majaliwaPaulo Sozigwa, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa Katibu wa Rais Julius Kambarage Nyerere, anakabiliwa na hali ngumu kimaisha.

Sozigwa, ambaye kwa sasa anaumwa ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (Alzheimer), anaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu, akisaidiwa na familia yake na wasamaria wema. 

Kutaabika huko kumechangiwa na kutopata malipo ya kiinua mgongo na pensheni, kwa kile kinachoelezwa kwamba ni kutokuwapo kumbukumbu zake za kiutumishi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ofisi Binafsi ya Rais hadi serikalini ambako aliwahi kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Habari na Utalii.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanywa na JAMHURI nyumbani kwake Magomeni Mapipa, Dar es Salaam, mke wa Sozigwa, Monica Kuga, anasema hali yao uchumi ni mbaya kiasi cha kumfanya amtunze mumewe kwa misaada kutoka kwa jamaa na watu waliomfahamu vizuri enzi za utendaji kazi wake.

Wakati Mama Kuga akisema kinachowataabisha ni kukosekana kwa mafao na pensheni, baadhi ya watu waliozungumza na JAMHURI wanasema, kilichomponza mwanasiasa na mtangazaji huyo mahiri wa redio, ni kazi yake aliyoifanya akiwa katika Kamati ya Maadili ya CCM.

“Ndani ya chama (CCM) hakuna asiyejua kazi iliyofanywa na Mzee Sozigwa na mwenzake Kanali mstaafu, Abdi Mhando, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

“Aliandaa ripoti kali kweli kweli ambayo pamoja na yote yaliyoainishwa, ilitupwa pembeni na Mwenyekiti wa wakati huo (Benjamin Mkapa). Ile ripoti ingezingatiwa, Kikwete (Jakaya) asingepitishwa kuwania urais,” kinasema chanzo chetu.

Inaelezwa kuwa kutokana na ripoti hiyo, ‘malipo’ aliyoyapata Sozigwa ni ‘kutelekezwa’ kwa kila namna, hali ambayo imeendelea hadi sasa akiwa anaishi kwa dhiki.

“Nguvu ya wanamtandao ilikuwa kubwa – kwa ushawishi na kwa fedha – wote tulikuwa mashuhuda. Kilichofuata baada ya watu hao kuingia madarakani, ni kutupwa kwa Sozigwa, Kanali Mhando na Mangula. Matokeo ya mtandao huo yaliathiri watu wengi waliokuwa ndani na nje ya chama hasa wale walioonekana kuwa tofauti na mtandao wenyewe, wengi wao walijikuta katika wakati mgumu katika kipindi chote cha miaka 10,” kimeongeza chanzo chetu.

Mama Kuga anasema licha ya Sozigwa kuitumikia Serikali kwa miaka zaidi ya 30 akiwa kiongozi mwandamizi, mchango wake haujathaminiwa.

“Kwa wale waliokuwa watu wazima katika miaka ile ya 1970, watakuwa wanakumbuka umahiri wa mzee huyu katika kipindi cha Mazungumzo Baada ya Babari. Akiwa Mkurugenzi RTD (Redio Tanzania Dar es Salaam), alianzisha kipindi kilichojulikana kama ‘Mikingamo’, aliamini ubepari ni unyama na kweli Mzee Sozigwa hata baada ya kusambaratika kwa siasa ya Ujamaa ameendelea kuishi kama mjamaa. Aliamini katika Ujamaa wa kweli ndiyo maana hakuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali… imani yake katika Ujamaa ndiyo iliyomfanya Mwalimu Nyerere amwamini katika shuguli zake.

“Nakumbuka mwishoni mwa miaka ya 1990, akiwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alienda Bukoba kwa shughuli za kikazi. Paul Kimiti, wakati huo akiwa ni Mkuu wa Mkoa, alimtumia gari ya kwenda kumpokea melini, dereva alipomtafuta katika vyumba vyote vya daraja la kwanza hakumpata, akarudi na kuripoti kwa bosi wake kuwa mzee hakuja; kumbe alisafiri katika chumba cha daraja la tatu,” anasema Kuga.

Anasema baadaye wakati wakinywa chai pamoja, yule dereva alikuja kuomba msamaha huku akijitetea kuwa alikuwa amepita kwenye vyumba vyote vya daraja la kwanza lakini hakumuona, hali iliyosababisha aamini kuwa huenda hakuja. 

“Alichomjibu mzee yule ni ‘wewe nani alikwambia kuwa chama kina fedha za kupoteza kwa kusafirisha watu daraja la kwanza?’ Aliyasema hayo miaka mingi baada ya Azimio la Zanzibar kuiweka CCM katika njia ya ubepari,” anasema.

Sozigwa anakumbukwa kwa umahiri wake katika utangazaji wa redio. Wakati wa Vita ya Kagera, baada ya vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuteka Jiji la Kampala, ni yeye aliyekuwa mstari wa mbele kutangaza habari hizo za ukombozi kwa raia wa Uganda.

