Joto la Uchaguzi Mkuu mwakani, litakalohusisha ngazi ya urais, ubunge na udiwani, limepamba moto. Mmoja wa vijana, ambao wanaelekea moja kwa moja kuhitaji kulitumikia Taifa kisiasa ni Kennedy Elimeleck Ndosi, mtaalamu wa Ununuzi na Ugavi. Sifa kubwa ya Ndosi ni kutokukubali kushindwa kwa urahisi. Ni mpambanaji. Hii ni kwa sababu mtaalamu huyo wa ununuzi na ugavi ni mchapakazi. Ndosi ana ndoto za kuwa mbunge, na katika makala hii anajibu maswali katika mahojiano na mwandishi wa makala hii yaliyofanyika ofisini kwake, jijini Dar es Salaam…
SWALI: Wewe ni mtaaluma wa mambo ya Ununuzi na Ugavi, utaalamu ulioupata kwenye vyuo vinavyoheshimika. Unaweza ukapata kazi nzuri tu ya kitaaluma kuliko kuingia kwenye siasa?
JIBU: Kwanza niseme tu kwamba ninafurahi sana pia kuelezea nafasi yangu kama kijana wa Kitanzania na kokote nilipopita kuhusu kuonesha uwezo wa kuongoza watu. Kama tujuavyo yawezekana kiongozi ni wito au yawezekana ni karismati itolewayo na Mungu kwa binadamu…hapa nitaelezea historia yangu fupi ya uongozi tangu shule ya msingi, ambapo nikiwa Shule ya Msingi Mbweera nilichaguliwa kuwa kiranja wa Chakula na Usafi hadi nikamaliza darasa la saba nikiwa kiranja. Baada ya kuanza Shule ya Sekondari Uroki, mwaka 1999 nilichaguliwa kuwa Katibu wa Serikali ya Wanafumzi na nilihamia kwenda Kibohehe Sekondari ambapo niliteuliwa kuwa Mzee Mshauri wa jumuiya ya dini kwa wanafunzi Walutheri UKWATA;
Nilipoanza kusoma Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA). Unajua nilisoma hapa hapa. Katika ngazi ya stashahada ya juu ya ugavi na usimamizi wa vifaa yaani Advanced Diploma in Procurement and Supply nilichaguliwa kuwa kiongozi wa darasa kwa miaka mitatu mfululizo, ambapo niliongoza wanafunzi zaidi ya 650 hadi tulipohitimu mwaka 2008. Nikiwa Mzumbe niliweza kutengeneza Mfumo wa kutoa taarifa kwa kujitolea (Voluntary Information Manager) hadi tulipomaliza shahada ya uzamili (Masters). Nikiwa Chuo cha Diplomasia nilichaguliwa kuwa kiongozi wa Darasa (CR) ambapo nimewakilisha wanafunzi wenzagu 177 katika mambo mbalimbali ya kitaaluma.
Swali: Je, ni hayo tu yanayokushawishi kutaka kuingia kwenye siasa?
Jibu: Katika taasisi ninayofanya kazi (jina tunalihifadhi) mimi pia ni katibu wa cha wafanyakazi zaidi ya 80 ambapo ninawakilisha hoja zao kwa mwajiri, maoni na ushauri mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha maslahi ya utendaji kazi kwa ujumla. Katika nafasi hii ya Katibu nitatumika miaka mitatu ambapo uchaguzi mwingine utafanyika tena.
Swali: Serikali inashutumiwa kushindwa kuwaletea watu maendeleo na zaidi ya hapo ni kwamba inashindwa kufanya hivyo kwa wakati. Je, umejipangaje kukabiliana na changamoto hii?
Jibu: Mimi kama kijana wa Kitanzania ninaamini Serikali inajitahidi sana kadri ya uwezo wake kwani kwa kumbukumbu zangu sijawahi kuona hata siku moja ikishindwa kuwaletea maendeleo wananchi kwa wakati. Hapa ninamaanisha siyo kila kitu Serikali lazima ifuate mtu mmoja mmoja na kumpa mwanga wa kujiingizia kipato au kujikwamua kimaisha, bali ninaamini ni jukumu la mwananchi mmoja mmoja kuangalia fursa zilizo karibu naye na kuzitumia ipasavyo kujiletea maendeleo yake mwenyewe. Hivyo, kwa utashi wangu binafsi ninaamini Serikali inafanya kazi kubwa sana kuletea wananchi maendeleo.
Swali: Utagombea kata au jimbo gani?
Jibu: Ni mapema kutaja jimbo. Hii ni kwa sababu naheshimu taratibu na kanuni ambazo chama changu — Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejiwekea. Lakini kama ilivyo desturi, mimi kama kijana ninafarijika sana kuona vijana wanajitahidi na kufanya mengi sana katika siasa hasa Serikali ya Tanzania yetu hii ya CCM. Mfano wa vijana ninaowapenda wanavyotumikia wananchi ni Meya wa Ilala, Jerry Silaa, Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Mjumbe wa Bunge Maalum, Paul Makonda, Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba na kwa wanawake mfano Esther Bulaya, Shy-Rose Bhanji na Bonnah Kaluwa, ni baadhi tu ya vijana ninaoamini wote ni chachu kwangu (role models) ninaotamani kuwa kama wao siku moja na ninaamini kwa uwezo wa Mungu nitaweza, ila hao ni baadhi ya vijana, lakini viongozi CCM ni wengi sana ninaowakubali nikiwataja watazidi 50, kwa kifupi ni chama chenye viongozi thabiti na wenye uwezo wa hali ya juu.
