Usajili WMA ulivyochakachuliwa
Wakati hayo yakiendelea, imebainika kuwa baadhi ya WMA zilipewa usajili na mawaziri – Zakia Meghji, Anthony Diallo na Jumanne Maghembe – kwa kutumia sheria iliyofutwa.

Baadhi ya WMA hizo ni Mungata, JUHIBU, Endumeit na Mbomipa. Zilipewa usajili wakati zikiwa hazina sifa ya kuwa WMA bali ‘Pilot WMA’ chini ya Tangazo la Serikali Namba 283 la mwaka 2005.

WMA hizo zilipewa Usajili na Hati za Haki ya Matumizi ya Wanyamapori (Wildlife Resources User Right), kwa kutumia Sheria Namba 12 ya mwaka 1974 na Kanuni zake za mwaka 2002, wakati vyote hivyo vilifutwa mwaka 2005 kwa Tangazo la Serikali Namba 283.

Jumuiya ya JUHIBU ilipata usajili Novemba 11, 2005 kwa Sheria ya mwaka 2002 iliyofutwa Septemba 16, 2005. Ikapewa Hati ya Matumizi ya Wanyamapori Na. 00000559 iliyotolewa Februari 2, 2007.

Muungano wa Ngarambe na Tapika (Mungata) walipewa Hati ya Haki ya Matumizi ya Wanyamapori yenye Namba S.001. na kupewa Hati ya Haki ya Matumizi ya Wanyamapori yenye namba 00000558 Februari 2, 2007.

Mbomipa ilipewa hati ya usajili namba S. 018 Oktoba 11, 2006 na kukabidhiwa Hati ya Haki ya Matumizi ya Wanyamapori iliyotolewa Julai 6, 2007.