Joto la uchaguzi nchini Marekani linazidi kupanda kufuatia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Novemba, mwaka huu huku kukiwa na ushindani mkubwa kati ya mgombea wa chama cha Republican na Democratic.

Wagombea wa pande zote mbili – Hillary Clinton wa Democratic na Donald Trump wa Republican – kura za maoni zinaonesha wanakabana koo kuwania nafasi hiyo muhimu.

Katika siku za hivi karibuni wagombea hao wamepambana vikali katika mdahalo wa kwanza, ambapo walitofautiana katika masuala mbalimbali ikiwamo masuala ya sera, kodi, ajira na uchumi ndani ya nchi hiyo.

Wagombea wote waliizungumzia vita ya Iraq na juhudi za kukabiliana na kundi linalojiita Dola ya Kiislam (IS) linalosadikiwa kuasisiwa na vita hiyo inayoendelea kugharimu maisha ya Wamarekani ndani na nje ya nchi hiyo.

Katika mdahalo huo, Hillary Clinton alimshutumu mpinzani wake kuwa amekuwa akikwepa kulipa kodi na kudokeza kwamba hilo lina maana kwamba Donald Trump hawezi kuwa na wanajeshi imara, pesa za kulipa wanajeshi waliostaafu pamoja na kufadhili elimu na huduma ya afya.

Katika kujibu hoja hiyo, Trump anasema atatoa hadharani taarifa hizo iwapo Clinton atakubali kutoa barua pepe takribani 33,000 ambazo zilifutwa kutoka kwenye akaunti yake wakati wa uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba alitumia akaunti binafsi ya barua pepe katika kazi rasmi alipokuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani.

Donald Trump pia alimlaumu  mpinzani wake huyo kuhusu kupotea kwa ajira, akisema nafasi za kazi ndani ya nchi hiyo zimekuwa adimu huku akilaumu mikataba duni ya kibiashara ambayo imeendelea kukandamiza nchi hiyo.

Tajiri huyo kutoka katika jiji la New York amesema akijitathmini, na uzoefu alionao kama mfanyibiashara, anatosha kabisa kuwa Rais wa Marekani kwa kile alichokieleza kuwa Marekani inamtaka kiongozi kama yeye katika kipindi hiki cha matatizo ya kupambana na ugaidi.

Kwa upande wake Clinton amemwelezea Trump kama mtu ambaye hana uwezo wa kuongoza Marekani kutokana na matamshi yake, ikiwa ni pamoja na kuwadhalilisha wanawake na kuwafafanisha na  nguruwe.

Idadi kubwa ya raia wa Marekani watakaopiga kura na walioutazama  mjadala huo wamesema kuwa  Hillary Clinton ndiye aliyeshinda katika mdahalo huo kwa kusema kuwa alikuwa na utulivu wa hali ya juu wakati wote wa mdahalo huo.

Wagombea hao watapambana tena katika midahalo mingine miwili kabla ya siku ya upigaji kura tarehe 8 Novemba katika sehemu itakayopangwa na waandaaji.

 Mdahalo huo uliandaliwa jijini New York huenda ukawa mdahalo uliotazamwa na watu wengi zaidi katika historia ya midahalo nchini humo. Watu zaidi ya milioni 100 inakadiriwa walitazama mdahalo huo.