Kwa kweli mimi ninapenda sana kutumikia wananchi na ndiyo maana baada ya kuanza masomo Chuo cha Diplomasia nimejitahidi kadri ya uwezo wangu na kuhakikisha tumefungua tawi la CCM la Chuo cha Diplomasia, kama ilivyo katika vyuo vingine vikuu nchini ambapo tawi hili lipo chini ya Mkoa Maalum wa CCM Vyuo Vikuu Tanzania. Katibu Mkuu wake ni Christopher Ngubiagai (MNEC) na Daniel Zenda wanaofanya kazi kubwa kukijenga chama. Ninaamini watafika mbali sana hawa viongozi wangu vijana na wachapakazi. Kwa sasa mimi ni Katibu wa tawi la kwanza la CCM Chuo cha Diplomasia na Mwenyekiti wangu ni Dk. Telesphory Kyaruzi.
Swali: Kwanini CCM na si vyama vinginevyo?
Jibu: CCM nimeipenda tangu nikiwa mdogo ambapo bibi yangu aliweza kutueleza mazuri yaliyofanywa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Hivyo nilianza kukipenda chama hiki na nilipokuwa mkubwa nilifuatilia kwa karibu na kuona CCM hadi sasa ndiyo chama pekee ambacho ninaamini kina sera zinazotekelezeka, chama chenye mfumo wa kitaifa, chama kisicho na upendeleo na ni chama pekee chenye mchanganyiko wa kada zote za Watanzania na makabila yao, pia ndiyo chama pekee kinachoheshimu utu, demokrasia na maadili.
Hadi sasa mimi kama katibu na mwenyekiti wa chama hiki tawi la Chuo cha Diplomasia tumeweza kuandaa kongamano la kitaifa kuhusu utelekezaji wa sera yetu ya mambo ya nje ndani ya miaka 13, lililofanyika Ukumbi wa Karimjee Julai 5, 2014 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali akiwamo Anna Tibaijuka, Ramadhani Madabida, Paul Makonda, Balozi Sokoine, Balozi mstaafu Ahmed Kiwanuka na Katibu mstaafu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kapteni Mohammed Ligora. Pia kwa sasa mimi kama Katibu wa CCM ambaye ndiye mtendaji wa kazi za tawi letu, nimefungua mtandao wa tawi letu unaojulikana kama www.ccmchuochadiplomasia.blogspot.com au CCM DIPLOMASIA BLOG ambapo kazi kubwa ni kuelimisha wananchi wa Tanzania na wana-CCM. Mimi pia ni mjasiriamali ninayefanya Network Marketing ya Forever Living kama njia ya kujiingizia kipato. Asante sana.
Swali: Tunaomba historia yako kwa ufupi?
Jibu: Nilizaliwa miaka 32 iliyopita katika kijiji cha Mbweera, Kata ya Msama Mashariki, wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro. Nilisoma elimu yangu ya msingi katika shule ya msingi Mbweera mwaka 1990-1996, baada ya hapo nilisoma shule ya Sekondari Uroki mwaka 1997-1999, nikahamia Kibohehe Sekondari mwaka 2000 na kumalizia kidato cha nne hapo. Baada ya kumaliza kidato cha nne nilijiunga na Taasisi ya Uhasibu (TIA) mwaka 2002 hadi 2004 nilipohitimu cheti cha Ugavi na Manunuzi yaani Pre-Foundation na Foundation Stage in Materials Management, ambapo pia ngazi hiyo ya mitihani ilisimamiwa na Bodi ya Ugavi na Usimamizi wa Vifaa (NBMM) ambayo kwa sasa ni PSPTB.
Elimu yangu ya juu niliianza mwaka 2005-2008 katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), na baada ya hapo nilifanya mitihani ya kitaaluma ya wataalamu na wasimamizi wa vifaa kwa ngazi ya juu kabisa yaani Certified Procurement and Supplies Professional of Tanzania (CPSP) (T) ambapo kwa uwezo wa Mungu nilifanya mara moja (single seat) mwaka 2008 na kumaliza na 2009 nilitunukiwa cheti hicho cha CPSP. Baada ya hapo nilipata ajira katika Taasisi ya Serikali ambapo nipo hadi sasa kama Afisa Manunuzi. Siku zote ninaamini penye nia pana njia, nilianza kusoma Shahada yangu ya Uzamivu (Masters) katika Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 2011 na nilihitimu 2013. Ninaamini ili ufikie malengo lazima uwe na uwezo wa kufanya vitu vingi na vyenye kugusa malengo yako ikiwamo utii, uvumilivu, kumuomba Mungu na bidii sana katika malengo yako.
Baada ya kupata Masters of Science in Procurement and Supply Chain Management kutoka Mzumbe, niliamua kukuza wigo wa upeo wangu kitaaluma, ndipo nikaanza kusoma katika Chuo cha Kimataifa cha Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia yaani Centre for Foreign Relations (CFR) au kama inavyotambulika na wengi ni Chuo cha Diplomasia. Pale nimesoma Postgraduate Diploma in Management of Foreign Relations (PGD MFR) ikiwa ni katika kutimiza ndoto zangu za kuwa msimamizi wa masuala ya uongozi na uhusiano wa kimataifa. Natarajia kutunukiwa cheti hicho mwezi Januari 2015.