Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umepokea ujumbe wa Kurugenzi ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Kenya (DOSHS) wenye dhumuni la kujifunza kutokana na mafanikio ya WCF Tanzania na kuboresha mahusiano baina ya taasisi hizo mbili.
Akizungumza baada ya kuupokea ugeni huo,Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu amesema ushirikiano baina ya WCF na DOSHS utaboresha maeneo mbalimbali ya utendaji kwa pande zote mbili.
“Karibuni WCF na Tanzania kwa ujumla, naamini ujumbe huu utapata nafasi ya kujifunza mengi kutoka WCF kama ambavyo dira yao inavyosema kuwa wanaazimia kuwa mfano wa kuigwa (role model) katika utoaji wa Fidia kwa Wafanyakazi barani Afrika”, amesema Prof. Katundu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John K. Mduma amesema anatarajia ushirikiano endelevu na chanya baina ya DOSHS na WCF katika kulinda nguvukazi za mataifa husika.
“WCF inategemea ushirikiano chanya wenye lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo hasa wakati huu ambao wenzetu wa Kenya wanajiandaa kuunda chombo kitakachokua kinasimamia masuala ya Fidia kwa wafanyakazi watakaopatwa na majanga wakiwa katika majukumu yao ya kikazi”, amesema Dkt. Mduma.
Kiongozi wa ujumbe huo kutoka DOSHS Kenya, Dkt. Musa Nyandusi amesema wanatarajia kujifunza mengi kutoka WCF Tanzania kutokana na mafanikio na uzoefu wa Mfuko.
“Nyumbani Kenya bado hatuna taasisi rasmi ya kushughulikia masuala ya Fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhila yanayotokana na kazi. Ziara hii ya mafunzo itatusaidia sana katika kuandaa njia ya kuunda Mfuko kama huu ili na sisi tunufaike”, amesema Dkt. Nyandusi na kuendelea
“Tuliamua kutembelea WCF Tanzania kwa sababu tangu kuanzishwa kwake mnamo Julai Mosi mwaka 2015, tayari wameonesha ukomavu na ubobevu katika utoaji wa mafao ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi” amesema.