Bandari ya Dar es Salaam imetumbukia tena katika kashfa, baada ya viongozi wake kutajwa kutumia kampuni wanayoimiliki kupata zabuni licha ya kutokuwa na sifa.

Mgogoro mkubwa unafukuta bandarini hapo, kutokana na zabuni AE/016/2012/DSM/NC/01B ya kutoa huduma za kupakua na kupakia mizigo bandarini, iliyotangazwa mwaka 2013 kutolewa kwa mizengwe kwa kampuni ambayo viongozi wa Bandari wana vinasaba nayo.

Kibaya zaidi, tangu Machi 1, 2016 kampuni hiyo inayolalamikiwa, ya Hai Sub Suppliers na nyingine kama Portable Enterprises na Freight Meridian, zimeendelea kufanya kazi bila mkataba wowote, kwani nyongeza ya mkataba ziliopewa awali iliisha Februari 29, 2016.

Zabuni inayosumbua vichwa ilitangazwa kwa nia ya kupata mrithi wa kampuni hizo ifikapo mwaka 2014, mwaka uliolengwa kuwa kampuni hizo zingekuwa zimemaliza mkataba kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, kutokana na mvutano wa kisheria, hadi sasa zabuni hiyo haijatolewa kwa kampuni yoyote, baada ya nia ya kuipa Hai Sub Suppliers kuzimwa, hali iliyoulazimu uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kuziongezea muda wa kati ya mwezi mmoja na mitatu hadi atakapopatikana mzabuni mwingine.

Afisa Mwandamizi wa Bandari, ameiambia JAMHURI kuwa kitendo kinachofanywa na Bandari kutumia kampuni yao waliyotumia ujanja wa kumtanguliza mfanyakazi wa chini aonekane ndiye mwenye kampuni (bila kujali mgongano wa maslahi), ni cha hatari.

“Kaka nakwambia hii kitu ni hatari mno. Kampuni hii ya Hai Sub Suppliers imeendelea kupewa kila kazi ya Bandari ya Dar es Salaam, hali inayotishia hata usalama wa Bandari.

“Kampuni hii sasa imehodhi asimilia 90 ya kazi zote, na hofu yangu ni kuwa ikitokea siku kampuni hii ikaamua kugoma, Bandari ya Dar es Salaam itasimamisha shughuli zote.

“Kwa kiwango cha kazi ilizopata kampuni hii nisiyojua inapata wapi nguvu, inaweza kufika mahala ikahujumu Bandari au ikaigeuza Bandari kuwa mateka wake. Uamuzi huu wanaofanya mameneja wa Bandari ya Dar es Salaam ni wa hatari kweli, ni lazima Serikali iingilie kati na kuvunja mtandao huu, kazi zigawanywe kwa kampuni tatu hadi tano, kwa nia ya kuongeza ushindani na kulinda usalama wa Bandari,” alisema afisa huyo kwa uchungu.

Kampuni hii inayopokea kati ya Sh milioni 300 na 400 kwa mwezi kutoka Bandari, malipo yake yalianza kuongezeka baada ya Bandari kupata Kaimu Mkurugenzi, Hebel Mhanga. Mhanga alianza kukaimu kazi hiyo Desemba, 2013 na ilipofika Mei, 2015 inaelezwa alianza kuzinyang’anya kazi kampuni nyingine na kuzirundika kwa Kampuni ya Hai Sub Suppliers, iliyotajwa na Mahakama kuwa haina sifa ya kufanya kazi za Bandari.

“Serikali ikaingie kwa wahasibu ione invoice na kiasi kinacholipwa kwa Hai Sub Suppliers ione malipo yalivyoanza kuongezeka tangu Mei, 2015. Kampuni hii ina uhusiano wa moja kwa moja na baadhi ya mameneja wa Bandari wachunguzwe,” alisema mtoa habari wetu.

Uchunguzi wa JAMHURI, unaonesha kuwa Kampuni ya Hai Sub Suppliers kwa sasa imepewa kazi katika gati 7 kati ya 8, imepewa kazi za maghala 7 kati ya 8, imepewa kazi ya usafi wa ofisi, usafi wa jumla, kushusha na kupakia malori na mabehewa.

