Na Cresensia Kapinga, JamhuriMediia, Songea
Diwani wa Kata ya Matogoro iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Issa Mkwawa kwa kushirikiana na uongozi wa kata hiyo wametoa msaada wa viti na meza 302 vyenye thamani ya sh.milioni 15 katika shule ya Sekondari ya kutwa ya Matogoro ili kupunguza tatizo la upungufu wa madawati uliyokuwa ukiikabili shule hiyo.
Akikabidhi viti na meza hizo Diwani Mkwawa kwa mgeni rasmi Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Fredrick Sagamiko, amesema kuwa wakati anaingia madarakani alikuta watoto wengi wanakaa chini kwa kushirikiana na uongozi wa kata na Chama cha Mapinduzi ( CCM), wameamua kujumuika na jamii katika kusaidia maendeleo mbalimbali ambayo yamekuwa na changamoto ambapo kwa hivi sasa uongozi umeamua kushirikiana na shule ya Sekondari Matogoro kwa kuchangia viti na meza .
Amesema kuwa lengo ni kusaidia Serikali pamoja na jitihada za rais Samia Suluhu Hassan za kujenga madarasa mengi na kupeleka viti lakini pia kata yake imejikita zaidi katika maeneo ya elimu na kwamba watahakikisha wanakuwa na benki ya viti na meza kwa shule zote zilizopo kwenye kata hiyo.
“Mkurugenzi sisi tunasema kuwa kwa Matogoro hatutaki mtoto wetu hata mmoja akae chini na hilo tumefanikiwa, na mpaka Sasa hivi ninapozungumza na nyie mtoto wa Matogoro hatokaa chini na bado tunaendelea kutengeneza ili tuwe na benki ya viti, meza na madawati kwa shule zetu za msingi na Sekondari” amesema diwani huyo.
Awali akisoma taarifa fupi ya kukabidhi viti na meza kwa mgeni rasmi Afisa Elimu kata ya Matogoro mwalimu Samson Mbunda amesema kuwa shule ya Sekondari ya Matogoro ina jumla ya wanafunzi 1080 ambapo kidato cha kwanza 360,kidato cha pili 290, kidato cha tatu 222 na kidato cha nne 208 na kwamba mpaka sasa wanafunzi wote wanakaa kwenye viti.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko ameshukuru kwa msaada wa viti , meza na madawati uliotolewa na Diwani wa kata ya Matogoro pamoja na uongozi wa kata na chama ambao umemaliza kabisa changamoto ya upungufu wa viti, meza na madawati katika shule za Sekondari na msingi katika kata hiyo.
“Mheshimiwa Diwani tunafahamu kwamba ilikuwa wajibu wetu, wajibu wa Serikali kuhakikisha watoto wetu wote kwanza wanapata maeneo ya kujifunzia kwa maana ya madarasa, tuhakikishe kunakuwa na viti,meza pamoja na madawati ,lakini mahitaji ni mengi nje ya sekta ya elimu tuna mahitaji katika sekta ya afya , miundombinu na sekta zingine ni matamanio yetu na matarajio yetu maeneo mengine wananchi waunge mkono serikali kama mlivyofanya ninyi hapa Matogoro ” amesema Dkt. Sagamiko.
Hata hivyo Dkt. Sagamiko amewataka madiwani, watendaji wa kata,mitaa, waratibu Elimu kata na wakuu wa shule katika Manispaa ya Songea kwenda kujifunza kata ya Matogoro badala ya kutumia gharama kubwa kwenda kujifunza maeneo ya mbali na Songea wakati Matogoro ni kata ya mfano kwa kila kitu.