Nimemfahamu zaidi Jenerali George Waitara wakati huo akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali.
Ukaribu wangu kwenye shughuli mbalimbali za kijeshi, uliochochewa na mapenzi yangu kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ulinisaidia kumwona mara kwa mara akiwa kwenye shughuli kadha wa kadha, akimwakilisha Mkuu wa JWTZ wa wakati huo, Jenerali Robert Mboma.
Nakumbuka fununu za kung’atuka kwa Jenerali Mboma zilipoenea; siku moja tukiwa katika Hoteli ya Sea Cliff, Dar es Salaam, nilimsogelea Jenerali Waitara na kwa utani nikamwambia; “Jenerali, nadhani wewe ndiye mkuu wa majeshi ajaye”. Alicheka kwa namna ambayo aliona kama nafanya ‘uchuro’. Siku chache zilizofuata, akatangazwa kuwa Mkuu wa JWTZ. Baadaye tulikutana bungeni Dodoma. Nikamkumbusha, na sote tukacheka kwa furaha. Tukapata picha ambayo nimeihifadhi.
Nimejaribu kuyaeleza haya kuonesha imani yangu kwa Jenerali Waitara.
Siku kadhaa zilizopita, Rais John Magufuli, kamteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA). Ni mtu mpole, mweledi na msikivu. Ni kamanda mahiri na mwenye ujuzi wa hali ya juu katika medani za mapambano ya ardhini. Lingekuwa jambo la maana kwa majangili kulifahamu hilo na kutafakari ili waone kama bado wana sababu au ubavu wa kuendelea na ujangili.
Shirika hili linasimamia hifadhi 16. Hifadhi hizo kwa mtiririko wake wa ukubwa kwa kilometa za mraba kwenye mabano ni kama ifatavyo; Ruaha 20,300, Serengeti 14,763, Katavi 4,471, Mkomazi 3,245, Mikumi 3,230, Tarangire 2,600, Udzungwa 1,900 Mlima Kilimanjaro 1,668, Mahale 1,618, Saadani 1,100, Arusha 552, Rubondo 457, Kitulo 413, Ziwa Manyara 648, Gombe 56, na Saanane (2.8).
Kwa jumla, Tanapa ina ukubwa wa kilometa za mraba 57,023.8. Ukubwa huu unazidi nchi ya Togo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 56,785. Kwa maneno mengine, ukubwa huu ni zaidi ya ukubwa wa Rwanda na Burundi zikiwekwa pamoja zikiwa na kilometa za mraba 54,172. Hili ni eneo kubwa mno.
Tanapa imekaa miaka mitatu bila kuwa na Bodi ya Wakurugenzi. Wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alikaririwa akisema utalii nchini mwetu unachangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni. Huu ni mchango mkubwa. Nje ya vivutio vya Tanapa, kuna Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mapori ya Akiba kama Serous.
Jenerali Waitara amepewa kazi ya kuiongoza Tanapa wakati ikikabiliwa na matatizo mengine ya uhifadhi. Anaingia kwenye vita ambayo bahati mbaya maadui wako ndani na nje ya Tanapa. Anaingia kwenye mapambano dhidi ya wanasiasa walioamua kwa makusudi kabisa kuwa maadui wa uhifadhi.
Jenerali Waitara anaingia kwenye mapambano dhidi ya wenye mifugo ambao wengi wao ni wanasiasa, maofisa wa Serikali na watu wenye ukwasi – wamo wa ndani na wengine kutoka nje ya nchi.
Amekabidhiwa kazi hii ilhali maeneo kama ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) yakiwa yamevamiwa na wafugaji walioingia ndani hadi kilometa 20. Wamefanya hivyo baada ya ‘kuliua’ Pori Tengefu la Loliondo.
Siku chache baada ya kuagwa rasmi pale katika Kambi ya Twalipo, Dar es Salaam, Jenerali Waitara alitamka kuwa hana mpango wa kuwa mwanasiasa! Ulikuwa uamuzi mzuri, lakini kwa kuwa mwenyekiti wa Bodi, ajue anapambana na wanasiasa. Kuna waziri mmoja kwenye wizara hiyo aliyeamua kushinikiza Bodi ya Tanapa ya wakati huo ugharimie Miss East Africa kwa kulipa Sh milioni 500. Alipokataliwa, akaibua majungu. Fikiria, zitumike Sh milioni 500 kwa mashindano ya urembo ilhali watoto katika vijiji vilivyo kando ya hifadhi wakiketi chini kwa kukosa madawati!
Kama nilivyosema, uhifadhi katika nchi hii unaathiriwa na wanasiasa, kwa hiyo jenerali awe tayari kukabiliana nao.
Jenerali Waitara, akiwa na ‘roho nyepesi’ kuyakabili makombora, vijembe, kejeli na vitisho vya wanasiasa, anaweza kukata tamaa. Hili si jambo la kutarajiwa hata kidogo, hasa ikizingatiwa kuwa msamiati wa kushindwa kamwe haumo kwenye maisha ya kamanda wa ngazi yake! Kule anakotoka, inaaminika kuwa ‘woga ndiyo silaha dhaifu kuliko kote.’
