Mombasa
Na Dukule Injeni
Hakuna ubishi, urais Kenya ni mbio za farasi wawili licha ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kupitisha majina manne ya wanaosaka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 9, mwaka huu.
Naibu Rais, William Ruto wa muungano wa Kenya Kwanza na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance ndio wanaochuana vikali.
Wengine wawili ambao wanatamba kuwapa wakati mgumu Odinga na Ruto debeni ni Profesa George Wajackoyah wa Chama cha Roots na David Wahiga wa Chama cha Agano.
Hata hivyo ni Wajackoyah ambaye amegonga vichwa vya habari tangu aweke wazi nia ya kuwania urais kisha kuchukua fomu na kuidhinishwa na IEBC.
Mgombea huyo wa Chama cha Roots amejizolea umaarufu hususan kwa kutetea ulimaji wa bangi na kusema endapo atachaguliwa Agosti 9 atatumia zao la bangi kuiingizia Kenya fedha nyingi za kigeni atakazozitumia kulipa madeni.
Lakini cha kushangaza ni kauli aliyoitoa hivi karibuni akiwa Kisumu ambayo ni ngome ya Odinga na kuibua maswali kama kweli Wajackoyah ana nia ya dhati kuwania urais au ni mradi wa Odinga?
Akiwa kwenye kampeni zake eneo la Kondele jijini Kisumu, Profesa Wajackoyah alidokeza mpango wa siri alioingia na Odinga ambapo miongoni mwa mambo mengi ni kuwa yeyote atakayeshinda atafungua milango ya serikali yake kwa mwingine.
Je, kuna uwezekano wa uwepo wa makubaliano kabla na baada ya uchaguzi kati ya mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Odinga, na mwenzake wa Chama cha Roots, Wajackoyah?
Ukiacha umaarufu walionao Ruto na Odinga, uwepo wa Wajackoyah na hususan kauli zake zimewachanganya wengi wasijue kama yeye ni mradi wa Odinga au mwanasiasa aliyekuja kuvuruga na kuwaharibia vinara wawili kwenye uchaguzi hivyo kuwanyima ushindi raundi ya kwanza.
Kauli ya Wajackoyah tena akiwa katika ngome ya Odinga imetafsiriwa ni ya kisiasa, yenye nia ya kuwashawishi wapiga kura wamsikize, ukizingatia alidai anamsafishia njia Odinga kutinga Ikulu.
Alikwenda mbali na kusema ametumwa na Odinga kuwasilisha ujumbe kwa wafuasi wake na kudokeza kuhusu uhusiano wake na waziri mkuu huyo wa zamani, ikiwamo uwezekano wa wawili hao kufanya kazi pamoja katika siku za usoni.
Kiongozi huyo wa Chama cha Roots pia alisema ushindi uwe wake au wa Odinga utakuwa ni ushindi kwa watu wa Magharibi mwa Kenya.
Wajackoyah ambaye ni wakili kitaaluma, alidai alikuwa muonja chakula mkuu wa Makamu wa Rais wa Kwanza, marehemu Jaramogi Oginga Odinga.
“Nitakaposhinda urais, nitakaa na Odinga katika chumba cha mkutano nikiwa na lengo la kufanya kazi naye baada ya uchaguzi,” amesema kiongozi huyo wa Roots Party ambaye mgombea mweza wake ni mwanamke Justina Wamae.
Wajackoyah katika mkutano huo kwenye kambi ya Odinga, alimtetea waziri mkuu huyo wa zamani, akiwataka wale wanaoendekeza kumshambulia kiongozi huyo wa Chama cha ODM kuacha.
Aliyekuwa analengwa na Wajackoyah ni Naibu Rais, Ruto, na imekuwa kawaida kwa kiongozi huyo wa Roots Party katika mikutano yake ya kampeni kumkosoa Ruto zaidi ya Odinga.
“Nimekuja nyumbani kwa baba na nikiwa njiani kuja hapa, niliambiwa kuwa kama utakwenda Kisumu, usimtukane Raila kwa sababu nitapata wakati mgumu. Kuna huyu kijana mmoja kutoka Sugoi (akimaanisha Ruto), ambaye imekuwa kawaida yake kumtukana baba akija hapa. Mpigieni kelele, mumwambie aachane na baba anapokuja hapa,” amesema.
Wajackoyah amesema aliamua kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa Agosti 9, mwaka huu kupitia Chama cha Roots baada ya juhudi zake kujiunga na vyama vikuu kama vile ODM, ANC na Ford-Kenya kukataliwa.