Tume ya Katiba isikwaze
Wanasiasa na wanaharakati wanaokwaza utendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba tuwaogope kama ukoma, kwa sababu wengi wao wanatafuta maslahi yao binafsi na umaarufu usio na tija kwa Watanzania. Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji (mstaafu) Joseph Warioba, ni kiongozi mwadilifu tangu enzi za uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Mzalendo wa Tanzania, Dar
0689 916 970
Dola idhibiti wasambaza sms mbaya
Ninapenda kutumia nafasi hii kuviomba vyombo vya dola kujiwekea mikakati thabiti ya kudhibiti vitendo vya kusambaza ujumbe mfupi wa maneno (SMS) unaohamasisha chuki za wananchi dhidi ya Serikali. Watu wasioitakia mema nchi yetu wameendelea kutumia simu za mkononi kutuma ujumbe wa uchochezi.
Julius B. Bartholomew, Kigoma
Hongera JK umesema kweli
Kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuwataka wapinzani kuheshimu Bunge na kuacha kasumba ya kuandamana mara kwa mara kinastahili pongezi, kwani kinalenga kudumisha amani nchini. binafsi ninampongeza pia JK kwa kusema kweli kwamba madai ya wapinzani yanazungumzika, hivyo wajenge tabia ya kukutana katika meza ya mazungumzo kuyatafutia ufumbuzi.
Mpenda ukweli na uwazi
0784 478 462
Operesheni Kimbunga ije Tarime
Hiyo Operesheni Kimbunga iko katika mikoa ya Kigoma na Kagera tu? Huku Tarime mkoani Mara kuna wahamiaji haramu wengi kutoka nchi ya Kenya, na ndiyo chanzo cha wizi wa mifugo. Unakuta mtu ana miji mitatu; mmoja uko Kenya, mwingine Tarime na mwingine tena wilayani Serengeti. Kwa hali hiyo wizi utakwisha Tarime?
Magutu, Nyamongo – Tarime
0752 469 159
Wazawa wasiporwe ardhi yao
Baadhi ya wazawa hapa Tanzania wanadhulumiwa ardhi yao. Hivi kweli sisi tukitaka ardhi ya kuwekeza kule Marekani wananchi wa Marekani wenye eneo hilo wataondolewa? Jibu la haraka ni hapana. Watu weusi tunajidharau kabla hatujadharauliwa! Huo ndiyo uhuru tuliopigania?
Mpenda amani, Monduli – Arusha
0787 683 360
Toangoma tunahitaji umeme, maji
Wakazi wa Toangoma Masuliza kwa Kongowe Kigamboni, Dar es Salaam tuna kero ya ukosefu wa umeme na maji kwa miaka mingi ingawa tunaishi umbali wa kilometa 20 kutoka Ikulu. Kila siku tunaona nguzo za umeme zinapita kwenda kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda na vigogo wengine. Sisi pia tuhahitaji umeme na maji kama wao.
Msomaji wa JAMHURI
0683 040 080
Viongozi CCM waache unafiki
Tatizo sugu kwa baadhi ya viongozi wa Serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuona matatizo na kutaka kuyatatua kwa lengo la kujionesha tu kwa wananchi. Vyama vya upinzani vilishinikiza Waziri Kawambwa ajiuzulu, CCM na Serikali vikakaa kimya. Swali: Je, kimya chao ni tiba?
Mtanzania mzalendo
0787 683 360
Matapeli washughulikiwe ipasavyo
Uovu wa matapeli si tu umewaumiza wageni bali ukwasi wanaopata kutokana na utapeli wa kimataifa umekuwa ukitumika kupora haki na mali za Watanzania maskini. Tatizo hilo linahitaji juhudi na mbinu za ziada kulikabili, vinginevyo litaendelea kuwaumiza watu wengi.
Mpenzi wa JAMHURI
0712 559 087