Na Andrew Chale, Dar es Salaam

Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), kupitia taasisi yake ya mikopo ya Uwezo Financial Service Limited (UFSL) limedaiwa kuuza nyumba ya muumini wake kwa kushindwa kulipa riba iliyopanda bila kuzingatia sheria mamlaka za kibenki nchini.

Akizungumza kwa uchungu, Festo Aron ambaye ni mume wa Happy Francis aliyekopa mkopo kupitia UWEZO, amesema kuwa mkewe Happy alikopa mkopo wa Milioni 6, lakini baada ya muda walikuja kushangaa kupewa deni kubwa lililofika zaidi ya Milioni 18 kama riba kitu ambacho walishindwa kulipa hilo deni.

“Baada ya kupewa riba hiyo ambayo haikueleweka tulienda kuomba Uwezo waondoe penati hiyo, walikataa tukaenda mamlaka za kisheria watusaidie

Lakini mwisho wa siku wao wakachezesha kesi kwa njia ya rushwa na kuja kuvunja nyumba yetu kututoa nje siku ya Jumanne Mei 16,2023, majira ya saa 11 jioni.

Festo amesema kuwa, watu hao hawakufika na nyaraka zozote zaidi wao walivunja na kutoa vitu nje huku mali zikiibiwa.

Festo ameongeza kuwa, pamoja na kuuza nyumba yao hiyo kwa milioni 25, Uwezo wamechukua pesa yote kwa kusema ni ya kwao bila kumuachia chochote na kutoa vitu nje.

… kwa sasa hatujui hatma yetu. Tunatoa tahadhari kwa waumini wenzetu wa TAG kuwa makini na mikopo hiyo kwani haipo kwa kusaidia waumini zaidi kurudisha nyuma waumini wao.” Amesema Festo.

Na kuongeza: “Leo ni siku ya tatu tunalala nje tunaomba Serikali itusaidie kwa hili, mke wangu hayupo sawa kwa sasa na familia ndo inapitia kwa wakati mgumu” amesema Festo.

Kwa upande wake Mwanasheria wa UWEZO, Godliving Mambo ambaye aliongea kwa njia ya simu, na mwandishi wa habari hizi amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa, zaoezi limefanyika na wahusika kama wameona ni kinyume na utaratibu  basi waende kwenye vyombo vya sheria.

‘’kuna mahakama, waende mahakamani watasikilizwa kama sie hatukufuata taratibu. Wao kama wana hayo madai yote basi twende mahakamani na mahakama itadai haki.’’ amesema Godliving huku akisisitiza kuwa wao walifuata sheria lakini hakuweka bayana ni viongozi gani walioshuhudia tukio hilo wakati wa kutoa vitu hivyo

Hata hivyo alipotafutwa mjumbe wa shina wa eneo hilo, Asha Shaban Mrisho ambaye ni Mjumbe wa Shina namba 07, mtaa wa Bonyokwa amesema kuwa hakushirikishwa na watu hao wa UWEZO.

‘’Mimi hao watu kwenda kuvunja sina taarifa zao, ila nina taarifa za waliovunjiwa walikuja kuripoti kwangu, ili waende mbele zaidi kupata msaada” amesema Mwenyekiti huyo, Asha Mrisho.
 
Nae Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bonyokwa, Maliatabu alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo amesema hakushirikishwa na wala hatambui jambo hilo.

“Mimi natambua jambo hili hatua ya awali miaka miwili iliyopita lililetwa hapa, lakini baada ya hapo sijashirikishwa tena mpaka leo hii unavyoniambia wewe Mwandishi ” amesema Mwenyekiti huyo Maliyatabu.


Naye kaka wa mke aliyekopa fedha hizo, Morice Aron amesema kuwa yeye alipata taarifa baada na kufika eneo hilo ambapo alikuta vitu vipo nje.

“Huu ni unyama, wamevizia nyumba watu hawapo wameingia na kuvunja. Hali hii sio nzuri kwa waumini wake kwani kutuvua nguo” amesema Morice.

Kwa upande wao baadhi ya waumini walioongea na Mwandishi wa habari hizi, wamesema kuwa: “Hili suala muumini huyu sio la kwanza. Kuna waumini wengine yamewatokea wengi hawaweki wazi kwa jamii.

Lakini pia hata watumishi kwa maana wachungaji nao wamekumbwa na mikopo hii mpaka kutaka kuuza kanisa” alieleza mmoja wa muumini wa TAG anayeabanisa la Ubungo.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa TAG ambaye hakutaka kuweka jina lake amesema kuwa yeye alikopa mikopo hiyo hata hivyo, aliposhindwa kulipa kwa wakati riba ilikuwa kubwa hali ambayo ilipelekea kutaka kuuza kanisa lake.

“Mie nilikopa. Ilipofikia hatua nikapata riba kubwa hali iliyopelekea walitaka kuuza kanisa langu, lakini wakaamua kuniondolea riba na kubakia deni pekee hii waliona italeta picha mbaya kwa waumini ndo ikawa hivyo, alieleza kiongozi huyo wa dini wa TAG.

Waumini wengine wa TAG, wamehoji taratibu za riba zinazopanda bila kufuata sheria za Benki kuu ni kinyume cha taaisi za mikopo.

“Kumekuwa na malalamiko kuwa riba yao inapanda bila kufahamika.

Hata mikopo ya mabenki haipo hivyo, tunaomba Benki kuu ifuatilie hii na kuona uhalali wake kwani tunamashaka na huu usajili na hizi riba zao” ameeleza mmoja wa waumini wa TAG.

Habari zaidi za tukio hilo zinaendelea kufuatiliwa ilikubaini juu ya madai ya baadhi ya waumini na UWEZO.