Spika Job Ndugai, ametoa kauli inayohitaji kufanyiwa kazi na mamlaka zinazohusika.
Akizungumza wakati wa kuahirishwa Mkutano wa Bunge jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Spika Ndugai alishangazwa na namna baadhi ya watumishi wa serikali wasivyotulia katika makao makuu hayo ya nchi.
Amesema baadhi yao wamekuwa wakihamishia shughuli mikoani, hasa Dar es Salaam na huko hulipwa masurufu. Shaka yake ni kuwa Dodoma inatelekezwa.
Watanzania wameipokea kauli hii ya Spika kwa uzito na tafakuri ya kipekee, hasa ikizingatiwa kuwa aliyezungumza maneno haya ni kiongozi mkuu wa mmoja wa mihimili mitatu ya nchi.
Kwa uzito wake, hii si kauli ya kuachwa ipite hivi hivi bila kufanyiwa kazi na serikali pamoja na vyombo vyake. Kumekuwapo kauli kuwa baadhi ya maofisa waandamizi katika vyombo muhimu vya serikali wamekuwa wakihangaika wauziwe nyumba za serikali jijini Dar es Salaam, hali inayofifisha uwezekano wa wao kuwapo Dodoma.
Lakini pia matumizi ya serikali yamekuwa makubwa mno kutokana na safari za kila leo za viongozi waandamizi serikalini na katika vyombo vyake. Safari hizo ni za Dodoma – Morogoro – Dar es Salaam, na Dodoma – Arusha. Mzigo wote huu unabebwa na maskini walipakodi wa Tanzania ambao bado wanabeba malipo ya tozo mbalimbali.
Utitiri wa magari, hasa ya serikali kwenye barabara zinazotoka Dodoma, hauhitaji utafiti. Magari ya umma yanayosafiri ni mengi mno, na tunaamini si safari zote zinakuwa na tija kwa nchi na wananchi.
Serikali haina budi kuweka utaratibu unaoeleweka wa mafuta, vipuri na posho za watumishi ili kudhibiti safari zisizokuwa na tija.
Spika ni kiongozi mkubwa katika nchi, kwa hiyo tunaamini kauli yake imetokana na taarifa za kina na za uhakika zilizotoka katika mamlaka sahihi.
Uhamiaji Dodoma utawezekana tu endapo viongozi wakuu wataendelea kuwa mfano halisi wa watumishi waliokubali bila shinikizo kuishi na kufanya kazi Dodoma. Kwa maana hiyo tunatarajia kuona hata ugeni mbalimbali wa kitaifa ukibisha hodi Dodoma.
Dunia itatushangaa mno kuona Tanzania inaendelea kuwa na miji mikuu miwili inayowafanya watumishi wake wasitulie sehemu moja. Nigeria walipohamia Abuja kutoka Lagos, mpango wote walikuja kuuiga Dodoma. Leo wamefanikiwa sana. Abuja ndiyo makao makuu ya nchi hiyo. Haiwezekani wao wafanikiwe, sisi tufeli. Tukiamua Dodoma itakuwa mahali sahihi kuwa makao makuu ya nchi yetu.