Kagasheki

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki

*Kiini macho chaibuka vitalu vya WMA
*Vyatangazwa Kagasheki akiapa Ikulu
*Ni kukamilisha ratiba, matajiri wavinasa

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, anakabiliwa na mtihani wa kwanza ndani ya wizara hiyo, baada ya kuibuka kwa kashfa mpya katika ugawaji vitalu 13 vya uwindaji vinavyomilikiwa na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs).

Vitalu hivyo ni tofauti na vile vilivyosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Ezekiel Maige. Habari za uhakika kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na katika WMA, zinaonyesha kuwa kutangazwa kwa vitalu hivyo kumefanywa haraka haraka siku Kagasheni na mawaziri wenzake walipokuwa Ikulu wakiapishwa.

Vitalu hivyo vipo katika madaraja matatu. Ada zake za maombi ni dola 1,000 (daraja la tatu); dola 2,000 (daraja la pili) na dola 5,000 (daraja la kwanza). Dola moja ni wastani wa Sh 1,570.

Kiinimacho cha kuvitangaza vitalu hivyo kilifanywa na Muungano wa Jumuiya Zilizoidhinishwa za Maeneo ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania, wenye ofisi zao jijini Dar es Salaam. Muungano huo, ingawa unajitanabaisha kuwa uko huru, unapata misaada na huduma mbalimbali za uendeshaji kutoka kwa ‘kampuni rafiki’ zenye vitalu.

Vitalu 13 vimetangazwa katika WMA 12. WMA hizo na vitalu vyake kwenye mabano ni Ngaramb-Tapika (Ngarambe-Tapika), Burunge (Burunge), Enduimet (Enduimet), Liwale (Liwale North na Liwale South), Ikona (Ikona), Uyumbu (Uyumbu), Indema (Makame), Makao (Maswa), Tunduru (Tunduru), Ipole (Ugunda), Mbomipa (Mbomipa) na Ukutu (Ukutu).

Uchunguzi unaonyesha kuwa kutangazwa kwa WMAs hizo kumefanywa kwa lengo la kukamilisha lengo tu, kwani tayari baadhi ya kampuni kubwa za kigeni zina mikataba.

“Wametangaza umiliki wa vitalu kuanzia mwaka 2013 hadi 2018… ukweli ni kwamba tayari kuna kampuni zenye mikataba na hizo WMA ya miaka 10, miaka 15 na kadhalika. Haiwezekani kampuni hizo zikanyang’anywa na kupewa kampuni nyingine mpya. Kufanya hivyo kutaibua migogoro,” kimesema chanzo chetu.

Aidha, imeelezwa kuwa kutangazwa kwa vitalu hivyo ni shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanaovimiliki na wanaovitaka, wakilenga kuhakikisha hawanyang’anywi au haviangukii kwa wengine kama ilivyotokea kwenye vitalu vilivyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii moja kwa moja.

Kuna habari kwamba baadhi ya viongozi waandamizi ndani ta Wizara ya Maliasili na Utalii, wameshitushwa na aina ya tangazo lililotolewa, na wanahoji iweje litolewe kabla ya Waziri Kagasheki kuingia ofisini.

Tangazo hilo limebainika kuwa na kasoro nyingi, jambo linaloweza kuifanya wizara ikaingilia kati na kuona linatangazwa upya.

Dosari nyingine kubwa imeelezwa kuwa ni kutangazwa kwa vitalu hivyo wakati hakuna kanuni mpya za WMA zinazokidhi matakwa ya Sheria Namba 5 ya Wanyamapori ya mwaka 2009.

Ingawa WMA zipo chini ya vijiji na halmashauri mbalimbali, Wizara ya Maliasili na Utalii ndiyo yenye dhima ya kusimamia rasilimali ya wanyamapori na nyara zinazotokana nao.