Pinda ahusishwa

*Mmoja wa washirika ajitoa kuepuka aibu
*Ni Chuo Kikuu cha Iowa cha Marekani
*Yabainika wanaleta teknolojia hatari nchini

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameendelea kubanwa kuhusu uamuzi wake wa kuwasaidia Wamarekani kujitwalia ekari laki nane za ardhi kwa miaka 99 mkoani Katavi.

Pamoja na Pinda, washirika wengine kwenye mpango huo ni Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam , Idi Simba kupitia kampuni ya Serengeti Advisors Ltd.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) ameliambia Bunge kwamba Pinda, amevunja sheria za nchi kwa kuhakikisha kampuni ya Agrisol Energy ya Marekani inajitwalia maelfu hayo ya ekari mkoani Katavi (Rukwa) bila kufuata sheria za nchi.

Wakati Agrisol wakihaha kutwaa ardhi hiyo yenye ukubwa unaolingana, au kuzidi baadhi ya nchi duniani, imebainika kuwa kwa pamoja (ukiondoa Tanzania ) kampuni hiyo inamiliki ardhi isiyozidi hekta 30,000 katika mataifa mbalimbali.

Mdee anasema chombo pekee cha kutoa ardhi kubwa kiasi hicho kwa wawekezaji ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), lakini kwa hili la Katavi kazi hiyo imefanywa na Pinda na uongozi wa wilaya, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za uwekezaji. Makubaliano (MoU) yalitiwa saini Agosti 11, 2010.

Tayari madiwani kadhaa wa Mpanda walipelekwa Marekani katika ziara ambayo ilizua mjadala mkali. Balozi wa Marekani hapa nchini, Alfonso Lenhardt, ni mmoja wa wapigadebe wakuu wa upokwaji ardhi huo.

Mdee anasema Serikali imefanya kila ililoweza kuhakikisha kuwa wakimbizi 162,000 wanapewa uraia wa Tanzania na kisha wanasambazwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Anasema mpango huo ambao umesimamiwa na Pinda, umefanywa ili maeneo yaliyokuwa kambi za wakimbizi wa Burundi – Lugufu, Katumba na Mishamo- tangu mwaka 1972, yatwaliwe na wawekezaji hao.

Hata hivyo, Mdee anasema kutokana na utata mkubwa wa mradi huo, mshirika wa Agrisol, ambaye ni Chuo Kikuu cha Iowa nchini Marekani (ISU), kimeamua kujitoa.

Taarifa ya Iowa kujitoa imetolewa chini ya kichwa cha habari, “Chuo Kikuu cha Marekani chajitoa kwenye uporaji ardhi Tanzania .

Kujitoa kwake kumeelezwa kuwa kumetokana na kubainika kuwa kampuni ya Agrisol imekuwa ikilaghai ili kupata aradhi kubwa. Ulaghai huo ni pamoja na hoja kwamba uwepo wake katika eneo la Lugufu, Mishamo na Katumba kutsaidia wakulima wadogo wadogo ili waweze kulima kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Mpango wa kuwasaidia wakulima wadogo wadogo umekuwa ni wa ISU pamoja na mshirika wake, Chuo cha Oakland .

Moja ya majarida yamebainisha kwa kusema, “Kusingizia kuwa wanataka kuwasaidia wakulima wadogo wadogo ni mbinu tu wanayotumia ili kupata misamaha ya kodi.”

Inaelezwa kuwa pamoja na mradi huo wa ekari laki nane kuhojiwa mara kwa mara, Agrisol haijapata kueleza ushiriki wake wa kuwaondoa wakimbizi 162,000 katika eneo hilo walioishi kwa miaka 40 sasa.

Mbinu za kutwaa eneo husika

Mdee anasema kampuni ya Agrisol imebainika kuwa imedanganya mambo mengi ili iweze kupata eneo hilo kubwa kuwahi kutolewa kwa kampuni ya kigeni hapa nchini.

