Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Kibaha
Halmashauri ya Mji Kibaha ,mkoani Pwani imeanza utekelezaji wa mkakati kabambe wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ili kutoa fursa kwa jamii kushiriki kikamilifu shughuli za uzalishaji kujipatia kipato cha familia na Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Kitengo cha ustawi wa jamii Halmashauri ya Mji Kibaha ,Faustina Kayombo ameeleza mkakati huo kama sehemu ya mbinu mpya alizozipata Manispaa ya Kigoma Ujiji alipoambatana na Kamati ya kudhibiti UKIMWI kwenye ziara ya Mafunzo mwanzoni mwezi Septemba,2023
“Katika utoaji wa huduma ya kupinga ukatili wa kijinsia tutaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la jinsia na wadau wengine wakiwemo wananchi wenyewe ili kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto na watu wazima ikiwa ni pamoja na matusi,vipigo,ubakaji na ulawiti,utumikishwaji kwa watoto,kunyimwa haki ya kuhudhuria masomo na kufanyakazi sambamba na utelekezaji watoto”amesema Kayombo
Mhe.Lidya Mgaya diwani wa viti maalum ametoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye upingaji wa ukatili wa kijinsia ili kuiweka jamii salama
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhe.Mussa Ndomba amesema upo ukatili wa watu kudhulumiwa haki yao ya kumiliki Ardhi lakini na umekuwa ukiwaumiza hasa akina Mama lakini umekuwa hauzungumzwi Sana,hivyo ametoa wito kwa Afisa ustawi kulitazama kwa jicho la pekee
Ikumbukwe kuwa Kitengo cha Ustawi wa jamii hutoa huduma za kifamilia,Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto,Marekebisho ya tabia na haki za Watoto Kisheria,huduma kwa watu wenye ulemavu na Wazee,huduma ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto pamoja na Elimu ya msaada wa Kisaikolojia.