Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, hatimaye amesalimu amri na kurejesha gari, mali ya Serikali alilojimilikisha akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa, Kanda ya Mbeya.

Gari hilo – Toyota Land Cruiser VX V8 – lenye namba STK 8299, ni mali ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, lakini Dk. Ulisubisya, akijua halina tatizo lolote la kiufundi, alijimilikisha kinyume cha maadili na kanuni za uhamishaji mali za umma kwenda kwa mtu binafsi.

JAMHURI imeshuhudia gari hilo likiwa limeegeshwa ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya. Kuna habari kwamba dereva alitumwa Machi 29, mwaka huu kwenda kulichukua Dar es Salaam na kufanikiwa kulirejesha Machi 31.

Hata hivyo, vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Waze na Watoto, zinasema kuna mikakati mahsusi imeandaliwa, ikiwa ni pamoja na kughushi nyaraka, ili ionekane kuwa gari hilo halikuwa mkononi mwa Dk. Ulisubisya, isipokuwa lilikuwa kwenye matengenezo jijini Dar es Salaam.

Transport Officer ni ndugu yake, wanahaha ili ionekane gari lilikuwa gereji, jambo ambalo ni uongo. Gari alishafanya taratibu zote za kulimiki na ndiyo maana likaondolewa Mbeya na kuletwa hapa Dar es Salaam,” kimesema chanzo chetu.

Katika hatua nyingine,Dk. Ulisubisya, anaelezwa kuwa hajakata tamaa kulitwaa gari hilo; na kwamba ndiyo maana limerejeshwa Mbeya, lakini limezuiwa lisitumiwe.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa sasa wa Hospitali ya Rufaa  Kanda ya Mbeya, Dk. Godlove Mbwanji, amehojiwa na JAMHURI na kukanusha madai hayo ya gari kuzuiwa kutumika.

“Ninachoweza kukueleza ni kuwa ni kweli gari tunayo hapa, ilikuja imefanyiwa service ndogo ya kawaida na inatumika. Ungekuwa karibu ningekuambia tupande uone inatumika,” amesema Dk. Mbwanji. 

Gari hilo ambalo liko katika hali nzuri, lilinunuliwa mwaka 2012 kwa ufadhili wa asasi ya Walter Reed Program ya nchini Marekani. Thamani yake ilikuwa zaidi ya Sh milioni 280, lakini taarifa ambazo bado zimefanywa siri zinasema Dk. Ulisubisya alilipata kwa kiwango kisichozidi Sh milioni 15.

Chanzo cha habari kimesema: “Taarifa kuhusu gari hilo zilighushiwa kwa kushirikiana na Transport Officer wa Wizara ya Afya na kuonesha kuwa gari hilo ni chakavu na bovu kabisa.

“Ofisi ya Rais, Idara Kuu ya Utumishi imeidhinisha alinunue kwa mkopo baada ya kudanganywa kuwa ni chakavu. Alilinunua huku akiacha Hospitali ya Mbeya ikiwa haina gari mbadala, wafadhili wamesikitishwa mno na kitendo hicho,” kimesema chanzo cha habari.

Wiki kadhaa zilizopita, Dk. Ulisubisya alihojiwa na JAMHURI kuhusu tuhuma mbalimbali, ikiwamo ya kujitwalia gari hilo, na kukiri kwamba bado alikuwa akiendelea na taratibu za kumilikishwa.

Alisema: “Lile gari lilikuwa bovu, niliamua kulinunua kama wanavyonunua watumishi wengine wa Serikali. Lilikuwa katika hali mbaya kutokana na ajali ililopata wakati mimi na dereva tukitokea Mbeya kwenda Dodoma, gear box yake haifai kabisa.”

Alipoulizwa kama alifuata taratibu za ununuzi wa mali za Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Dk. Ulisubisya alisema: “Nilikuwa sijui hiyo sheria hadi wiki iliyopita tulipokwenda kwenye semina elekezi ya makatibu wakuu Ikulu ndipo tukaelezwa taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kuuza na kununua mali za Serikali.”

