Si mara moja wala mbili kupitia safu hii ‘Fasihi Fasaha’ niliwahoji na kuwataka fikra Watanzania wenzangu, je, wakati umetimu kwa vyama vya siasa vya upinzani kupewa ridhaa ya kushika dola kupitia sanduku la kura?

Nilifanya hivyo kutaka kujiridhisha baada ya kukiri, kukariri na kuheshimu kauli za viongozi wawili ambao ninawahusudu na kuwajaza moyoni mwangu, kutokana na maneno na vitendo vyao vya ukweli ndani ya medani za siasa. 

Hao ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Kepteni wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Ukiwaona Ditopile Mzuzuri. Wote ni marehemu.

Mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alipokuwa akimnadi mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benjamin William Mkapa, katika mikoa ya Rukwa, Mbeya na Iringa, aliwaambia Watanzania kuwa hakuna chama chochote cha upinzani ambacho kingeweza kushika dola kwa wakati ule.

Aliendelea kusema kuwa vyama vile vilikuwa vichanga, havikuwa na nguvu na kuishinda CCM. Hata mwaka 2000 visingeweza. Alisema kuwa labda labda mwaka 2015.  Kwa hiyo, matarajio yangewekwa mwaka huu.

Mwaka 2000, Kepteni Ditopile akiwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, akiwanadi wagombea ubunge katika majimbo ya mkoa huo pamoja na mgombea urais katika muhula wa pili wa Mh. Benjamin Mkapa, alisema kuwa vyama vya upinzani ni vichanga, havina nguvu wala uwezo wa kuongoza nchi.

Ditopile akiwa katika mikutano ya hadhara vijijini na mijini, alilinganisha uwezo wa vyama hivyo kuwa sawa na watoto wa shule za msingi kuwa hawawezi kufanya kazi kama vile za kulima mashamba makubwa, kutunza familia, kuhudumia jamii n.k., vivyo hivyo vyama vya upinzani havina elimu ya kutosha ya siasa, jamii na uchumi kuweza kuongoza na kutawala watu.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Lindi aliwahamasisha wananchi na kuwaeleza vyama hivyo vinacheza mchezo wa madangi na ngoma yao wachezayo haikeshi; ni ya kitoto. Kauli ya Ditopile na kauli ya Mwalimu Nyerere mara kwa mara hunitia katika udodosaji, ni kweli wayasemayo?

Viongozi hao wanazungumzia yafuatayo. Mosi, mwaka 1995 vyama hivyo vilikuwa kweli vichanga mno kwa maana ya kuanzishwa mwaka 1992. Hawakuwa na viongozi wengi na madhubuti wa kuweza kushawishi na kuhamasisha wananchi kujiunga na vyama vyao ili kuipiku CCM.

Pili, havikuwa na uwezo wa kupambana na kuvunja itikadi ya CCM ya Ujamaa na Kujitegemea kwa wanachama wake walioshamiri kuanzia vijijini hadi mijini chini ya mfumo na umoja wa wakulima na wafanyakazi ndani ya Ujumaa ni Imani.

Tatu, idadi ya watu na rika za watu waliofuata itikadi za vyama vya upinzani ilikuwa ndogo ikilinganishwa na ile ya watu wa CCM. Hii ina maana kuwa vijana, watu wazima na wazee wengi walikuwa na mapenzi makubwa juu ya CCM kuliko vyama vya upinzani.

Hayo yote yalionekana katika chaguzi za mwaka 2000 na 2005. CCM ilivyosononesha vyama vya upinzani na kuvigaragaza. Chenyewe kikishinda kwa kishindo. Mtikisiko kwa CCM ulianza kuonekana katika uchaguzi wa mwaka 2010. Vyama vya upinzani vilipojitutumua na kupeleka salamu kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

CCM imetimiza miaka 38 (1977-2015) na vyama vya upinzani vimetimiza miaka 23 (1992-2015). Vyama vyote vimekua na vimekomaa. Kama vingekuwa ni binadamu leo wangekuwa wameoa au kuolewa. Wana watoto na uwezo wa kufanya kazi na kuhudumia jamii. Hawachezi tena madangi na ngoma yao inakesha.

Ukweli huo tumeuona mwezi uliopita katika uchaguzi wa Oktoba 25, vyama vya upinzani vilivyoipeleka mchakamchaka CCM. Hata hivyo, kutokana na ukomavu na kupendwa kwake na Wananchi, CCM imeshinda kwa asilimia 58 na kuvibwaga vyama vya upinzani kwa kupata jumla ya asilimia 39 na ushei.

Nini kimetokea? Vijana wengi walijiandikisha na kupiga kura wakijivunia asilimia yao 57. Hawa ni wale waliozaliwa wakati vyama vingi vilianza 1992. Wamezaliwa, wamelelewa na wamekuwa ndani ya mfumo vya vingi na kuamini itikadi mbalimbali za vyama.

Vijana hao wamechambua na kupima itikadi za vyama vyote vya siasa na kuweza kuamua la kufanya. Watu wazima na wazee walitafakari na kuchambua misimamo ya vyama na maadili ya viongozi katika uwezo wa kuongoza. Wake kwa waume wakatumia haki yao ya kidemokrasia na kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi.

“Labda labda mwaka 2015” ya Mwalimu Nyerere imeonekana. Laiti vyama vya upinzani (Ukawa) vingetumia kete zake mbili za awali UFISADI na KATIBA YA WANANCHI huenda leo tungezungumza vinginevyo. Lakini kwa kuacha kete zao na kuvamia kete za maleteo ya “hakuna kilichofanyika miaka 54 “ wamekwenda na maji. Kauli ya Mwalimu Nyerere bado inatinga.

“Vyama vya upinzani havina elimu ya kutosha”. Kauli ya Kepteni Ditopile imejichomoza katika uchaguzi huu. Vyama vya upinzani (Ukawa) kuacha ajenda yao ya KATIBA YA WANANCHI na kukumbatia mabadiliko yasiyokuwa na maelezo ya kukidhi, wametupwa nje.

Mwaka 2020 hauko mbali penye uhai na majaaliwa. CCM ina kazi kubwa na nzito ya kuwapa imani wananchi ya kurekebisha mfumo uliopo na kurejesha mfumo wenye itikadi ya CCM. Hata vyama vya upinzani vina kazi ya kuwarudisha wanachama wao na kuwajaza kasumba na itikadi yenye nguvu ya kuiondoa CCM madarakani. Kusema rahisi kutenda shughuli.