Kampuni ya Portable Enterprise Limited imepewa kazi moja kwenye gati Na 8 na Kampuni ya Freight Meridian imepewa kazi moja tu katika ghala Na 8. Mkataba wa awali wa Hai Sub Suppliers ulikuwa wa kupakua na kupakia meli za magari.

Katika hali isiyoelezeka, kampuni hii ilipata mkataba mnono wa kufanya kazi na taasisi kubwa kama Bandari bila kuwa na sifa stahiki. Tangu mwaka 2012 ilipopewa mkataba wa kwanza, Hai Sub Suppliers kumbukumbu zinaonesha haikuwa na Namba ya Mlipa Kodi (TIN) badala yake ilikuwa inatumia Na 102-303-229, ambayo ni namba ya mtu binafsi anayejulikana kwa jina la Hidaya Ibrahim Amri.

Hapana shaka kadri muda ulivyokwenda walipata ushauri wa kisheria na hasa masuala ya kodi yasiyoelezeka kama kampuni hii ilikuwa inalipa kodi kwa njia ipi, ilipofika Mei 22, 2015 ikiwa imekwishafanya kazi miaka zaidi ya mitano na Bandari, ndipo kampuni hii iliposajiliwa Brela na kisha Mei 25, 2015 ilipata TIN namba 127-110-069, kisha ikaomba ipewe zabuni kubwa zaidi na ikapigiwa chapuo na uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kuwa ndiye mshindi.

Januari 19, mwaka huu Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma (PPAA), ilitoa hukumu juu ya kesi iliyofunguliwa na kampuni – Nagla General Services Limited, Portable Enterprises Limited na Carnival Investment Limited wakipinga upendeleo unaovunja sheria kwa kuipatia zabuni Hai Sub Suppliers bila kuwa na sifa.

Katika hukumu hiyo, iliieleza Bandari ya Dar es Salaam kusitisha utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Hai Sub Suppliers Limited, kwani haikuwa na uzoefu wa miaka miwili unaotakiwa kisheria. Uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam unajenga hoja kuwa Hai Sub Suppliers ni taasisi ile ile kwani ilichofanya ni kujiondoa katika kufanya biashara na Bandari kama mtu binafsi (sole proprietor) na kugeuka kampuni ilipofika mwaka 2015. 

JAMHURI imezungumza na mfanyakazi wa Bandari, ambaye ni mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Hai Sub Supplier, Yusufu Ibrahim, ambaye anamiliki asilimia 50 ya kampuni hiyo yenye zabuni ya kufanya kazi katika Bandari ya Dar es Salaam, aliyesema:

“Ni kweli nilikuwa namiliki kampuni hii, lakini nimefilisika.” 

Alipoulizwa ni lini amefilisika na ni lini ameacha kumiliki kampuni hii, akasema: “Sikusikii.” Akakata simu. JAMHURI ilimpigia simu mara mbili tena, akawa anapokea na kuiacha simu hewani bila kuzungumza. 

JAMHURI imepata nakala za malalamiko ya wazabuni waliomwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, kuingilia mgogoro huu unaotishia amani kwani vibarua kutoka kampuni nyingine wanajipanga kugoma kutokana na wale wa kampuni ya Hai Sub Suppliers kupata kazi kila siku, huku wengine wakipiga miayo.

Kaimu Meneja wa Bandari, Mhanga, alipoulizwa juu ya tuhuma hizo kuwa yeye ni mmiliki wa kampuni ya Hai Sub Suppliers kwa mgongo wa mfanyakazi wa kada ya chini wa Bandari, alisema yeye hahusiki na kampuni hiyo anasingiziwa.

