Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia ,Chalinze

Kikundi cha bodaboda cha Kazikazi, Kata ya Lugoba ,Chalinze, Bagamoyo Pwani, kimekabidhiwa pikipiki kumi zilizogharimu milioni 30, kutoka Halmashauri ya Chalinze.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Hassan Mwinyikondo aliwaasa vijana kujiunga katika vikundi ili waweze kupata fursa mbalimbali za kuwezeshwa kirahisi.

“Vijana mjiunge katika vikundi halmashauri yenu kupitia asilimia kumi ina pesa za kutosha bila kujiunga mlawa na umoja hamwezi kunufaika na fursa hii”

Mwinyikondo alieleza, Halmashauri hiyo ipo vizuri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kuwezesha makundi ya vijana , wanawake na kundi maalum ,hivyo kinachotakiwa ni kuchangamkia kupata fedha hizo ili kujiinua kiuchumi.

“Hivi karibuni tumekabidhi gari ya abiria aina ya Costa yenye sh. milioni 70, kwa kikundi kimpha kilichopo Chalinze, tumepeleka pikipiki Msoga, Msata na maeneo mbalimbali, niwaombe vijana tuchangamkie kujiunga vikundi ili hii keki ya Halmashauri iwafikie kila kikundi” alihamasisha Mwinyikondo.

Mkurugenzi Ramadhani Possi alisema kuwa Halmashauri imepeleka pesa kwa ajili ya kukamilisha choo kilichopo jirani na ofisi ya Kata, ikiwa ni sehemu ya chanzo cha mapato katika kata hiyo.

“Mkikitumia vizuri hii michango midogomidogo haitowasumbua ikiwemo ya kununua umeme, bili ya maji na mahitaji mengine na kwamba kisiwe cha bure,” alisema Possi.

Katibu wa kikundi Cha Kazikazi,Muhsin Mpangala alieleza,kila siku wanajiwekea sh. 5,000 ambapo kwasasa Wana jumla ya shilingi milioni 2.5.