- Wananchi wahamasishwa kuchangamkia fursa
- Wamshukuru Rais Samia kwa programu hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Sawala amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi wa majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 kwa wananchi wa maeneo ya vijijini mkoani humo.
Ametoa shukrani hizo leo Januari 2, 2025 ofisini kwake mkoani Mtwara wakati wa utambulisho wa mradi na mtoa huduma atakayesambaza majiko hayo mkoani humo ambaye ni Kampuni ya Taifa Gas uliofanywa na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emanuel Yesaya.
“Tumepokea mradi huu ambao unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya na pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza mazingira na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi,” alisema Kanali Sawala.
Kanali Sawala alitoa wito kwa wananchi kuunga mkono jitihada za Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kununua majiko hayo ya ruzuku.
“Mhe. Rais anawapenda wananchi wake, ametuletea mradi nasi tuupokee na tumuunge mkono kwa kununua majiko haya ya ruzuku ili kulinda afya zetu sambamba na kuimarisha mazingira kama alivyoazimia,” alisisitiza Kanali Sawala.
Aidha, alitoa wito kwa REA na Taifa Gas kuhakikisha wanashirikiana na viongozi katika maeneo yote ili waweze kuufahamu mradi na hivyo kurahisisha utekelezaji wake.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mhandisi Yesaya alisema REA inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia 2024-2024 kupitia programu mbalimbali ili kufanikisha azma ya Serikali ambayo muasisi wake ni Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na lengo la kulinda afya za wananchi wake pamoja na kuhifadhi mazingira kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao unaelekeza ifikapo mwaka 2034; asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi kupikia,” alifafanua Mhandisi Yesaya.
Alisema jumla ya majiko ya gesi 16,275 ya kilo sita pamoja na vifaa vyake yatasambazwa katika wilaya tano za Mkoa wa Mtwara ambazo ni Mtwara, Masasi, Nanyumbu, Newala na Tandahimba ambapo kila wilaya itapata majiko 3,255 na mwananchi atalipia shilingi 19,500 tu na kwamba gharama nyingine imebebwa na Serikali.
Alisisitiza kuwa mtoa huduma atawajibika kusajili na kuandaa orodha ya wananchi watakaopatiwa majiko hayo. “Majiko haya yatauzwa kwa wananchi wenye vitambulisho vya NIDA au namba inayoweza kuhakikiwa; hakuna mwananchi atakayeruhusiwa kununua mtungi wa ruzuku zaidi ya mmoja,” alisisitiza.
Kwa nyakati tofauti wananchi mkoani humo walimshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi huo na waliahidi kumuunga mkono kwa kuendelea kuhamasishana na kuelimishana ili kufikia azma.