*Mwanamke ‘mgeni wake’ adaiwa kumpoka maelfu ya dola kitaalamu

*Yeye amgeuzia kibao mtumishi wa ndani, amsweka rumande siku saba

*Mtumishi wa ndani afukuzwa, aieleza JAMHURI kila kilichotokea

*Walinzi wawili wa kike wasimamishwa, mishahara, posho vyafyekwa

 

Kuna harufu ya kashfa dhidi ya Naibu Spika, Job Ndugai, ambaye ameibiwa dola 15,000 (Shilingi zaidi ya milioni 24), nyumbani kwake Area ‘D’ mjini Dodoma.

Wakati Ndugai akidai kwamba fedha hizo zimeibwa na mfanyakazi aliyedumu naye kwa miaka 12, mfanyakazi huyo, George Sendwa (33), katika maelezo yake Polisi, anadai kwamba mhusika ni mwanamke aliyekaribishwa na Ndugai kwa siku mbili. Anamtaja kwa jina la Rehema, na kwamba ni mwanasheria.

 

Sendwa anasema hajui  uhusiano wa mwanamke huyo na Naibu Spika, lakini anachojua ni kwamba alimpokea na akaishi naye kwa siku mbili nyumbani hapo akimhudumia kama mgeni wa “Mheshimiwa Naibu Spika”.

 

Sendwa anadai alikamatwa na kuwekwa rumande katika Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Dodoma, kwa siku saba kwa amri ya Ndugai.

 

“Muda wote huo sikufikishwa mahakamani, niliteseka sana hasa nikikumbuka kuwa nimeishi na Mheshimiwa kwa miaka 12 tena bila mshahara. Kama kuiba, ningeweza kuiba kwa miaka yote hiyo kwani nilikuwa na uwezo wa kufanya hivyo, lakini sikuwa na tamaa,” anasema.

 

Anaongeza, “Alikuwa Dar es Salaam, akanipigia simu akisema kuna mtu (mwanamke) atakuja, nimkaribishe sebuleni. Kweli, muda si mrefu alifika na mheshimiwa naye akafika baadaye. Alikaa siku mbili. Alipoondoka Mheshimiwa akanifuata na kuniambia kwamba nimeiba dola 15,000 za Marekani.

 

“Akadai nimeiba eti kwa sababu nimekuwa mjanja. Akadai fedha hizo zilikuwa katika kabati, lakini funguo alikuwa nazo yeye mwenyewe. Alinifukuza saa 12 jioni akasema niende ninakojua. Akamtuma Bahati (mdogo wake Ndugai) wakanikamata wakiwa na polisi wawili wakaniweka ndani. Akawaambia polisi ‘mwekeni ndani siku saba hadi abadilike rangi’.

 

“Dada yangu, Magreth Mfinde, na mama yangu mzazi Agness Makanyaga wakahangaika, wakaniwekea dhamana ya Sh milioni tano. Dada alilazimika kuweka rehani nyumba yake. Nikaambiwa nirudi baada ya siku saba. Askari wakanitaka niwe naripoti; mara ya mwisho nimeripoti Aprili 25 ndiyo polisi wakasema nipumzike hadi hapo watakaponiita.”

 

Sendwa anasema tangu wakati huo maisha yake yamekuwa mabaya, kwani hata kazi aliyopewa bungeni, ya kumhudumia Naibu Spika chai, aliipoteza.

 

“Wakati nikifanya kazi nyumbani kwake alinitafutia kazi bungeni, nilikuwa nalipwa mshahara pamoja na marupurupu yanayofikia Sh 291,000 kwa mwezi. Akaamuru nifukuzwe kwa madai kwamba nimeiba nyumbani kwake,” anasema.

Kijana huyo analalamika kwamba kwa miaka yote 12 aliyofanya kazi kwa Ndugai, hakulipwa mshahara kwa vile aliahidiwa kujengewa nyumba na kuanzishiwa biashara.

 

“Alinichukua nikiwa mdogo kutoka kwa mama mkubwa, Damalisi Kingamkono. Tulikuwa tunaishi Kongwa, nikaanza kumfanyia kazi za kila siku za kupika, kufua nguo, kunyoosha nguo na usafi wa nyumba katika nyumba zake tatu. Mbili zipo Area D, nyingine ipo Ipagala. Hizi ni mbali na zile za Kongwa,” anasema.

