*Wadaiwa kukingia kifua waliotafuna fedha za wastaafu
*Msaidizi wa JK Mtawa abeba siri nzito, Katibu anena
*Mabilioni ya Hazina, bilioni 1.7 za NORAD zaliwa
Kashfa nzito inawazunguka watendaji wakuu wa Ofisi ya Rais Ikulu, wanaodaiwa kushirikiana na maofisa kadaa wa Hazina ama kutafuta fedha za wastaafu au kuwakingia kifua wabadhilifu.
Maofisa hao wanalalamikiwa kuwazuia waliokuwa wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kukutana na Rais, Jakaya Kikwete wamueleze malalamiko ya mapunjo ya mafao yao.
Msaidizi wa Rais Kikwete, Kassim Mtawa, ndiye anayelalamikiwa zaidi kwamba anawakingia kifua maofisa kadhaa wa Serikali waliotafuna mamilioni ya fedha za wastaafu wapatao 933.
Wastaafu hao wanahitaji kukutana na Rais wamweleze malalamiko yao baada ya kuchoshwa na danadana nyingi walizopigwa katika ofisi mbalimbali za Serikali kwa zaidi ya miaka 16 sasa bila mafanikio.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa viongozi wa kamati ya wastaafu hao wanakwenda Ikulu karibu kila siku wakihitaji kuonana na Rais wamweleze malalamiko yao lakini juhudi hizo zimeendelea kugonga ukuta.
Mtawa aruka kimanga
Mtawa alipotakiwa na Jamhuri kuzungumzia malalamiko hayo kwamba ndiye kikwazo kikubwa, amekanusha tuhuma hizo na kuwatupia mzigo huo Katibu wa Rais, Prosper Mbena na Msajili wa Hazina, Elipina Mlaki.
Huku akizungumza kwa jazba kiasi, Mtawa amebeza malalamiko ya wastaafu hao akisema ni watu wanaopoteza muda kwa vyombo vya habari na kwamba madai yao hayana ukweli wowote.
“Hizo habari siyo za kweli, hao [wastaafu] wanawapotezea muda, liko kwa Katibu wa Rais, Mbena, mimi ni Msaidizi wa Rais, anayeruhusu watu kuonana na Rais ni Katibu wa Rais,” amesema Mtawa na kuendelea:
“Walikuja [viongozi wa wastaafu] mimi nikawaunganisha na Katibu wa Rais. Lakini hao [wastaafu] ni waongo, suala lao hasa liko kwa mama Mlaki [Elipina] ambaye ndiye analijua A hadi Z.”
Mbena awashutumu wastaafu
Kwa upande wake, Mbena alipotakiwa na Jamhuri kuzungumzia suala hilo, naye ameishia kuwashutumu wastaafu hao akidai madai yao ni ya uongo.
“Hizo habari si za kweli, hao wazee ni waongo, madai yao si ya kweli,” amesema Mbena.
Nyaraka zaonyesha kinyume
Jamhuri inazo nyaraka zenye kuonyesha kuwa wastaafu hao 933 wanaidai Serikali zaidi ya Sh bilioni saba ambazo ni mapunjo ya mafao yao mbalimbali baada ya kustaafishwa kazi UDSM mwaka 1995 na 1996.
Baadhi ya wastaafu waliozungumza na JAMHURI kwa siku na nyakati tofauti kwa sharti la kutotajwa majina, wamesema uongozi wa chuo hicho umekuwa ukipotosha kwamba idadi halisi ya wastaafu hao ni 638.
“Awali idadi ya wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliopaswa kupunguzwa miaka hiyo ni 265 kulingana na fungu la fedha zilizokuwa zimetengwa, lakini wakaiongeza hadi 638 kwa sababu wanazozijua wao,” amesema mmoja wa wazee hao.
Nyaraka zinaonyesha kuwa Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) Oktoba, mwaka 2002 liliipatia Serikali kupitia Hazina msaada wa Sh bilioni 1.727 kuchangia malipo ya mafao ya wastaafu hao.
Wastaafu hao wamesema nyaraka nyingine zinaonyesha kuwa Juni 2012, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilipokea Sh milioni 460 kwa ajili ya malipo ya wastaafu hao lakini zikaelekezwa katika matumizi mengine ambayo hayajabainishwa.
Pia inaelezwa kwamba mwaka 2008 hundi za sehemu ya malipo ya wastaafu hao zilitayarishwa lakini zikazuiwa na ‘wanjanja’ wachache na hadi sasa haijajulikana zilikoelekezwa.
