BAGAMOYO
Na Marie binti Shaba
Katika hotuba yake kwa taifa kupitia wanawake, Rais Samia Suluhu Hassan, aligusia mambo yaliyojaa busara. Binafsi niliguswa na mbinu aliyoitumia kuelezea kwamba binadamu wote tuna nguvu sawa mithili ya pande mbili za sarafu moja.
Samia alifafanua kwamba Mwenyezi Mungu ametupa nguvu mbalimbali na zote ni nzito. Mwanamume anabeba mizigo, anajenga miundombinu, anafanya uamuzi mgumu kama kupigana vita.
Mwanamke ana uwezo wa kufanya uamuzi mgumu kama kutunga mimba na kulea, ana kipaji cha ushawishi kwa kutumia ulimi. Mwanamke ana subira na uvumilivu wa pekee.
Mwanamume ameumbwa kuwa hazina ya mbegu za uzazi, na mwanamke ni shamba ambapo mbegu itamea kisha atakuwa ‘karakana’ iliyojitosheleza ya Mwenyezi Mungu ya kuendeleza kazi yake ya uumbaji na ulezi. Kwa uvumilivu wake mwanamke anaangaliwa kama kiumbe dhaifu.
Nguvu za mwanamke hazionekani; ni kama mbegu ardhini, hufukui kuangalia kama mizizi imeshaanza kuota; kabla haijatoa matunda haina thamani ya fedha. Baba analipwa mshahara anajenga, mama anasimamia, analisha vibarua, anaangalia familia na kumtunza mumewe. Mama pato lake litahudumia mahitaji ya familia. Mama akitangulia mali yake ni kanga zigawiwe kwa binti zake. Akitangulia baba mali alizochuma na mama ni za ukoo si familia.
Tanzania tumeshuhudua kiongozi wa taifa amefariki dunia katikati ya utumishi wake kabla hajakamilisha ndoto zake. Laiti angemaliza muhula wa pili angetueleza kwa nini alifanya alivyofanya na kukiri pale alipokosea, lakini hana kauli.
Mimi ninaamini 2015 tulimhitaji JPM katika muktadha wa sitiari ya Rais Samia. Tulihitaji aina ya uongozi wake ambao uliendana kabisa na hulka za wanaume. Pengine hatukumwelewa kwa sababu hatukuwahi kupata kiongozi aina yake. Baba alitutandika viboko mpaka tukalia, lakini ni kawaida kwenye mabadiliko kuna matamu na machungu.
JPM hakutumia ulimi, alitumia vitendo. Pia hakuona haya kujigamba na utajiri mabeberu wasikie. Katuzindua kuwa jukumu la serikali ni kutoa huduma kwa haki, kuongeza ubora wa miundombinu na kufuatilia matokeo hata bila chama cha siasa. Chama kitaelekeza utekelezaji kwa kuzingatia mahitaji na matarajio ya wananchi.
Mzee Mwinyi alimsifu JPM kwa kutekeleza makubwa kwa miaka mitano ambayo waliomtangulia hawakufanya kwa miaka 55. Wengine wakabeza kwani tutakula madaraja na mabombadia? Tumelia baba ametujengea jengo tutafanya nini liwe nyumba ya kuishi familia?
Mola wetu ametupatia Samia Suluhu Hassan ambaye ni mrithi tuliyemhitaji! Kama Makamu wa Rais, alielewa umuhimu wa JPM kutoa kipaumbele kwa miundombinu kufikia kuwa nchi ya viwanda. Anajua ukali wa vita ya uchumi ndiyo maana ya kauli ‘Kazi Inaendelea’. Asingemuelewa angeshajiuzulu. Watoto wanaangalia jinsi Mama anavyomrithi Baba, je, uwekezaji waliofanya pamoja utawafaidia wajukuu au wajanja watapora kila kitu pamoja na jina la Baba?
Kumrithi aliyekutangulia si kazi rahisi, lakini kwa kutumia nguvu alizopewa mwanamke tunaona namna anavyoongoza nchi. Kafunga mkaja kwa hatua kukabiliana na vinyamkera na vipambe nuksi vinavyojitokeza baada ya kukalia kitimoto.
Kabla ya mwaka 2025 tuwe na muafaka ndani ya Katiba; je, tunataka taifa la kijamaa na kujitegemea au ubinafsi na utegemezi? Vyama vipewe Ilani moja ya wananchi ili vieleze vitatekeleza vipi ujamaa na kujitegemea katika muktadha wa Katiba na Muungano wa Afrika. Wakati wa kila chama na itikadi yake umekwisha, si lazima tugezee wengine, ni Yarabi nafsi yangu!
Mwandishi wa makala hii ni mwandishi mkongwe nchini na ni msomaji mzuri wa JAMHURI.