inzunza (Mexico), Haji Lal Jan Ishaqzai (Afghanistan), Kamchybek Asanbekovich Kolbayev (Kyrgyzstan) na Javier Antonio Calle Serna (Colombia).
Hadi tunakwenda mitamboni kesi hiyo ya kilo nane za dawa za kulevya ilikuwa bado inaendelea na hatukuweza kujua itatajwa tena lini. Kesi hii imetajwa baada ya Gazeti JAMHURI kubainisha kuwa kesi nyingi zilizopelekwa mahakamani kuwa zimetelekezwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, ametoa taarifa mwishoni mwa wiki iliyopita akiunga mkono juhudi za JAMHURI kwa maelezo kuwa kati ya kesi 149 zilizofunguliwa tangu mwaka 2006, ni kesi moja tu iliyohitimishwa na Mahakama.
Kati ya aliyoyazungumza Waziri Lukuvi ni kuwa Serikali inajiandaa kufuta Sheria ya Dawa za Kulevya Na. 9 ya mwaka 1995 na kutunga sheria mpya itakayomaliza tatizo la dawa za kulevya.
Akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, Lukuvi alisema haoni sababu ya Sheria ya Dawa za Kulevya kutoa fursa ya watuhumiwa kupigwa faini au kifungo.
“Nimesema Sheria hii ipitiwe na wadau wote na kisha tuandae muswada. Muswada huu ninavyoona mimi, kesi lazima iishe ndani ya siku saba, na sheria isitoe fursa ya faini. Mtu akithibitika kuwa ana hatia, alipe faini na kifungo.
“Sheria isiseme faini au kifungo, bali isema faini na kifungo. Wakubwa hawa wanaouza dawa za kulevya hawataki kufungwa. Ukiwafunga hata miaka 30 tu, na ukabahatika kufunga watatu au watano, tatizo hili litakwisha hapa nchini,” alisema Lukuvi.
Kwa muda wa miezi miwili sasa Gazeti JAMHURI limekuwa likipambana na wauza dawa za kulevya na kati ya mafanikio yaliyofikiwa, ni Serikali kuanza mchakato wa kufuta Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya ya Mwaka 1995 na kutunga mpya itakayokuwa kali na kumaliza tatizo hili.