Sehemu iliyopita, mwandishi alisema Katiba nzuri ni ile inayokuwa na maadili ya kitaifa. Alieleza namna Katiba ya kwanza ya Tanganyika ambayo baadaye ilitumiwa kwenye Muungano wa Tanzania ilivyokuwa na misingi imara ya kulinda maadili ya nchi. Endelea

 

Tunaona hapa kiona mbali cha Mwalimu Nyerere. Hakukomea kusema hivyo tu, bali alidiriki hata kutaja baadhi ya sifa za hayo maadili ya kitaifa kwa Serikali au Taifa lenye kuwa na Katiba yenye maadili mema. Taifa namna hiyo litajaribu kuleta umoja na usawa kwa sheria zake.

Serikali haitabagua raia wake kwa mitazamo ya rangi, dini, makabila jinsi, elimu au kwa aina yoyote. Wote watatendewa kwa haki wala hapatakuwa na upendeleo wa vikundi vya watu.

 

Mbele ya sheria za nchi watu wote watatendewa sawa kabisa na sheria za nchi zitawalinda. Katiba inapatia wananchi wake nafasi sawa za kufanya kazi za kupatia riziki zao binafsi na kwa familia zao na kadhalika (The National Ethic: Nyerere Uhuru na Umoja uk. 264 – 263).

 

Kuanzia hapo tujiulize hii Rasimu ya Katiba yetu inagusia mambo ya maadili ya Taifa hili? Kama mawazo namna hiyo yamo sasa KERO za Muungano zitakujaje? Ni kweli kero zilizoko zinaweza kusababisha mvunjiko wa Muungano wetu? Kweli zipo sababu za msingi za kuunda Serikali Tatu? Ni akina nani hasa wanaoshabikia kuvunja huu Muungano wetu uliodumu takribani miaka 49 sasa?  Tumefikiria au tumechambua misingi na sababu zilizofanya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziungane kwa haraka haraka vile?

 

Ndiyo, nazo zilikuwa za msingi kwa hali na mazingira ya wakati ule. Historia inatuonesha hivi: Wiki tatu tu baada ya Mapinduzi kulikuwa na wasiwasi mkubwa kule Visiwani. Hakukutarajiwa. Serikali mpya ya ASP ilichukua hatua za kujiimarisha (consolidate its position). Kwanza kabisa ilihitaji kutambuliwa ulimwenguni. Kule kusitasita kwa Serikali za Magharibi kuitambua Serikali ya Mapinduzi kulizua wasiwasi mkubwa Visiwani.

 

Wananchi walitaka kujihakikishia kuwa Zanzibar sasa inajengwa kwa misingi ya nchi za Kiafrika. Hatua ya kufikia azma hiyo ni ilikuwa kufufua na kuinua utamaduni wa Mwafrika.

 

Pili, lugha ya Kiswahili ilitangazwa kuwa lugha ya Taifa Visiwani. Tatu, Serikali ile ya Mapinduzi ilisitisha na kuifuta kabisa mikataba yote ya Serikali ya Sultani kwa uongozi wa ZNP ambayo iliingia na nchi za Kiarabu za Sudan, Misri na Saudi Arabia.

 

Jambo hili lilikuwa muhimu sana maana liliondolea mbali yale mawazo ya Waarabu kuifanya Zanzibar nchi ya Kiarabu. Serikali ya Mapinduzi ilikatisha kabisa uhusiano na nchi za Kiarabu.

 

Jambo hili liliwaudhi na kuwakasirisha Waarabu hasa wa asili ya Oman na kuzusha wasiwasi wa mapinduzi mengine (conter coup de’ tat) Visiwani. Serikali ya ASP tangu miaka ya 1957 ilikuwa na fikra sahihi kuwa Zanzibar ilikuwa sehemu ya Tanganyika. Ikumbukwe hapa kwa wakati ule yalitokea machafuko Tanganyika, Uganda na Kenya kwa majeshi ya KAR (King African Rifles) kuasi na hali hiyo iliyakaribisha majeshi ya nchi za kigeni kuvinjari katika Pwani ya Afrika Mashariki katika Bahari ya Hindi.

 

Usalama wa Visiwani ulikuwa shakani. Urusi, Ujerumani Mashariki na Uchina ziliitambua mara Serikali ile ya Mapinduzi Zanzibar, wakati nchi za Magharibi zilikuwa zikisuasua na ndipo lilizuka tishio la msuguano wa Vita Baridi kati ya Urusi na Marekani lisije likaingia Zanzibar na hivyo kufanya uwanja mpya wa mapambano kati ya Mashariki na Magharibi.

 

Hili tishio liliongezwa uzito kutokana na maneno ya Balozi wa Marekani jijini Nairobi la Aprili 2, 1964 pale alipolaumu Zanzibar kugeuzwa kuwa nchi inayofuata siasa ya ukomunisti.

 

Kupinga hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliwarudisha kwao wanajeshi wa Marekani kwenye kile kituo chao cha kijeshi katika ule mradi wa ‘Mercury’kwa kuwaamuru wafungashe virago vyao na waondoke mwishoni mwa Aprili, 1964 kabla ya Muungano wetu.

 

Katika hali ya misukosuko namna ile, ASP iliona kwa usalama wao kule Visiwani na kwa usalama wa ukanda huu wa Afrika Mashariki waharakishe kuungana na ndugu zao wa Tanganyika ili kujenga nguvu kubwa zaidi ya kujihami na hivyo kuepusha mapinduzi mengine Visiwani.

