Rais wa Kenya, William Ruto, ametangaza kufuta mikataba ya ubia kati ya serikali na kampuni ya India ya Adani Group, ikiwemo ule wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na mamlaka ya umeme.
Rais Ruto alitaja madai ya ufisadi kama sababu kuu, kufuatia mashtaka ya rushwa yaliyofunguliwa dhidi ya Gautam Adani, mmiliki wa kampuni hiyo, nchini Marekani.
Adani Group, moja ya makampuni makubwa nchini India, inawekeza katika sekta za nishati, miundombinu, na usafiri duniani kote. Mkataba wake na Kenya ulilenga kuboresha ushindani wa JKIA katika Afrika Mashariki.
Hata hivyo, mkataba huo ulikumbwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wafanyakazi waliogoma hivi karibuni, wakipinga mipango ya ubinafsishaji.
Madai ya zamani dhidi ya Adani Group yanahusisha ununuzi wa hisa kupitia makampuni ya nje, tuhuma ambazo kampuni hiyo imekana mara kwa mara.
Kwa sasa, Adani Group inaendelea kuwekeza Afrika, ikiwa na mkataba wa kuendesha bandari nchini Tanzania, huku wakosoaji wakiendelea kuibua maswali kuhusu uwazi wa shughuli zake.