 

Ahangaikia mafao

Sozigwa anadai mafao kutokana na utumishi wake serikalini na katika CCM. Hata hivyo, kumekuwa na sintofahamu ya namna mkanganyiko wa mafao yake ulivyojitokeza, kwani kuna maeneo ambayo hakuna rekodi zinazomtambulisha kama mmoja wa watu waliowahi kuajiriwa sehemu hizo.

Wakati fulani alielezwa kuwa faili lake wakati akiwa RTD lilipelekwa Hazina kwa ajili ya kuandaliwa malipo, lakini huko aligonga mwamba.

Mama Kuga anasema walishafika hadi Ikulu, wakatakiwa wapeleke nyaraka mbalimbali za kuthibitisha utumishi wake. Walifanya hivyo, lakini anasema baadaye nyaraka hizo waliambiwa zimepotea katika mazingira yasiyoeleweka.

“Tulipeleka nyaraka Ikulu, tulipeleka salary slip na nyaraka nyingine na kukabidhiwa kwa Mhasibu wa Ikulu, anayeitwa Joseph Sanga.

“Mwaka 2011 tulimuona Sanga na alitutaka tuache nyaraka zetu na turudi baada ya siku tatu atakuwa ameshughulikia, lakini tulipokwenda kwake tulielezwa kuwa faili letu limepotea,” anasema Mama Kuga.

Anasema waliendelea kufuatilia suala hilo hadi Hazina ambako hawakuweza kupata msaada wowote.

Anasema mwaka jana walifika Ofisi ya Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kumuona Waziri Celina Kombani (marehemu), kwa ajili ya kupata ufumbuzi, lakini Kombani alifariki dunia akiwa anaendelea kushughulikia suala hilo.

Anasema Kombani aliwasiliana na Hazina ambako walielezwa kuwa mafao ya Mzee Sozigwa yalishalipwa muda mrefu, ila kilichokuwa hakijafanyika ni kuanza kulipwa pensheni ya kila mwezi.

“Baada ya kufa kwa Celina Kombani ni kama tumebaki yatima kwani pamoja na kuendelea kuhangaikia suala hili hadi kufika Ikulu, kote huko ni kama tumegonga mwamba,” anasema Mama Kuga.

Anasema mwanzoni mwa mwaka huu, walifika Utumishi na kumuona Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki.

Kwa mujibu wa Mama Kuga, Waziri Kairuki alishangazwa na taarifa za Mzee Sozigwa kutopata stahiki zake.

“Angella alitupokea vizuri, akaahidi kutusaidia kutatua suala hili, tukamwachia barua zetu, lakini tuliporudi mara ya pili Katibu wake  Muhtasi akasema barua hizo hazioni kwani aliyekuwapo mwanzo alibadilishwa. Ilitulazimu kuandika nyingine. Lakini pia Waziri alionekana kusita kumsaidia mzee kutokana na mambo yaliyowahi kuandikwa kwenye mitandao,” anasema Mama Kuga.

Machi 15, mwaka huu walimwandikia barua Waziri Kairuki kumkubushia malipo ya pensheni ya Mzee Sozigwa.

Sehemu ya barua hiyo inasomeka: “Tulifika ofisini hapo baada ya kuambiwa jalada la Mzee Sozigwa la RTD lilipelekwa Utumishi, wakati ndugu Kasekwa wa Hazina alipokuwa akifuatilia suala la pensheni ya mzee tokea Ikulu. Hii ni hatua iliyotulazimu na mzee tufuatilie tujue tatizo limefikia wapi ndiyo ujio wetu wa awali kwako. Naomba ofisi yako iliangalie suala hili kwani mzee amechoka, hata na mimi najisikia kuchoka.”

JAMHURI imemtafuta Waziri Kairuki mara kadhaa bila mafanikio.

Mara ya kwanza alisema: “Naomba unipigie saa 11”. Alipopigiwa muda huo alieleza kuwa yuko kwenye vikao. Na alipotafutwa tena simu yake haikuwa ikipatikana.

Kwa upande wake, Sanga anasema nyaraka alizoachiwa na Mzee Sozigwa na mkewe alizikabidhi kwa wahusika ambao, kutokana na kuwa suala lenyewe ni la muda mrefu, hawakumbuki.

Hata hivyo, anasema baada ya kufikishiwa suala hilo, alifanya juhudi za kupata nyaraka za utumishi wa Mzee Sozigwa Ikulu, bila mafanikio.

“Hajawahi kuwa mfanyakazi wa Ikulu, hawa watu wanachanganya mambo, yeye aliletwa hapa na Rais kutokea kwenye chama kama ambavyo huwa inafanyika, kwa makubaliano ambayo hayamfanyi kuwa mfanyakazi wa Ikulu moja kwa moja. 

“Alikuwa mfanyakazi Ofisi Binafsi ya Rais, hiyo pekee haikutosha kumfanya kuwa mtumishi wa Ikulu kwa sababu hakuna nyaraka zake ambazo zingeweza kutumiwa na Hazina kumlipa mafao.