“Mimi napenda nikuhakikishie kwamba kwa kitu ambacho nimekifanya, kama nilikifanya juzi, kweli nitaendelea kukwambia kwamba ni kweli ni mimi niliyekifanya, kwa sababu naamini kwamba wakati nakifanya, nilikuwa na nia gani. Hata kama mazingira yamebadilika, lakini nitakwambia kwamba hiki wakati nakifanya, mazingira yalikuwa moja, mbili, tatu…

“Mimi si mtu wa kutafuta makampuni ya kufanya biashara bandarini. Mimi mtazamo wangu wa maisha siyo mtu wa kutafuta utajiri. Mimi ni mtu ambaye nafikiria kutumikia nchi, nimefanya kitu gani ambacho nitakapokuwa nimeondoka kitakuwa kinatazamwa kwamba kile pale kilisimamiwa na Mhanga.

“Lakini maisha yangu nataka kuishi maisha ya kawaida kabisa ya Mtanzania, maisha ya watoto wangu waende shule, waishi maisha mazuri, siyo niwe na mali ya kujilimbikizia. Mimi nitafika mahala nitakufa tu,” alisema Mhanga.

Suala la Hai Sub Suppliers kufanya shughuli karibu zote za Bandari, alisema hata yeye kwa ajili ya usalama wa Bandari linamtia hofu, na alipoulizwa wanazipataje, akasema: “Kwa mujibu wa sheria na taratibu za zabuni.”

Aliishutumu Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 inayowapa nafasi wazabuni walioshindwa kulalamika, akisema imezaa mvutano usio na ukomo kwa maana waliokosa zabuni hawakubali kushindwa.

Mhanga alipoulizwa kama Hai Sub Suppliers walishinda kihalali, kwa nini PPAA imeamuru wasipewe zabuni? Alisita kidogo kisha akasema, kinachopiganiwa ni maslahi binafsi ya hizo kampuni kwani Hai Sub Suppliers wamekuwa wakifanya nayo kazi tangu mwaka 2012, hivyo anashangaa kuona hawaitambui iliposajiliwa rasmi mwaka 2015. 

“Kimsingi hata vibarua ni wale wale, hivyo iwe hiyo Hai Sub au nyingine, wanachopigania ni maslahi binafsi tu,” alisema.

Amezishutumu kampuni shindani katika zabuni hiyo kuwa mkurugenzi mmoja amekuwa anaingiza zaidi ya kampuni tatu kwenye zabuni moja, hivyo inaposhinda yoyote kati ya zinazoteuliwa, basi anabaki mtu yuleyule, lakini akasema yeye si msemaji wa Hai Sub Suppliers watafutwe wenyewe.

Kuhusu madai ya kampuni ya Hai Sub Suppliers na nyingine kuendelea kufanya kazi bila mkataba tangu Machi 1, mwaka huu, amesema anachofahamu ni kuwa amekwishapitisha mikataba ya nyongeza kwa kampuni hizo na kama haijawafikia, wataipata si muda mrefu.

Kuhusu suala la hatima ya zabuni hiyo inayopigwa danadana tangu mwaka 2013, Mhanga amesema wao mara zote wanaomba ushauri wa PPRA na wamefanya hivyo katika hili, hivyo ikibidi kuitisha upya zabuni au kuwapa wazabuni waliokuwa na sifa wanaofuata baada ya Hai Sub Suppliers kutamkwa na Mahakama kuwa haina sifa, atafuata ushauri wa PPRA.

Kwa muda mrefu Bandari ya Dar es Salaam imekuwa na kashfa za hapa na pale ikiwamo wizi wa makontena ulioleta mtikisiko mkubwa nchini, ilipobainika kuwa baadhi ya matajiri wakubwa wameshiriki dhambi ya kukwepa kodi.

Baada ya gazeti la JAMHURI kufukua kwa kina utendaji mbovu katika Bandari nchini na kuwezesha kuziba mianya ya uvujaji wa mapato ikiwamo uchunguzi wa aina yake uliobainisha wizi wa mafuta kutokana na kutotumika kwa flow meters, sasa inaelezwa kuwa wakubwa wanataka kutumia kampuni za zabuni kujipatia pato la ziada.

Kubwa linaloshtua ni suala la uzoefu katika kufanya kazi za bandarini na historia ya wizi wa ajabu ulioibuka kuanzia miaka ya 2010 ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambayo Bandari yenyewe na kampuni chache zilikuwa zinafanya kazi ya kushusha na kupakia mizigo bandarini.