Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akitoa maelekezo kwa mkandarasi pamoja na wafanyakazi wake alipokagua vifaa vilivyopo katika karakana na mkandarasi huyo anayetekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vijiji vilivyo pembezoni mwa mji katika wilaya ya Tabora mjini, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani Tabora.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza na wakazi wa kijiji cha Katunda wilayani Uyui wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa usambazaji wa umeme vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili na kuwasha umeme katika kijiji hicho ,tarehe 26 Septemba 2023 mkoani Tabora.
Wakazi wa Kijiji cha Katunda wilayani Uyu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Judith Kapinga wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili na kuwasha umeme katika kijiji hicho, tarehe 26 Septemba 2023 mkoani Tabora.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza na Wakazi wa kijiji cha Katunda wilayani Uyui baada ya kuwasha umeme katika kijiji hicho, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili na kuwasha umeme katika kijiji hicho ,mkoani Tabora.
Vijana wakiendelea na kazi ya kusimika nguzo ili kuendelea kusambaza Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini mzunguko wa Tatu awamu ya Pili mkoani Tabora,
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga(kulia) na Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Almas Maige (kushoto) wakiwa kwenye mkutano katika kijiji cha Katunda wilayani Uyui, wakati wa ziara ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini mzunguko wa Tatu awamu ya Pili na kuwasha umeme katika kijiji hicho, mkoani Tabora.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO), mkoani Tabora wakati wa ziara ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini mzunguko wa Tatu awamu ya Pili na kuwasha umeme katika kijiji cha Katunda wilayani Uyui, tarehe 26 Septemba 2023 mkoani Tabora.
…………………………………………………………………………………………………………………………………
Zuena Msuya, na Theresia Lugwisha, Tabora
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema kuwa ifikapo mwezi Desemba mwaka huu, utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili katika vijiji vyote utakamilika na hivyo kupelekea kuanza utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme vitongojini.
Kapinga amesema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Tabora ambapo katika siku ya pili ya ziara yake amewasha umeme katika kijiji cha Katunda wilayani Uyui mkoani humo.
“Tunatarajia kumaliza kazi ya kusambaza umeme vijijini ifikapo mwezi Desemba mwaka huu, nawahimiza wakandarasi fanyeni kazi yenu kwa uadilifu mkubwa, hatuhitaji kukimbizana juu ya hilo kila mmoja atekeleze jukumu lake kwa maslahi mapana ya taifa letu”, alisema Kapinga.
Kapinga amewaagiza wakandarasi wote nchini kuhakikisha kuwa vifaa vya kufanyia kazi vinakuwepo wakati wote katika maeneo ya miradi ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo na hivyo kuukamilisha kwa wakati.
Pia, amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukagua vifaa vya wakandarasi ili kujihakikishia kama vipo vyote katika karakana zao ili kuhakikisha kuwa kazi zinafanyika kwa wakati na zinaendana na muda wa mkataba uliowekwa.
Vilevile, amewataka REA kuchukua hatua stahiki kwa wakandarasi wote watakaokwenda kinyume na makubaliano ya mikataba ya kupeleka umeme vijijini.
Kapinga amewaagiza REA kuendelea kuwasimamia wakandarasi kwa karibu kwakuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha fedha inazozitoa zinaenda kuwafikishia wananchi umeme kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri wa Nishati amewasisitiza wananchi kuendelea kusuka nyaya katika nyumba zao ili kujiweka tayari kuunganishiwa umeme pindi utakapowafikia katika maeneo yao na kwamba watu wote watafikiwa na umeme.
Pia alizungunza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Tabora na kuwaeleza kuwa watanzania wanataka umeme hivyo wafanye kazi kwa weledi, juhudi na maarifa usiku na mchana kuhakikisha watanzania wote wanapata umeme na kuwatatulia changamoto za umeme zinazowakabili wananchi hao.