Hata hivyo, awali katika mahojiano, alisema alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, alikuta hospitali hiyo ikiwa haina taratibu za ununuzi, na kuwa ni yeye aliyeziasisi.

“Nilipofika Mbeya ndipo nikaunda Bodi ya Ununuzi, awali haikuwapo, nikahakikisha kila kitu kinanunuliwa kwa kufuata sheria ya manunuzi (ununuzi),” alisema.

Kuhusu ubovu wa gari hilo, majibu yake yalikuwa hivi:

JAMHURI: Unasema hilo gari lilikuwa bovu, ubovu wake ulikuwa upi?

Dk. Ulisubisya: Lilikuwa halifai kabisa. Lilipata ajali na gear box ikafa.

JAMHURI: Ajali ilitokea wapi?

Dk. Ulisubisya: Wakati naenda Dodoma nikitokea Mbeya mimi na dereva wangu.

JAMHURI: Ulitoa taarifa kituo kipi cha polisi ili tuweze kujiridhisha kwa kupata taarifa ya polisi inayohusu ajali hiyo?

Dk. Ulisubisya: Sikutoa taarifa polisi.

JAMHURI: Ulipata ajali, lakini hukuona umuhimu wa kuripoti polisi?

Dk. Ulisubisya: Ndiyo, kwa sababu kwanza ulikuwa usiku; na ajali yenyewe tuligonga ng’ombe.

JAMHURI: Mwenye ng’ombe alijitokeza?

Dk. Ulisubisya: Hakujitokeza kwa sababu ulikuwa usiku na kwa hiyo hatukumjua.

JAMHURI: Unaweza kugonga ng’ombe halafu ukashindwa kutoa taarifa polisi ukizingatia gari ni mali ya Serikali, na limeharibika vibaya?

Dk. Ulisubisya: Nilizungumza na Transport Officer wetu wizarani akasema kama gari limepata ajali, na mimi niko katika gari hilo, basi hakuna haja ya kupeleka taarifa polisi kwa sababu shahidi ni mimi mwenyewe. Ndivyo alivyoniambia.

JAMHURI: Wizara ilipata taarifa za ajali hiyo?

Dk. Ulisubisya: Ndiyo, nilimweleza Katibu Mkuu.

JAMHURI: Kwa maandishi?

Dk. Ulisubisya: Hapana, ilikuwa verbally (kwa maneno).

 

Taratibu za mtumishi kuuziwa gari la umma

Mmoja wa wasomaji wa JAMHURI, aliyesoma habari hii, aliandika haya: “Naomba kuchangia kidogo taratibu za kufuatwa kwa magari ya Serikali.

“Kwa mujibu wa Kanuni za Fedha za Serikali, mara baada ya gari la Serikali kupata ajali, yafuatayo yanapaswa kutekelezwa na si hiari ya ofisa wa ngazi yoyote.

1: Kutoa taarifa kituo cha polisi kilicho karibu.

2: Polisi watakagua gari na kutoa Police Vehicle Inspection Report wakiainisha uharibifu uliotokana na ajali hiyo. Fomu hii ndiyo itakayoonesha ubovu na gharama itakayohitajika kulirejesha gari hili barabarani au la.

3: Polisi watafanya uchunguzi (upelelezi) ili kujua chanzo cha ajali na kutoa taarifa ya awali (PF90) na mwisho watatoa taarifa ya mwisho (PF115)

4: Baada ya Katibu Mkuu anayehusika kupokea taarifa hizi atajaza Treasury Form No.80 (TFN80) na kuiwasilisha Hazina pamoja na nakala za taarifa za polisi.

Transport Officer wa wizara kama anafanya kazi zake kwa weledi, hawezi kutoa ushauri mlioandika katika taarifa yenu kama utetezi wa Dk Mpoki.

Kama taarifa ya ajali hii hazitolewa polisi, TFN80 haikujazwa na kuwasilishwa Hazina, basi zoezi (utaratibu) zima lililofuata ni batili. 

“Vile vile inashangaza kwa vipi ofisi ya CAG haikuhoji vipi gari husika liliondolewa kwenye Daftari la Mali za Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (Serikali) bila ya Kanuni za Fedha za Serikali kufuatwa.”