Bodi ya Udhibiti wa Kamari na Utoaji Leseni imesimamisha matangazo ya kamari kwenye majukwaa yote ya mawasiliano na vyombo vya habari kwa siku 30, na marufuku hiyo inaanza kutekelezwa mara moja.
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Jane Mwikali Makau, akisimamisha matangazo hayo, alisema Serikali imebaini kwa wasiwasi mkubwa, kukithiri kwa shughuli za kamari kote nchini.
Shughuli za kamari zilizoathiriwa ni pamoja na kamari, michezo ya kubahatisha, mashindano ya kuzawadi kutokana na bahati na nasibu, na shughuli zote zinazohusiana na hilo.
Mwikali alisema baadhi ya wanaoendeleza kamari wanazidi kupotosha na kuichukulia kama fursa halali ya uwekezaji katika njia ya mkato ya uzalishaji mali.
Alisema hii imesababisha athari mbaya kwa watu binafsi, familia na jamii kwa ujumla.
