Wapendwa waamini, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, nanyi nyote ndugu zangu wenye mapenzi mema! Baada ya Mkutano Mkuu wa SECAM, huko Kinshasa ambao pia ulihitimisha kipindi changu cha miaka sita na nusu kama Rais wa SECAM, napenda kuwaletea salamu za mkutano mkuu huo kwa kutafakri pamoja nanyi kipengele kimoja kati ya vingi vilivyozungumzwa katika mkutano huo: Wajibu wa Viongozi wa watu Barani Afrika kutekeleza haki kwa kila mwana nchi pasipo kukawia wala kusitasita.
Nimechagua kipengele hicho cha mkutano wa SECAM kwa sababu ya umuhimu wake katika mazingira ya sasa ya nchi yetu ya Tanzania. Lengo langu ni kuchangia katika kuhakikisha kwamba ninawekwa misingi imara kwa ajili ya taifa letu kwa leo na kesho.
Kwamba waamini Wakristu katika Tanzania wamekosa kutekelezewa haki kama raia wa taifa hili kwa miaka ya karibuni ni dhahiri kabisa. Mifano wazi ni matukio ya hivi karibuni ya: i) kumjeruhi vibaya sana Mheshimiwa Padre Ambrose Mkenda kule visiwani Zanzibar ii) Mauaji ya hayati Padre Evarist Mushi pia huko visiwani Zanzibar iii) Mashambulizi ya uharibifu wa makanisa ya madhehebu mbalimbali ya Kikristu kule Mbagala jijini Dar es Salaa.
iv) Mauaji ya ukatili wa kinyama ya Mchungaji Mathayo Kachila wilayani Chato v) Mashambulizi ya kutupa bomu kati ya waamini Wakatoliki waliokuwa wakijiandaa kwa ibada ambayo ilipangwa kuongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu Francisco Padilla – Mjumbe wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania – akishirikiana na Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat L. Lebulu wa Arusha. Shambulizi hilo, kama tunavyofahamu wote, lilipelekea vifo vya waamini watatu papo hapo na kujeruhiwa waamini wengine wengi.
Kwamba maafa yote hayo yalikuja baada ya mihadhara ya muda mrefu ya kuwatukana Wakristu na kutishia vifo vya viongozi wa Wakristu na kudai wazi wazi kuondolewa kwa Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania, inajengwa hisia za moja kwa moja kwamba wapo watu wanaoanza kutekeleza matishio yao ya mihadhara dhidi ya Wakristu.
Hata ikisemekana kwamba mashambulio hayo yanaweza yakasukumwa pia na watu wenye malengo yasiyo ya kidini, ukweli wa uwepo wa mihadhara ya vitisho kabla ya matukio yanawatwika wana mihadhara hiyo jukumu la kuhakikisha kwamba si wao wanaohusika. Katika matukio hayo yote, viongozi wa Wakristu pamoja na waamini wao kamwe hawakujichukulia hatua za kutaka kulipiza kisasi aidha kwa maneno au kwa matedo.
Hatua yoyote ya kulipiza kisasi ingeleta maafa kwa watu wengi wasio na hatia. Msimano huo wa subira ambayo kwa wanadamu wengine inaonekana ni udhaifu au hata upumbavu unajengwa juu ya mafundisho ya Mwanzilishi wa imani na dini ya Kikristu – Bwana wetu Yesu Kristu mwenyewe ambaye waamini wake wa kweli hawadiriki kumsaliti. Alitoa maisha yake kwa ajili ya watu; wala hakumwua mtu ili kuimarisha dini yake.
Hata hivyo, kutotaka kulipiza kisasi hakuna maana yakutodai haki itendwe na wale wenye jukumu hilo ndani ya Taifa letu la Tanzania. Kushindwa kudai haki itendeke baada ya kumwagwa damu ya watu wasio na hatia ingekuwa ni usaliti wa Mungu mwumbaji Mwenyewe. Yeye alimkumbusha Kaini baada ya kuwa amemwua nduguye Abel kwamba kilio cha damu ya nduguye kilimfikia Mwenyezi pamoja na kwamba ardhi ilijaribu kuificha hiyo damu.
Ni kwa sababu hiyo, Waamini Wakristu wote nchini Tanzania pamoja na watu wengine wengi wenye mapenzi mema wameendelea bila kuchoka kutaka Serikari ya Tanzania itekeleze wajibu wake wa kuhakikisha kuwa haki inatendeka hasa kuhusu damu ya watu wasio na hatia iliyomwangwa nchini mwetu.
Kwa bahati mbaya, madai hayo ya haki au yamepuuzwa kwa kauli zenye kejeli au kwa kutolewa ahadi za kuchukuliwa hatua za kisheria ambazo kamwe hazikuzaa matunda ya kuonekana. Watu watangoja hadi lini kuona kwamba serikali inakusudia kweli kutenda haki? Ni vizingiti vikubwa kiasi gani vinavyoizuia serikali isitekeleze wajibu wake licha ya ahadi zake nyingi?
Ombi langu kwa serikali yetu ni kwamba wale wanaohusika wasiendelee kupuuza maombi ya haki za Wakristu kama vile za Watanzania wengine wote. Kufanya hivyo ni kuitafutia nchi yetu balaa kubwa katika siku zijazo. Kwa waamini Wakristu, ombi langu ni kwamba tusitumbukizwe kwa namna yoyote katika matendo ya kulipiza kisasi.
Kwetu viongozi wa Kanisa, Mkutano wa SECAM wa Kinshasa umetutaka tusikubali kugawanyika katika swala muhimu la kutetea haki za Kanisa letu na za watu wote barani Afrika.
Kwetu tuliokwisha kutumbukia katika mitego ya kugawanyika, sharti tujutie makosa yetu mbele ya Mwenyezi Mungu na kurudi kwenye umoja pamoja na viongozi wenzetu. Wale walio imara hadi sasa, wamwombe Mwenyezi Mungu kudumu katika umoja na Kanisa.