Na Isri Mohamed
Beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe amesema sababu zilizomfanya mshambuliaji wa Al Ahly Tripoli, Agostinho Cristóvão Paciência ‘Mabululu’ kumkimbilia na kumshika mkono ni kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuzuia mashambulizi yao.
Mabululu alionekana akizungumza na Kapombe baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza za mchezo wa kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF CC) kati ya Simba vs Al Ahly Tripoli uliochezwa Jumapili ya Septemba 22, 2024 katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam uliomalizika kwa mnyama kupata ushindi mnono wa mabao 3-1.
Awali watu wengi akiwemo Meneja wa Simba walivyomuona Mabululu anamkimbilia Kapombe wakahisi huenda anataka kugombana nae kutokana na presha ya mchezo ambapo mpaka wanaenda mapumziko Tripoli walikuwa nyuma kwa bao moja.
“Alinikamata mkono na kuniita jina ‘Kapombe’ , Zaidi alichokuwa anazungumza ni kunipongeza na ku ‘Appreciate’ Nilichokifanya, aliona ni wakati sahihi wa kunipongeza na mm nikaona ni jambo jema kwa sababu si kawaida kwa mchezaji wa timu pinzani kukufata moja kwa moja na kukueleza kitu kama hicho, niliona ni Fair play iliyopitiliza”
“Tulivyorudi kipindi cha pili tukakutana tena kwa sababu mimi ndiye nilipewa jukumu la kumkaba kwenye kona, mechi ilivyoisha hatukuzungumza tena kwa sababu alipewa kadi nyekundu, hata mawasiliano hatujabadilishana” amesema.
Aidha Kapombe amesema hii si mara ya kwanza kwa wachezaji wa timu pinzani kumfata na kumpongeza, imewahi kutokea pia kwa mlinzi wa Al Ahly, Ramy Rabia ambaye walibadilishana mpaka jezi.