Majangili na watu wanaotumia hifadhi na mapori yetu kwa manufaa yao, wana nguvu na ushawishi mkubwa. Mtandao wao umeenea ndani na nje ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Wahusika kwenye matukio haya mawili si watu wadogo wala hohehahe. Ni watu wenye ukwasi wa kutosha. Wana uwezo kifedha na hata kisiasa. Kuna wabunge majangili. Wanajulikana. Tutakusaidia kukupatia majina.
Jenerali Waitara atambue anakwenda kupambana na wabunge wenye ng’ombe wengi – maelfu kwa maelfu – wanaoingizwa kwenye Hifadhi za Taifa kwa ajili ya kunenepeshwa na baadaye kuuzwa.
Atambue kuwa kuna ng’ombe wa Wanyarwanda, Warundi, Wakenya na Waganda ambao, kutokana na sera na sheria za ardhi katika nchi zao, hawana maeneo ya malisho; hali inayowafanya wawatumie Watanzania, ama kwa ujira, au kwa kuwagawia sehemu ndogo ya mifugo ili wafanye kazi ya kuwachungia mifugo.
Jenerali Waitara atambue pia kuwa mifugo inayoingizwa katika Hifadhi za Taifa inatumiwa kama mbinu ya utakatishaji fedha. Wenye fedha hizo wananunua mifugo, wanainenepesha, kisha wanaiuza. Fedha wanazopata zinaonekana ni fedha halali kwa sababu zimetokana na kazi halali ya ‘ufugaji’.
Uongozi wake utakapoanza kushughulikia tatizo la mifugo kwenye hifadhi, atapata upinzani mzito kutoka kwa wahusika.
Operesheni Tokomeza haikuwa mbaya kama iliyotangazwa. Ukiacha dosari za hapa na pale, ilisaidia kweli kweli kupunguza kasi ya uuzaji wanyamapori hasa tembo, faru na wengine. Watu wenye maslahi, kwa kuwatumia wabunge, walihakikisha Serikali inayumbishwa kiasi cha mawaziri kadhaa kujiuzulu na wengine kutenguliwa uteuzi wao. Kufutwa kwa operesheni hiyo kukawa ushindi mkubwa kwa majangili na wahalifu wengine, wakiwamo wachoma mkaa, wafanyabiashara ya magogo na kadhalika.
Jenerali Waitara, bila shaka yoyote, anatambua dhamira njema ya Rais John Magufuli katika suala zima la kuwa na Tanzania mpya. Uongozi wake usiwe wa kusubiri aambiwe atekeleze nini, bali yeye na wajumbe wake na kwa kushirikiana na menejimenti ya Tanapa wawe chachu ya ubunifu na usimamizi wa uamuzi mbalimbali watakaokuwa wameufikia.
Maslahi ya watendaji, hasa wale ndugu zetu wanaoshinda na kukesha wakilinda rasilimali hii, hayana budi kutazamwa upya. Najua NCAA haipo kwa Jenerali Waitara, lakini nitoe mfano mdogo halisi nilioushuhudia Ngorongoro miezi kadhaa iliyopita.
Tukiwa katika gari, karibu na eneo la juu kabisa ambako watalii husimama ili waweze kuifaidi mandhari nzuri ya Ngorongoro, askari wawili wa wanyamapori, wakiwa na silaha wakasimamisha gari letu. Wakaomba lifti. Baada ya kuwadadisi, ikaonekana suala la usafiri lilikuwa tatizo.
Hapa ni Ngorongoro, lakini naamini hali kama hiyo ipo katika Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na kwingineko. Mazingira ya aina hiyo yanaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazowasukuma askari na watumishi wengine wa ngazi za chini kushiriki vitendo vya ujangili.
Jenerali Waitara ajitahidi kuishawishi Serikali Kuu iiruhusu Tanapa iweze kuajiri askari wake kadri ya mahitaji, badala ya kupangiwa kota kutoka Utumishi.
Narejea kumweleza Jenerali Waitara kuwa amepewa kazi wakati hali ya Hifadhi za Taifa ikiwa mbaya. Tanapa ina watendaji wengi weledi na wenye ari ya kulinda rasilimali hii. Wanakwamishwa na mwingiliano wa siasa na ukosaji ‘maamuzi’ (uamuzi) unaosababishwa na hofu, hasa wanapogusa maslahi ya wanasiasa na matajiri kadhaa.
Kama alivyosema Rais Magufuli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni mwanajeshi mwenye cheo cha Meja Jenerali; Mwenyekiti wa Bodi ya Tanapa ni Jenerali. Nguvu hizi zikiunganishwa, rasilimali hii ya wanyamapori na misitu katika ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 57,000 itakuwa imepata tiba.
Jangili gani mwenye uwezo wa kuwatisha au kuwashinda majenerali hawa? Simuoni. Ni wajibu wetu wapenda uhifadhi kuwaunga mkono. Karibu sana Jenerali Waitara.