Ijumaa iliyopita Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Dk. John Magufuli, alikutana na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Ni wafanyabiashara kutoka mikoa yote nchini. Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam kwa saa zaidi ya nane, mengi yalijitokeza huku Rais Magufuli binafsi akionyesha utayari wa kiwango cha juu wa kuhakikisha vikwazo visivyo na sababu dhidi ya wafanyabiashara na biashara nchini vinaondolewa.

Wafanyabiashara walibainisha kasoro kadhaa, na miongoni mwa kasoro hizo, taasisi kadhaa za serikali zimetajwa kama sehemu ya kasoro hizo. Taasisi zilizotajwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), sambamba na mamlaka nyingine za udhibiti na ukaguzi.

Kwa mfano, TRA imedaiwa kuwa na mwenendo mbaya katika ukadiriaji wa kodi kwa wafanyabiashara, kwamba baadhi ya maofisa wa chombo hicho wamekuwa wakiweka makadirio ya juu ya kodi ili hatimaye wafanyabiashara wanaolengwa watumie mlango wa ‘uani’ kutoa rushwa moja kwa moja kwa maofisa hao, na tafsiri katika mazingira hayo ni kwamba serikali hupoteza mapato.

Lakini mbali na hayo, imeelezwa hali ya urasimu imekuwa kikwazo vilevile dhidi ya tasnia ya biashara. Kumekuwa na mlolongo mkubwa wa vibali ili kumwezesha mwekezaji katika biashara fulani kuanza shughuli zake.

Kwa ujumla, kwa kuzingatia yaliyojiri katika mkutano huo kati ya Rais Magufuli na wafanyabiashara, unaweza kusema kwamba kuna mkatiko mkubwa wa ufanisi kati ya Rais Magufuli na watendaji wengine wa ngazi za chini wanaomsaidia, vinginevyo kero zilizobainishwa na wafanyabiashara wale Ikulu wiki iliyopita zingepaswa kutatuliwa na wasaidizi wake ngazi za wilaya, mikoa au hata taifa kabla ya kumfikia rais mwenyewe.

Kwa hiyo, sisi JAMHURI, ni matumaini yetu kuwa kasoro zote zilizobainishwa zitapatiwa ufumbuzi ili hatimaye kukwamua hali ya uendeshaji wa biashara nchini ambayo imekuwa ikitajwa kuporomoka siku hadi siku. Ni vizuri wakati wote kutambua kuwa tunajenga nchi moja, lakini ujenzi huo ni lazima uhusishe juhudi za mtu mmoja mmoja. Itashangaza sana kama mwakani au miaka michache baadaye ukafanyika mkutano kama huu wa wafanyabiashara na rais, kisha malalamiko yaleyale yakaendelea kujitokeza.