 

Je, hamuoni sasa busara za wazee Karume na Nyerere kuharakisha Muungano kwa manufaa ya nchi zetu zote mbili? Ule mzozo wa Vita Baridi kati ya Mashariki na Magharibi ungeathiri sana Uhuru wa nchi mbili hizi. Muungano ule uliimarisha sana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

Na kwa Muungano ule, misingi ya kuunganisha ASP na TANU iliimarishwa (Tazama Historia ya Mapambano ya Ukombozi Zanzibar – by Mrina na Matoke – TPH uk. 99 fikra za ASP 1957-1964).

 

Pamoja na kuharakisha Muungano, lakini Katiba ya Muungano iliyoridhiwa na pande zote mbili ilikuwa wazi, nzuri na yenye kuonesha nia ya wakazi wa Tanganyika na Zanzibar. Nanukuu kipande cha mwanzo kabisa hapa:-

 

Kila mwenye kusoma yale makubaliano ya Muungano (Articles of Union) akisoma ibara ile ya kwanza tu atajua ilikuwa na viashiria vya undugu na umoja wetu wa asili kati ya watu wa nchi hizi mbili.

 

Maneno yaliyotumika yalisema hivi, nanukuu; “Whereas the government of the Republic… being mindful of the long association of the peoples of these lands and of their ties of kinship and armity and being desirous of furthering that association and strengthening the unity of African people have met and considered the union of the Republic of…” na kifungu kile kilihitimishwa kwa maneno ya hekima namna hii (i) The Republic of Tanganyika and the Peoples Republic of Zanzibar shall be United in one sovereign Republic …ndivyo mambo yalipokomaliwa.

 

Maneno mazito namna hii na ya kizalendo kutoka kwa watu wa Zanzibar, leo mtu aje aseme mbona hatukushauriwa, oh! mbona hatukuulizwa hivi. Wanaofyatuka kusema hivi walikuwa na umri gani Aprili 26, 1964? Pengine wala hawakuwa wameingia ulimwenguni. Leo waje na stori za watu wa Zanzibar eti waulizwe wanautaka Muungano au hawautaki ndipo Katiba yetu iandikwe ni sahihi kweli wazee wenzangu?

 

Labda Mzee Brigedia Jenerali Ramadhani Haji Faki ambaye ndiye pekee yu hai miongoni mwa wale wajumbe 14 wa Kamati ile iliyoongoza Mapinduzi Januari 12, 1964 aulizwe kama haya ninayoyaandika ni matukio ya kweli au la.

 

Mwingine ni Mzee Hassan Nassor Moyo aliyehudhuria hata kile kikao cha Katiba kule Laucaster House, Uingereza, Septemba 20-24, 1963 na ndiye aliyefuatana na Mzee Karume katika mikutano yake na Mwalimu Nyerere mara baada ya Mapinduzi anasemaje? Kinachokosekana hapa ni elimu na maelezo ya kihistoria kwa vizazi vipya waone na watambue Muungano ulikotoka mwaka ule wa 1964.

 

Nimetumia muda mrefu kuelezea hali ya Muungano ulivyoanza ili kusiwe na utata (ambiguity) katika mawazo ya wananchi kuhusu umuhimu wa kupata Katiba sahihi, sanifu na ya watu wote.

 

Tusipumbazwe na makelele ya wenye uchu wa madaraka. Maswali muhimu hapa ni je, sisi sote leo hii kwa hali ilivyo tu Taifa gani? Tuko mataifa mangapi katika nchi hii? Tunataka Katiba mpya ili iweje? Tuwe na uraia wa mataifa mengine au Taifa moja tu?

 

Kwa namna Muungano wetu ulivyo, pande zote mbili za Jamhuri zinanufaika. Bila kuwa na hali namna hii ingewezekana kweli mtu wa Zanzibar kuwa Mbunge wa Jimbo lolote huku Bara? Hivi kwa style yetu hii ya Muungano tulikuwa na Mbunge wa Mkuranga mwenye asili ya Visiwani, nani alishtuka?

Leo hii, tunapodai Muungano una kero nyingi mbona wa Visiwani zaidi ya watu wake 600,000 (Jamhuri Toleo No. 88 la tar 18-24 Juni uk. 2) wana umiliki wa ardhi huku Bara? Wametapakaa huku Bara wana majumba, mashamba na miradi kemkem.

 

Wapemba wapo Rukwa, Kigoma, Morogoro, Iringa, Mwanza, Mtwara hata Ruvuma. Je, hawa si wataathirika sana? Kero wanaziona viongozi wa siasa wenye uchu wa madaraka, lakini wa Visiwani wengi wanafaidi sana maisha ya huku Bara. Wameoa na kupata watoto ambao ni WATANZANIA. Je, wanaweza kuwa Wazanzibari kesho Katiba ikiamua hivyo? Watoto wetu namna ya hao watapata malezi ya Taifa lipi?  Tanganyika, Zanzibar au Tanzania? Mie sintofahamu lolote katika hili.

 

Kule visiwani kweli ipo ardhi ya kuwameza hawa “Wazanzibara” wakirejea kule? Tuwe tunasema kwa kufikiria matokeo ya wengi sio kusema kwa kunogewa na madaraka ya kisiasa.

 

Itaendelea