Inaelezwa pia kwamba viongozi wa kamati ya wastaafu hao wamefanikiwa kushinda mara kadhaa vishawishi vya kupokea rushwa kutoka kwa maofisa husika serikalini waache kufuatilia madai hayo.
Mwaka 1997 wastaafu hao walifungua kesi ya madai Na 299 chini ya Jaji Kalegea, lakini ikafutiliwa mbali kutokana na kukosa vielelezo wakati huo. Wazee hao sasa wanasema vielelezo wanavyo ila hawana fedha za kuwalipa mawakili kukata rufaa.
Profesa Mukandala ajitetea
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala, yeye alipoulizwa amesema ofisi yake imefunga kushughulikia malalamiko ya wastaafu hao baada ya mahakama kufutilia mbali kesi yao ya madai dhidi ya Serikali kupitia Hazina.
Hata hivyo, Profesa Mukandala amesema bado wastaafu hao wana haki ya kukata rufaa iwapo wanadhani hawakutendewa haki katika hukumu iliyotolewa na mahakama.
“Haya mambo yote yameamriwa na mahakama baada ya kuona madai haya hayana msingi… sisi tulikuwa tayari kuwasikiliza na tungewasikiliza, lakini sisi kama taasisi ya Serikali lazima tuheshimu mahakama kwani ndicho chombo cha sheria kinachotambulika na mamlaka husika.
“Sisi kama chuo (UDSM) tunajua hili suala limeisha, lakini kama wao wana hoja nyingine basi litaangaliwa na vyombo husika lakini sisi tunajua mahakama ilishaliangalia suala hili na kulifunga,” amesema Profesa Mukandala.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa mamlaka husika, hususan Ikulu, Wizara ya Fedha na UDSM zinasuasua kulipatia ufumbuzi suala la madai ya wastaafu hao, wengi wao sasa wakiwa ni wazee wa umri kati ya miaka 60 na 80.
Luhanjo adaiwa kulikoroga
Katibu Mkuu Kiongozi aliyestaafu, Philemon Luhanjo, ni miongoni mwa viongozi wa Serikali walioshiriki kwa nyakati tofauti kushughulikia suala hilo bila mafanikio huku wengine wakijaribu kuuaminisha umma kuwa wastaafu hao hawastahili kulipwa wanachokidai.
JAMHURI limepata nyaraka kadhaa zinazoonesha jinsi makatibu wakuu tofauti wa ofisi hizo walivyotoa maelekezo mbalimbali kwa nyakati tofauti, ambayo hayakuweza kulipatia ufumbuzi suala la wastaafu hao.
Nyaraka hizo ni pamoja na barua yenye Kumb. Na. CEA110/404/IV/01 iliyotoka Ikulu kwenda Hazina ikiwa imesainiwa na Msaidizi wa Rais, Kassim Mtawa, Januari 23, 2008.
Wazee wagonga mwamba wizarani
Uongozi wa Kamati ya Wastaafu wa UDSM umefanya juhudi za kuwaona viongozi wa wizara za Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, mawakili wa kujitegemea, chama tawala (Chama Cha Mapinduzi – CCM) waingilie kati suala hilo kuwawezesha kulipwa mapunjo ya mafao yao bila mafanikio.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeagiza malalamiko ya wastaafu hayo yaendelee kushughulikiwa ikiwa ni pamoja na wao (wastaafu) kupeleka mchanganuo wa mapunjo yao lakini hadi sasa hakuna kilichotekelezwa hata baada ya kupeleka mchanganuo husika.
Msajili wa Hazina, Elipina Mlaki, hakupokea simu mara kadhaa wala kujibu ujumbe mfupi wa maneno (sms) kutoka JAMHURI juu ya sakata hilo.
Balozi Ombeni anena
Katibu Mkuu Kiongozi wa Ofisi ya Rais – Ikulu, Balozi Ombeni Sefue, alipoulizwa na JAMHURI kuhusu sakata hilo alisema yuko likizo, lakini Wizara ya Fedha ndiyo inastahili kulitolea ufafanuzi.
“Niko likizo. Waliostaafu miaka hiyo inabidi wazungumze na Wizara ya Fedha,” amesema Balozi Sefue.
Waziri Mgimwa ‘auchuna’
Kama ilivyotokea kwa Mlaki, Waziri wa Fedha, William Mgimwa, aweze kuzungumzia suala hilo ziligonga ukuta baada ya JAMHURI kufika ofisini kwake mara mbilia bila kufanikiwa kumwona na hata simu yake imekuwa ikiita bila kupokewa.