Leo ni Siku ya Wanawake Duniani. Kwa kawaida huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Usawa wa jinsia leo kwa maendeleo ya kesho’. Lengo likiwa ni kutambua mchango wa wanawake na wasichana duniani kote katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Sisi Gazeti la JAMHURI tunawarejesha katika historia kwamba siku hii imeanzaje? Kimsingi, imeanza mwaka 1908 kutokana na jitihada za wanawake 15,000 walipoandamana jijini New York, Marekani wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, malipo yanayoridhisha na haki ya kupiga kura. Mwaka mmoja baadaye Chama cha Kisoshalisti cha Marekani kikatangaza kuwa ni siku ya kwanza ya kitaifa ya wanawake.
Aidha, wazo la kuwa siku ya kimataifa lilianzishwa na Clara Zetkin, akaliwasilisha mwaka 1910 katika mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi wanawake Copenhagen, Denmark.
Katika mkutano huo kulikuwa na wanawake 100 kutoka nchi 17, wakakubaliana, na kwa mara ya kwanza ikasherehekewa mwaka 1911 nchini Austria, Denmark, Ujerumani na Uswisi.
Sherehe za 100 zilifanyika mwaka 2011. Siku hii ilianza kusherehekewa rasmi mwaka 1975 baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kuanza kuiadhimisha na baadaye kubuni kaulimbiu. Mwaka 1996 ilitolewa kaulimbiu ya kwanza iliyosema ‘Furahia yaliyopita, panga kwa ajili ya baadaye.’
Sisi JAMHURI tunafahamu kwamba siku ya kimataifa ya wanawake duniani ina jukumu la kutathmini maendeleo ya wanawake katika jamii kupitia siasa, uchumi, sayansi, afya, teknolojia, ujasiariamali, uongozi na sekta mbalimbali.
Kama hivyo ndivyo, tunashauri kaulimbiu ya mwaka huu ianze kutekelezwa kwa vitendo, kuanzia serikalini hadi sekta binafsi.
Kama ambavyo Katibu Mkuu wa UN, António Guterres, alivyopigia chapuo usawa wa kijinsia katika Siku ya Wanawake ya Machi 8, 2018 kwamba dunia inapaswa iwe mfano wa kufanikisha hilo.
Huo ndio ukweli, kwa sababu JAMHURI tunafahamu kwamba mfumo dume umeota mizizi kuanzia serikalini, mashirika ya kiraia na sekta binafsi na sasa vitendo vianze kuchukuliwa katika utekelezaji wa uwiano wa 50 kwa 50.
Pia katika utekelezaji wa uwiano huo tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo hapa nchini na kuendelea kuwateua wanawake wengine kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali yake akiwamo Dk. Stergomena Tax, aliyemteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Sisi JAMHURI tunaamini wanawake wakipatiwa uongozi ni rahisi kukabili vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kingono, kwa sababu usawa wa kijinsia ni faida kwa kila mtu, si tu kwa wanawake na wasichana, bali ni kwa yeyote ambaye maisha yake yatabadilika kutokana na dunia yenye usawa.
Kwamba, ni lazima kuwe na kizazi chenye usawa kinachojikita na masuala yanayowakabili wanawake na wasichana wa vizazi na vizazi.
Vilevile tunafahamu kwamba hakuna usawa kwa sababu baadhi ya wanawake katika maeneo mbalimbali hapa nchini wanateswa na kutiwa hofu ya mustakabali wao na wanakosa uvumilivu na hali hiyo imetawala maisha yao kwa muda mrefu.