Rais William Ruto ametangaza kifo cha Ogolla pamoja na maafisa wengine 9 wa jeshi huku wawili wakinusuruka.
Akitangaza kifo cha Jenerali Ogolla rais Ruto amesema kutakuwa na siku tatu za maombolezo kuanzia Ijumaa tarehe 19 Aprili ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kwa kipindi hicho .
Amemtaja Jenerali Ogolla kama afisa shupavu aliyefariki akiwa kazini.
Maafisa hao walikuwa wamesafiri hadi eneo la kaskazini mwa Kenya ambalo limekuwa likikumbwa na visa vya wizi wa mifugo.
Walikuwa kwenye shughuli ya kufungua tena baadhi ya shule zilizofungwa kufuatia mashambulizi ya majambazi. Pia walitembelea maafisa wa kijeshi waliotumwa kuleta utulivu katika eneo hilo.
Jenerali Francis Ogolla alikuwa afisa mkuu wa kijeshi wa Kenya na mshauri mkuu wa kijeshi wa Rais na Baraza la Mawaziri.
Aliteuliwa na Rais Ruto Aprili mwaka jana baada ya kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga na Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.
Katika ajali hiyo maafisa wengine wamepoteza maisha ni; Brigedia Swale Saidi,Kanali Duncan Keittany, Luteni Kanali David Sawe, Meja George Benson Magondu,Kapteni Sora Mohamed, Kapteni Hillary Litali, Sajenti Mwandamizi John Kinyua Mureithi, Sajenti Cliphonce Omondi, na Sajenti Rose Nyawira.