Na Eleuteri Mangi, WUSM Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu ametoa tuzo UNI AWARDS na kusisitiza kuwa Serikali inashirikiana na taasisi za kifedha za benki ya CRDB na NBC na wafadhili wengine ndani na nje ya nchi kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania ili kukuza na kuendeleza kazi za Sanaa nchini.
Akizungumza katika tamasha la utoaji tuzo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu na vya kati la UNI AWARDS Agosti 5, 2023 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Bw Yakubu amesema Serikali ina Mipango kabambe ya kuendeleza tasnia ya sanaa nchini ikiwemo wasanii kazi zao.
“Sasa ni wakati muafaka wa kuwajulisha Mhe. Rais ametupatia Sh Bilioni. 2.5 kwa ajili ya kuwasaidia wadau ambao wana maandiko na vipaji vya Sanaa ili kuviendeleza, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania unaendeshwa kisayansi, peleka wazo lako hapo utasaidiwa liwe andiko ambalo unaweza kupata mkopo.
Sasa benki za CRDB na NBC wanaongeza fedha na tumepata wafadhili wengine kutoka nje ya nchi ambao nao wanaongeza fedha.
Kwa hiyo mtu yeyote mwenye uwezo wa jambo lolote la Sanaa na hana hela ya kutekeleza wazo lake, basi Mfuko ni kimbilio lako” amesema Katibu Mkuu Bw Yakubu.
Katibu Mkuu Bw Yakubu amesema kuwa hadi sasa mfuko huo tayari ulishatoa mikopo ya Sh. Bilioni 1 na hivi karibuni zinatarajiwa kutolewa Sh. bilioni 1.4 na Sh. bilioni 2.4 zitafuata muda sio mrefu na kusisitiza kuwa mfuko huo ni mahali pa kuinua na kuendeleza vipaji na kazi za Sanaa nchini.
Aidha, Katibu Mkuu Bw Yakubu ameongeza kuwa kwa upande wa filamu, Serikali inashirikiana na Korea kutoa mafunzo ya kozi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa filamu na kuwasihi washiriki wa tamasha la UNI AWARDS kwenda Bodi ya Filamu kupata utaratibu wa namna ya kujiunga ambapo kwa sasa wapo vijana 15 wanapata mafunzo hayo.
“Kwa kutambua kwamba mmekuwa ‘consistent’ na mmegangamara miaka mitano kufanikisha jambo hili mpaka mmefika hapa, Serikali itawaunga mkono kwenye tamasha lijalo kwa kutoa Sh. milioni 50 ili tamasha lifanyike kwa mafanikio zaidi. Kwa hiyo tuwe pamoja, tushirikiane.
Hili ni tamasha ambalo Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaliunga mkono, vijana kukusanyika katika sehemu hii kutambua vipaji vya wenzao, ni kitu ambacho tunakiunga mkono” amesema Katibu Mkuu Bw Yakubu.
Tamasha la tano la UniAwards linaongozwa na kaulimbiu inayosema “Pinga Ukatili wa Jinsia” na historia ya tamasha hilo imeanzia mwaka 2019 tangu kuanzishwa kwake kwa lengo la kuinua na kuendeleza vipaji kwa wanafunzi wanasoma vyuo vikuu na vya kati nchini