Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu) Patrobas Katambi amesema serikali itaendelea kuongeza kasi ya kutatua migogoro, kusogeza huduma karibu na wafanyakazi na waajiri kupitia Tume inayotembea yaani ‘Mobile Labour Disputes Settlement Services’ na kuendelea usimikaji wa mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha usajili na utatuzi wa migogoro ya kazi.
Ameyasema hayo leo Agosti 27, 2024 wakati akifunga mafunzo ya mfumo ya uendeshaji na usimamizi wa mashauri kwa njia ya mtandao (OCMS) kwa wadau wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
Amesema serikali inatambua kwamba kati ya changamoto zilizowasilishwa na Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA) katika hotuba yao katika Meimosi ya mwaka huu ni kuhusu mifumo ya utatuzi wa migogoro ya Kazi ambapo kuna maeneo Tume haina ofisi hivyo kupelekea kukosa huduma za Tume.
“Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha kujali wafanyakazi na waajiri kwenye eneo hili la utatuzi wa migogoro ndiyo maana iliwahakikishia na kuweka wazi kupitia hotuba ya Dkt. Phillip Isidor Mpango, Makamu wa Rais akimwakilisha Rais siku ya Meimosi.
“Kwa msisitizo katika aya ya tatu ya ukurasa wa 7, Makamu wa Rais alisema Serikali inaendelea kusimika mifumo ya kielektroniki ya usajili, utatuzi na usimamizi wa migogoro ya Kazi. Mifumo hii itawawezesha wafanyakazi na waajiri popote walipo kusajili migogoro ya kazi ikiwemo kutumia simu-janja pasipo kulazimika kuzifata ofisi za CMA,” amesema.
Ameongeza kuwa watahakikisha kuwa huduma zinazotolewa na tume pamoja na taasisi zote zilizo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ni za hali ya juu na zinawafikia wananchi popote waliopo.
“Ifahamike kwamba mkakati na agenda ya kuboresha utendaji wa Serikali katika kuwahudumia wananchi ni msisitizo mkubwa wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwani yeye ndiye aliyetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 2.1 kuwezesha usimikaji wa mfumo pamoja na miundombinu yake na vitendea kazi.
“Tumemsikia mara nyingi Rais Samia akisisitiza matumizi ya mifumo na kwamba mifumo isomane ili kupunguza na ikibidi kuondoa urasimu katika utoaji wa huduma. Mifumo hii itawafanya wananchi waweze kupata taarifa na kuhudumiwa kwa muda mfupi,” amesema Katambi.
Aidha ametoa wito kwa Tume kuyafanya mafunzo hayo kwa upana wake ili kuhakikisha wafanyakazi, waajiri, mawakili, wawakilishi binafsi na jamii yote wanaelewa kuhusu umuhimu na matumizi ya mfumo huu.
Awali Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla amesema mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa migogoro ya kikazi ni utekelezaji wa mradi namba 5505 ambao unafadhiliwa na serikali kwa asilimia 100.
“Mafunzo haya ni utekelezaji wa maagizo na mkakati wa serikali na maelekezo ya Rais Samia ambaye alilisisitiza kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi lakini pia kutumia mifumo na iweze kusomana ili wananchi na hasa wafanyakazi, waajiri na waajiriwa ambao ni wawekezaji waweze kupata huduma za tume ya usuluhishi na uamuzi au za utatuzi wa migogoro ya kazi kwa haraka.
“Na tunaamini baada ya mafunzo haya na mfumo kutekelezwa, utakuwa ni majibu kwa changamoto za muda mrefu za wananchi katika maeneo mbalimbali nchiniā¦tangu kuanzishwa kwa tume hiyo tulikuwa tunatatua migogoro manual, tulikuwa tunatakiwa kupeleka majarada mahakama kuu na kumekuwa na malalamiko ya ucheleweshwaji,” amesema.
Amefafanua kuwa, Mfumo taarifa zake zitasomana na mahakama, ofisi ya kamishna wa kazi, wadau mbalimbali wataweza kuwasilisha mashauri bila kufika ofisini kupanga foleni au kusafiri umbali mrefu
“Kupitia mfumo huu tunaamini ufanisi wa tume utaongezeka lakini tunaamini utatuzi wa migogoro ya kikazi utakwenda kwa haraka Zaidi ya ilivyozoeleka.
“Tunaamini pia kupitia mfumo huu watu wengi watafikiwa kwa wakati mmoja pasipo kuleta usumbufu,” amesema.