Kamishna aliyeteuliwa aanza ubadhirifu mali za Tume
*Waziri Lukuvi aapa kufa naye, Yambesi amvutia pumzi
Miezi miwili baada ya kuingia kazini kama Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, Kenneth James Kasseke, ameanza kuwatia shaka wapambanaji wa dawa za kulevya nchini kwa kuonyesha nia ya ubadhirifu.
Katika hali inayotia wasiwasi iwapo ataweza kuifanya kazi ya kupamnana na wauza ‘unga’ kwa uadilifu na ufasaha, Kasseke ameanza mchakato wa kujiuzia mali za tume hiyo kwa lengo la kudhoofisha utendaji wa taasisi hiyo.
Wakati Tume inamiliki magari matatu, ila mawili aina ya pick up yakiwa na hali mbaya, Kamishna Kasseke anataka kujiuzia gari pekee lenye nguvu, linalotumiwa kupambana na dawa za kulevya nchini.
“Tumepata mshituka mkubwa mno. Gari hili ni jipya kabisa halina hata miaka miwili tangu linunuliwe. Maafisa ndilo wanalolitumia kufukuza wauza unga na kupanda milima kwenda kuteketeza bangi huko Morogoro, Arusha na Rushoto – Tanga, lakini ajabu huyu baba ambaye ana miezi miwili tu ofisini anataka auziwe gari hilo.
“Hii ina maana akiuziwa hili gari, Tume itakuwa haina gari lolote linaloweza kusafiri safari ndefu na kupanda milima kama ya Morogoro kwa nia ya kuteketeza mashamba ya bangi. Ameandika barua rasmi kuomba kuuziwa gari hilo, na sisi hapa utumishi tukashangaa kweli kupokea ombi hili,” kimesema chanzo chetu kutoka Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Nakala ya barua hiyo, ambayo JAMHURI limeipata na kumpelekea Kasseke kwa njia ya Whatsapp, inakwenda kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, S. L. P. 2384, Dar es Salaam, ya Oktoba 17, 2014.
Barua hiyo inasomeka hivi: Yah: Maombi ya kuuziwa gari chakavu STK 5337 (Hard Top) Chasis Na. jTERB71j00—47106 Engine Na. 1HZ-0590111.
Kichwa cha habari chahusika.
Mimi ni Mtumishi wa Umma ambaye nimeteuliwa kuwa Kamishan wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini tangu tarehe 19/05/2014.
Ninaomba kuuziwa gari chakavu Iliyotajwa hapo juu iliyopo katika Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ili inisaidie kukidhi mahitaji ya usafiri katika utekelezaji wa majukumu ya kazi na familia baada ya saa za kazi. Pamoja na barua hii nimeambatanisha “salary slip”.
Natanguliza shukrani zangu za dhati.
K. J. Kasseke
Kamishna
Ombi hilo la kununua gari alilipitisha kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisa Tawala za Mkuu, Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, ambao wote wameliridhia.
Baada ya JAMHURI kupata taarifa hizo, iliwasiliana na Kasseke aliyekiri kuwa na nia ya kununua gari hilo, kwa kusema: “Ndiyo, nataka kulinunua,” alipoulizwa kwa nini anataka kununua gari ambalo si chakavu na tegemezi kwa Tume akaongeza: “Gari hili si tegemezi na ni chakavu, lakini kuna magari mengi tunayoyatumia kwenye Tume.”
Majibu hayo yasiyo na uhalisia, yalilifanya JAMHURI kuwasiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi, alipoulizwa juu ya nia ya Kasseke kununua gari la Tume alisema:
“Miezi miwili tu kazini ameishataka kununua gari? hii ni hatari! Ndo napata taarifa hizi, lakini nakuhakikishia nitazifanyia kazi kwa kina. Nitafute wiki ijayo nitakuwa na jibu sahihi. Hii haikubaliki,” alisema Lukuvi.
Kwa Upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yamesi, alishukuru kwa kupewa taarifa na kuahidi kulifuatilia kwa kina suala hili.
Mbali ya kuteuliwa Mei 19, 2014 kumridhi Kamishna Shekiondo aliyestaafu, Kasseke (58) ameingia rasmi ofisini Agosti 1, 2014 na hivyo kwa kutoa ombi la kunua gari Oktoba, wafanyakazi wa Tume wamesema kasi yake ya ubadhirifu inatisha.
Baadhi walimtuhumu kuwa anasaidiwa na ofisa mmoja kuendeleza mchezo wa kulipwa posho bila kufanya kazi, ingawa hilo yeye hakutaka kulizungumzia kwa kudai anataka ushahidi kama amewahi kufanya hivyo.
Tume hii inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa na hili ndilo gari pekee linalotegemewa hivyo likiuzwa itakuwa imeishia uwezo kabisa wa kufanya kazi kwa mujibu wa watumishi waliopo ndani ya Tume hii.