Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt Hussein Mwinyi amesema serikali inatarajia kuajiri wastani wa vijana 6,000 waliopitia JKT kwa ajili ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Aidha amesema kujiunga na JKT kwa kujitolea, hakutoi uhakika wa kijana aliyejitolea kuajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Aidha, akijibu hoja zilizoibuka wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusu kuajiriwa kwa vijana wa JKT, Dk Hussein alisema vijana wanaojiunga na JKT kwa kujitolea wamekuwa wengi, hivyo kufanya uhakika wa kuajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa mdogo.
“Wale wachache wanaobahatika wataajiriwa, na wale ambao hawapati nafasi za ajira watapewa stadi za kazi ili wanapotoka kwenye mafunzo waweze kujiajiri.
Aliongeza: “ Wakati wa usaili kujiunga na JKT kwa kujitolea kwenye halmashauri zetu wanatakiwa kutambua hilo, kuwa si wote watakaoajiriwa kwa sababu ajira zinategemea na idadi ya nafasi za ajira zinazotolewa.”
Alisema vijana hao miezi sita ya kwanza hupewa mafunzo ya kijeshi na miezi sita mingine hupewa mafunzo ya stadi za kazi na kusisitiza kuwa vijana wanaokwenda kwenye mafunzo hayo wawe tayari kujifunza stadi za kazi ili waweze kujiajiri.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt Mwigulu Nchemba alisema Serikali iko katika mchakato wa kuajiri vijana waliopita JKT kwa ajili ya idara katika wizara yake.
Alisema kuwa wanaotaka kuajiriwa, kupeleka maombi kwenye kambi walizohudhuria mafunzo au kujitolea. “Tunataka kuajiri na vijana kwa ajili ya idara zetu ikiwa ni wale waliojenga ukuta wa Mirerani na wengine ni kwa wale waliohitimu kwenye makambi mbalimbali ya JKT.
Aliongeza: “ Kwa idadi tuliyopewa ni zaidi ya vijana 1, 500 kwa upande wa Jeshi la Polisi, 1,500 Uhamiaji, vivyo hivyo kwa idara ya Magereza na upande wa Zimamoto, wote tunatarajia kuwapata kutoa JKT.”
Aidha, Mwigulu alisema Jeshi la Polisi na idara zake havijashindwa kazi ya kukabiliana na uhalifu na kusisitiza kuwa hawaombi wahalifu kuacha kufanya uhalifu, ila watakabiliana nao na kuhakikisha uhalifu hautamalaki hata kwenye mtaa moja nchini.
Akijibu hoja ya kuwa tangu kuondolewa maduka kwenye makambi ya Jeshi, hakuna posho yoyote ambayo askari hao wamepewa, Dk Hussein alisema maduka hayo yalikuwa na kasoro nyingi, ikiwa ni pamoja na waliokuwa wakiyaendesha kuuza bidhaa ambazo hazijalipiwa ushuru nje ya makambi na malalamiko ya askari ya bei kubwa ya bidhaa.
Alisema kwa sasa wanaangaliwa uwezekano wa maduka hayo, kuendeshwa na jeshi lenyewe ili kuondokana na kasoro hizo, lakini wakiwa wanasubiri utekelezaji wa hilo, kila mwanajeshi hupewa Sh 100,000 kama fidia kila mwezi.
Akichangia kujibu hoja hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema serikali iliamua kuondoa msamaha wa kodi kwenye maduka hayo ili motisha hiyo iwanufaishe walengwa na si baadhi ya askari.
Alisema kwa upande wa Ngome mpaka kufikia Machi posho ya kufidia kwa msamaha wa kodi, Serikali imetoa Sh bilioni 63.59 na kwa JKT ni zaidi ya Sh bilioni 5.