Na Mwandishi Wetu
Umewahi kutulia na kumtazama kwa jicho la tatu kiungo wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam na timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Mzamiru Yassin?
Kwa upande mwingine, unamfuatilia kwa umakini kiungo wa Klabu ya Chelsea jijini London, England na timu ya taifa ya Ufaransa, Ngolo Kante?
Kama ni shabiki makini wa soka la kisasa, nina uhakika tayari kuna picha umeipata kichwani mwako.
Katika eneo lile lile la Kante pale Chelsea na Ufaransa, ndilo eneo hilo hilo analocheza Mzamiru akiwa na mabingwa watetezi wa soka Tanzania Bara, Simba na Taifa Stars.
Licha ya ukweli kuwa Mzamiru ana wajihi na Kante katika vitu vingi, bado kuna kitu cha ziada ambacho Mzamiru anatakiwa akifanye katika kuboresha au kukuza soka lake. Kitu chenyewe ni kimoja na kidogo tu. Kidogo sana!
Akiwa uwanjani Simba na Stars, Mzamiru hufanya kazi ngumu sana, wakati mwingine hulazimika hata kufanya kazi chafu uwanjani.
Ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Simba na Stars wanaomwaga jasho jingi na kukimbia kilomita nyingi karibu katika kila mchezo. Kila ulipo mpira, karibu yake atakuwapo Mzamiru.
Hauwezi kuwa hivyo kama wewe ni mchezaji goigoi uwanjani, usiyependa kukimbia kwa bidii wakati wote ukiwa uwanjani.
Licha ya kufanya kazi ngumu na chafu, shida yake ni moja tu. Hapigi pasi sahihi – za uhakika na hawezi kuanzisha mashambulizi ya hatari kwenda katika ‘box’ la adui. Ni hapa tu ndipo Mzamiru anapopishana na Kante.
Kwa upande wake, Kante anafanya kazi ngumu na chafu akiwa Chelsea na Ufaransa kama ilivyo kwa Mzamiru, lakini yeye akiwa na mpira, anaisukuma timu kwenda mbele kwa adui. Hapotezi mipira. Ni mchezaji mahiri katika kukaba. Pia mchezaji mahiri katika kuanzisha mashambulizi.
Kante alipokuwa Leicester City alikuwa kiungo ‘punda’ kwelikweli kama tunavyomuita Mzamiru huku kwetu. Ndani ya Leicester City alikaba zaidi kuliko kuisukuma timu juu, lakini maisha yamekuwa tofauti alivyohamia na kusajiliwa na Chelsea.
Ndani ya Chelsea, Kante amekuwa mahiri katika kulinda lango la timu yake; mahiri katika kulitafuta ‘box’ la adui kupeleka mashambulizi.
Waliombadili Kante kwa asilimia kubwa ni makocha raia wa Italia; Antonio Conte na Maurisio Sarri. Ni hawa waliotupa sisi mashabiki wa soka huyu Kante tunayemfahamu leo.
Mzamiru ana kitu kikubwa cha kujifunza kutoka kwa Kante. Anachokifanya Mzamiru katika ulinzi, akikifanya pia katika kushambulia hata kwa asilimia 30 tu, sidhani kama majina ya kina Chama na Miquessone yangekuwa makubwa pale Msimbazi.
Tungekuwa tunapoyataja majina ya kina Chama, jina linalofuata ni yeye. Mtazame Kante licha ya kuwapo utitiri wa mafundi Chelsea, lakini huwezi kutaja majina matatu, usimtaje na yeye. Wataje kina Cristian Pulisic, Mason Mount, lakini bado nafasi ya Kante itabaki. Naye utamtaja tu.
Mzamiru aanze kumtazama Kante kama kioo chake. Viko vingi vya kujifunza, atavipata. Hii kuwa na sifa ya kukaba sana, kisha ukipata mpira hauna madhara langoni mwa adui haimpi thamani anayostahili.