 

Maelezo ya walinzi wa kampuni ya Full Time

Sakata hilo la upotevu wa fedha za Ndugai limegharimu ajira za wanawake wawili, ambao ni walinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Full Time ya mjini Dodoma.

 

Sophia Ngonyani (35) katika mahojiano na JAMHURI, anasema, “Jambo hili kweli lilitokea, natakiwa kuripoti polisi kila mara. Kesi ipo kwa afande Khamis.”

 

Kuhusu kuiba fedha hizo, Sophia anasema, “Nichukue wapi ndugu yangu? Nina shida sana, ningekuwa nimeiba hizo fedha leo nisingekuwa na maisha haya ya tabu, sijui kuiba. Nimeonewa sana. Mungu ndiye anayejua.

 

“Kazi tulisimamishwa na hatujui kama tutarejeshwa. Hatuna malipo yoyote. Maelezo tulitoa, lakini sidhani kama kuna faili. Nadhani hata polisi wenyewe wameona hatuhusiki. Ningekuwa nazo ningepotea kabisa, nisingekuwa dunia hii, hela haijifichi bwana, ningekuwa nayo watu wangejua tu.

 

“Siwezi kujua aliyeziiba, lakini kulikuwa na mwanamke (hataki kueleza uhusiano wa Ndugai na mwanamke huyo), ni mweusi, mnene kidogo na mfupi wa wastani. Simfahamu kwa jina, lakini nikimwona nitamtambua,” anasema Sophia.

 

Mlinzi mwingine, Nusura Ramadhani (27), anasema siku ya tukio hakuwapo, isipokuwa ameunganishwa tu kwenye kesi hiyo. Ingawa hasemi, maelezo kutoka kampuni ya Full Time yanasema mlinzi huyo alihusishwa kutokana na kuwa na uhusiano wa karibu na kijamii na mmoja wa watuhumiwa katika kesi hiyo.

 

“Mimi niliunganishwa tu, kwani hata kwenye maelezo polisi mimi sikutoa, lakini nikaambiwa nimo. Wanasema ziliibwa dola 15,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 24. Kazi tumesimamishwa, kwa sasa nipo tu nahangaika,” anasema Nusura.

 

Kampuni ya Full Time yanena

Hamid Mbembela ambaye anajitambulisha kama supervisor (msimamizi) wa Kampuni ya Ulinzi ya Full Time mkoani Dodoma, anakiri kuwapo kwa tukio la kuibwa fedha za Naibu Spika, na kusimamishwa kazi kwa walinzi wake wawili.

 

“Tukio lipo Polisi, kwa kweli sijui linaendeleaje. Mtuhumiwa ni mmoja (Sophia), mwingine anahusishwa kutokana na madai kwamba alikuwa na uhusiano na kijana pale nyumbani. Hawa (Sophia na Nusura) ni marafiki. Wakati wa tukio alikuwa nyumbani kwa Mheshimiwa ni Sophia. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Ndugai, huyu mwingine ni mpenzi wa mfanyakazi mtuhumiwa,” anasema.

 

Mbembela anaeleza kwamba walinzi hao wawili walisimamishwa kazi kutokana na tuhuma dhidi yao. “Wanakuja kuripoti hapa ofisini, lakini hakuna mshahara wala posho tunazowalipa wakati huu ambao wamesimamishwa,” anafafanua.

 

Polisi wanena

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alipoulizwa na JAMHURI kuhusu tukio hilo, amesema hana taarifa zake.

 

“Aliibiwa lini? Mwaka huu hakuna kitu kama hicho. Ngoja nifuatilie, inawezekana ikawa kwenye vitabu, nawauliza waliokuwapo kama wana taarifa hiyo,” amesema.

 

Naibu Spika agoma kujibu

Kwa upande wake, Ndugai amegoma kuzungumzia tukio hili, licha ya kumpelekea ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu zake za mkononi. Kila akipigiwa simu inaita hadi inakatika.


JAMHURI ilipiga kambi kwenye ukumbi wa Bunge kwa wiki sasa na kumpelekea karatasi ya maandishi kwenye Kiti cha Spika kumtaka kupitia wahudumu wa bungeni, kumwomba ajibu tuhuma hizo, lakini hakujibu ujumbe huo pia.