“Niliwashauri waende kwenye misingi ya ajira, nani alimwajiri? Hazina wanalipa kwa documents, kama anazo naamini atalipwa lakini inavyoonekana ni kwamba hana. Kama hana nyaraka sidhani kama anaweza kulipwa hivi hivi tu, sidhani,” anasema Sanga.

Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, ameiambia JAMHURI kuwa Sozigwa ni miongozi mwa viongozi waadilifu waliotoa mchango mkubwa nchini.

Anasema Mzee Sozigwa alifanya kazi kubwa ya kuisaidia nchi kupata Uhuru pamoja na kusimamia misingi ya nidhamu ya chama na wanaCCM kwa jumla.

“Siwezi kutoa kauli mpaka nimuone na nifuatilie hiki ulichoniambia, ila nitafuatilia kwa kina kujua tatizo lipo wapi pamoja na kuhakikisha anapata haki zake haraka bila usumbufu. Haiwezekani watu wanaoitumikia nchi kwa uadilifu wa kiwango chake wapate shida kama unavyosema.

‘Nafahamu Sozigwa alikuwa Msaidizi wa Mwenyekiti Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama na Mwenyekiti wa Nidhamu ndani ya chama. Alikuwa ni mtu wa misimamo, hayumbishwi,” anasema Sendeka.

Sendeka alizungumza na JAMHURI akiwa safarini Iringa, na akaahidi kwenda kumuona Mzee Sozigwa mara atakaporejea Dar es Salaam.

“Nitaenda kumuona pamoja na kupata ufafanuzi wa kina kuhusiana na kuteseka kwa kukosa mafao yake,” amesema.

 

Ugonjwa

Mama Kuga anasema Mzee Sozigwa alianza kuugua ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu kuanzia mwaka 2008.

Mwaka 2009 Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, alimsaidia matibabu nchini Finland. Alitakiwa arejee Finland kwa matibabu, lakini alishindwa kutokana na kukosa fedha.

Mama Kuga anasema kwa sasa hali ya Mzee Sozigwa si nzuri, kwani kwa siku analazimika kutumia ‘pampasi’ kadhaa kuzuia haja ndogo ambayo imekuwa ikimtoka kila mara. Kasha lenye pampasi sita bei yake ni Sh 25,000.

“Kwa kawaida pampasi za watu wazima ni gharama kubwa sana na inalazimika kutwa atumie tatu, hali ambayo inaendelea kuwa ngumu kwetu kuweza kuimudu,” anasema Kuga.

 

Mwito kwa Serikali

Mama Kuga anaiomba Serikali ya Awamu ya Tano imsaidie Mzee Sozigwa, kwa kuhakikisha anapata mafao na pensheni ili fedha hizo zimsaidie kumtunza.

“Kama unavyoona, tumegeuka ombaomba kana kwamba hatukuwa watumishi ndani ya Serikali, tunaishi kwa kutegemea hisani kutoka kwa wasamaria wema na pensheni kidogo ninayoipata mimi,” anasema Mama Kuga.

Anasema ana imani taraifa hii ikimfikia Rais Magufuli, atachukua hatua stahiki za kumsaidia mumewe.

Sozigwa (83), alizaliwa mwaka 1933 katika Kijiji cha Kidunda, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Minaki na kuhitimu darasa la nne. Alijiunga na Shule ya Kati ya Mpwapwa mkoani Dodoma kabla ya kwenda Tabora Boys. Baadaye alijiunga Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda ambako alitunukiwa Shahada ya Uchumi.

Mwaka 1959 aliteuliwa kuwa Ofisa Tawala, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe. 

Kuhusu Mwalimu, Sozigwa amewahi kuhojiwa na kusema: Nilimfahamu Mwalimu, nilifanya naye kazi. Sikuomba niwe Katibu wake. Aliniteua mwaka 1967, siku chache kabla ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Wakati huo nilikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Utalii. alisema, “Njoo, kuna nafasi na wewe utakuwa msaidizi wangu.’ Nikasema, ‘Sawa. Asante Mungu’.’’ Nikaripoti na huo ukawa mwanzo wangu kuwa na Mwalimu. 

Sikuwa na ujuzi wowote wa kazi ya ukatibu wa Rais. Mimi nilifuzu uandishi wa habari. Nilisomea Syracuse, New York na kutumia mwaka mmoja katika Chuo Kikuu cha London. Kwa hiyo, kwa jumla nilikuwa mwandishi wa habari, lakini si katibu wa rais. Nilipoenda Ikulu kuwa Katibu wa Rais, nilipaswa kujifunza. Ilikuwa rahisi sana kufanya kazi na Mwalimu Nyerere. Alikuwa mwalimu mzuri, alikuwa msikivu. 

“Aliweza kuvumilia ujinga wako na kukufundisha. Yeye alinifanya mimi niwe nilivyo sasa (umahiri wa kazi). Kwangu mimi, yeye ni kiongozi mnyenyekevu sana – sana, mnyenyekevu sana na alikuwa tayari kujifunza kutoka kwa mtu yeyote, kitu chochote.”

Mwaka 1960 Sozigwa alifunga ndoa na Monica Kuga, na wana watoto wanne.