Viongozi mbalimbali duniani wameendela kulaani jaribio la mauaji dhidi ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Trump alishambuliwa kwa risasi Jumamosi alipokuwa kwenye kampeni ya uchaguzi huko huko Pennsylvania.

Baada ya kauli za viongozi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, na mataifa mengine, uongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Vatican umelaani tukio hilo na kulielezea kama shambulio dhidi ya demokrasia.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema:

” Sote tulishuhudia hapo jana kwa mshtuko jaribio la mauaji ya kihalifu dhidi ya rais wa zamani na mgombea urais wa Marekani Donald Trump. Huu sio tu uhalifu mbaya, lakini pia ni jaribio la kuiua demokrasia ya Marekani.”

Trump mwenyewe amesema ni Mungu pekee ndiye aliyezuia jambo lisilofikirika huku akiwashukuru maafisa wa idara ya Ujasusi na maafisa wote wa usalama kwa hatua zao za haraka wakati wa shambulio hilo.