Miongoni mwa ahadi alizoziita za uongo ni za kusaidia wakulima wa vijiji jirani, kutoa ajira na kupunguza uhaba wa chakula nchini.

Anasema ukweli ni kwamba kwenye makubaliano (MoU) ya kampuni hiyo na Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Agrisol kwa kuwatumia Seregenti Advisors Ltd imejipa jukumu la kufanya upembuzi hadi vijiji jirani lengo likiwa ni kutambua mtandao wa maji yatakayonufaisha mashamba makubwa ya wawekezaji, na si ya wanavijiji.

Pia anasema uchunguzi wa wataalamu mbalimbali umebaini kuwa kwa kuitwaa ardhi hiyo, wanavijiji watageuzwa kuwa vibarua na manamba kwenye mashamba ya wawekezaji. Amesema tayari kuna mipango ya kuwaleta raia wa Afrika Kusini kuongoza shughuli mbalimbali za kilimo kwenye mradi huo.

Mbaya zaidi, anasema teknolojia wanayodai kwamba itasambazwa kwa wakulima-teknolojia ya GMO ni hatari, na kwamba itawafanya wakulima wa vijiji jirani na Watanzania kwa jumla kuwa wategemezi.

“Hii ni teknolojia ya mbegu za kutengenezwa katika maabara. GMO ni hatari, ukishaitumia katika ardhi huwezi kutumia tena mbegu za asili. Ulaya na Marekani teknolojia hii inalalamikiwa sana kwa sababu inaua mazao ya asili.

“Ukishaiweka Katavi au Rukwa, ina maana wakulima wadogo wadogo watalazimika kununua mbegu kutoka kwenye viwanda vya hawa wawekezaji. Kwa sasa wakulima wetu wadogo wadogo wana uwezo wa kulima kwa kutumia mbegu za asili na kuvuna, ukishaweka GMO ni lazima wanunue kwa hawa wawekezaji. Kwa hiyo pamoja na kuwa vibarua katika mashamba yao , watakuwa watumwa wa kununua mbegu kutoka kwao. Hili halikubaliki,” amesema Mdee katika mahojiano maalumu na JAMHURI.

Mdee anasema Pinda anachofanya ni kukaribisha ukoloni mpya nchini, na hasa kwa eneo la Mkoa wa Katavi.

Anasema eneo linalofaa kwa kilimo katika mkoa huo ni asilimia 19 pekee, huku jingine likiwa ni maji, misitu na hifadhi mbalimbali.

“Kama unachukua ekari nane na kuwapa wageni, huku ukitambua kuwa eneo linalofaa kwa kilimo ni dogo, maana yake ni kuwafanya wananchi katika eneo hilo wawe vibarua na manamba kwenye mashamba ya wakubwa,” anasema.

Lakini anasema uwekezaji wa dola milioni 100 za Marekani kwa kwa miaka 10 ni kwango kidogo mno ambacho Watanzania wenyewe wakiwezeshwa wanaweza kabisa kuufanya uwekezaji huo.

“Wanasema baada ya miaka 10 wataanza kutengeneza faida ya dola milioni 350 za Marekani…hii ina maana kwamba kuanzia mwaka wa 11 tangu wawekeze. Hivi kweli Watanzania sisi wenyewe tunashindwa kufanya kitu kama hiki hadi tulete wageni, tuwape ardhi kwa miaka 99?” Anahoji.

Mdee na wanaharakati wengine wanaopinga uporaji ardhi katika Tanzania wanasema kilimo kikubwa kinachoendeshwa na wageni, hakina tija kubwa, isipokuwa kinaongeza umasikini kwa wananchi.

Pinda ajibu mapigo

Pinda anakiri kuwa amekuwa mshirika wa karibu wa mpango huo wa kuwakaribisha wawekezaji, lakini anasema kwa sasa kilichopo ni hatua za mwanzo tu.

Katika majibu yake, alianza kutoa historia kwa kusema, “Maeneo haya yalikuwa ni ya misitu iliyohifadhiwa kwa mujibu wa sheria. Ni maeneo ya Serikali. Tuliyatoa katika kukidhi haja hii ya kuweka wakimbizi katika maeneo hayo. Kilichotokea nini? Baada ya hali ya Burundi kutuwama -kuwa na amani- uamuzi wa Serikali ukawa ni kwamba (wakimbizi) mrudi kwenu. Ndipo jambo hili likaibuka, sasa hii ardhi tuliyokuwa tumeitoa kama misitu, ama tuirejeshe iwe misitu tena, ama tuone namna ya kuitumia kwa maana ya kuongeza tija katika udongo au ardhi hiyo.

“Ndiyo tukaanza kutafakari mimi, mkuu wa mkoa na wabunge wengine tuliokuwa na nia njema; jamani hii ardhi wakiondoka hawa, tunafanyaje? Ndipo ikatokea hiyo kampuni ikasema iko tayari kama tutaridhia kuwekeza katika eneo hilo . Mimi nikafarijika sana . Tukaona pengine ni jambo zuri.

“Nje ya kambi hizo tunavyo vijiji 42 ambavyo vinaendelea na shughuli zake, kwa hiyo mtazamo ukawa ni kwamba tukimkuta mtu mzuri, hawa wote tunaweza tukaona namna ya kuwasaidia wakaona hizo tekenolojia, wakaona hivyo vitu vingine pia tukawa na soko la uhakika. Kubwa kwa Katavi ni kuongeza uzalishaji wa mazao.

“Kwa hiyo hatua ya kwanza tuliyoanza nayo, ikawa kwamba basi wewe bwana tulitiliane MoU-maelewano hivi maana yeye alitaka kuanza na uchunguzi wa udongo maana wenzetu kidogo wamekwenda mbali. Hawezi kuanza kulima kama sisi tunavyoanza…unavyeka tu, hapana. Wakasema tunataka kwanza tujihakikishie. Kwa hiyo tukakubali, ‘haya njoo uanze kufanya uchunguzi’. Lile jambo tukaenda kwenye Baraza la Madiwani tukalizungumza mwishoni tukasema mwacheni afanye uchunguzi, yote mema. Uchunguzi ule umechukua mpaka majuzi walikuwa bado wanafanya ule uchunguzi ili baada ya pale sasa ndiyo tukubaliane eneo gani tunafikiri tuwape kwa ajili ya kitu gani. Tulichosema, tukasema sisi kwa mujibu wa sheria zetu ni vizuri ukajua kwamba ardhi yetu sasa hivi mtu akitaka kuweka kitu pale lazima alipe hiyo kodi ya ardhi ambayo kwa mujibu wa utaratibu ni Sh 200 (mia mbili). Ilikuwa Sh 600 (mia sita), wakatupa ushauri watu wa private sector tukapunguza mpaka mia mbili. Wawezekaji wote wale ni Sh 200 (mia mbili) kwa eka moja. Ndicho tulichofanya. Lakini, hatujafika mahali tukaingia mkataba na hao watu katika uzalishaji wenyewe, ilikuwa kwamba tukishamaliza hatua hiyo ya mchakato ndiyo tutaingia kwenye mambo ya msingi tuone tunapangiana vipi, uwiano utakuwaje, halmashauri imiliki kiasi gani cha hisa, na kadhalika na kadhalika.

Hili jambo nimekuwa nalisema, nalirudia, lakini kila nikiwasikiliza wenzangu (wapinzani), naona limepamba moto utafikiri tumefikia mwisho wakati kumbe jambo lenyewe bado. Nimeona niliseme hili ili wenzangu Mpanda wanielewe, maana wasije wakanielewa hapa kwamba nimeuza ardhi, nimeshawapa Agrisol, na kadhalika. Hapana, hatujafika kote huko. Ilikuwa muhimu katika hatua hii ya kwanza kujua nini tufanye.”