Januari, 2016 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikamilisha uanzishwaji wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency- PBPA). 

PBPA inatekeleza majukumu ya iliyokuwa kampuni binafsi ya kuratibu uagizaji wa mafuta ya petroli kwa pamoja (Petroleum Importation Coordinator Limited- PICL). 

Wakala huo ulianzishwa rasmi mwaka 2015 kwa lengo la kusimamia usalama wa mafuta ya petroli, dizeli, mafuta ya ndege (JET) na mafuta ya taa; pia, kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini wakati wote na kuhakikisha kuwa wale wote walioagiza mafuta wanapata malipo stahiki na kwa wakati.

Lengo la kuanzisha wakala huu ni kuongeza ufanisi katika shughuli za uagizaji mafuta nchini. 

Majukumu ya PBPA ni kusimamia mfumo wa uagizaji wa mafuta ya petroli kwa pamoja, na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya petroli ya kutosha wakati wote nchini. 

JAMHURI imefanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Michael Mjinja, kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya wakala wa uagizaji wa mafuta wa pamoja ikiwa ni pamoja na mikakati yake katika kusimamia biashara hiyo nchini.

JAMHURI: Nini PBPA mnafanya katika kufanikisha uagizaji wa mafuta wenye manufaa kwa nchi?

Mjinja: Katika mfumo huu wa uiagizaji wa mafuta kuna ‘key stakeholders’ ambao wapo katika mnyororo huu wa uagizaji wa mafuta. Tunazo kampuni za mafuta ambazo zimepewa leseni na EWURA ya biashara ya mafuta kwa ujumla, ambao ndiyo huwa wanatoa oda zao, na kutokana na zile oda sisi tunaandaa mtu wa kusambaza hayo mafuta.

Lakini pia tunazo kampuni ambazo tunakuwa tunazi pre-qualify kwa ajili ya kushindana kuleta mafuta. Lakini tuelewe kwamba katika mfumo huu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja, sisi kama wakala wa Serikali hatununui mafuta hayo kwa fedha yetu, ni hizi hizi  kampuni za mafuta zilizopewa leseni ya mafuta kufanya biashara ya jumla ndizo zinazomlipa huyo anayeleta mafuta hayo.

Kwa hiyo, kuna suala zima la kifedha, lakini tuelewe kwamba katika masuala ya fedha ni vyombo vya fedha ndivyo vinavyohusika. Tulipoanza mfumo huu, tulianza kwa zabuni za miezi miwili miwili, mitatu mitatu, na wakati ule shughuli hizi zilikuwa hazisimamiwi na wakala, zilikuwa zinasimamiwa na chombo kingine kinacoitwa Petroleum Importation Coordinator Ltd ambayo ilikuwa kampuni ya hawa wenye kampuni za mafuta wanaofanya biashara ya jumla ndiyo Serikali ilipowaambia waanzishe hiyo kampuni.

Katika kipindi hicho mpaka leo hii tunapofanya mahojiano haya, ni kampuni za nje tu ndizo zimekuwa zinashiriki katika hizi zabuni, pamoja na kuwa zipo kampuni za ndani ambazo zimeonesha ku pre-qualify. Lakini ni kampuni za nje tu ndizo zilizokuwa zinaweza kushiriki katika hizi zabuni.

Tulilazimika kufanya utafiti mdogo kuwauliza hawa wengine kwanini wanashindwa kushiriki katika hizi zabuni. Moja ya sababu walizozitoa ni kwamba kiasi cha mafuta kinachoagizwa na uwezo wao wa kifedha wa kuweza kununua hayo mafuta ulikuwa haviendani. Kifedha hawakuwa vizuri na wala vyombo vya fedha (benki) havikuweza kuwawezesha.

Kwa mfano, mafuta ya mwezi mmoja unaongelea kwa matumizi tu ya ndani hapa nchini mafuta ya ndege, petroli, mafuta ya taa unaongelea takriban 200,000 metric tons, lakini pia ukichukua na mafuta ya kusafirisha nje ya nchi (nchi jirani) unaongelea karibu 380,000 metric tons mpaka 400,000 na bei zinabadilika-badilika.

Kwa hiyo, unaweza ukakuta huyu anayesambaza mafuta anatakiwa kuwa na kama dola za Kimarekani milion 600 hadi 800 kwa mwezi, maana anasambaza mafuta ya Tanzania pamoja na nchi nyingine za jirani. Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa, hata benki za hapa nchini haziwezi kukuwezesha; inakuwa ni ngumu.

Kutokana na changamoto hiyo, tukaona ni vyema tukabadili utaratibu wa zabuni, badala ya kutoa zabuni za miezi miwili miwili tukaanza kutoa mwezi mmoja mmoja ili tupunguze ile gharama. Maana kwa miezi miwili ulikuwa unaongelea dola milion 800 mara mbili ambayo ni dola bilioni 1.6.

Lakini pamoja na kuweka kwa mwezi bado wakawa hawawezi. Tukasema hapa tunataka tushirikishe kampuni nyingi za kiushindani na hasa za hapa ndani. Hivyo, uamuzi tuliouchukua kwanza ni kuanza kufanya zabuni za meli kwa meli ili kuwezesha kampuni za ndani kuweza kushiriki, lakini pia uamuzi mwingine uliochukuliwa na unaotarajiwa kuanza Januari 2017, ni kwamba kampuni zote sasa ni lazima ziwe zimeandikishwa nchini. Hata zile za nje zikitaka kushiriki hii biashara lazima ziandikishwe nchini.

Tunategemea kwa kupunguza hiki kiasi cha mafuta yatakayokuwa yanashindaniwa yaani meli kwa meli, tunategemea hata hizi kampuni za ndani zitaweza.

JAMHURI: Wiki mbili zilizopita mlikaa na benki mbalimbali nchini, kikao hicho kilikuwa kinahusikaje na biashara ya mafuta?

Mjinja: Kwenye kikao hicho tulikuwa tumeita benki zote nchini ili tuwapatie hii taarifa, kuwa tunakwenda kwenye mfumo huu, wajiandae kupokea wateja hawa na kuwapatia ushirikiano, ni biashara tunawaletea.

Mjiandae ili kuwezesha hizo kampuni kwa sababu unaweza ukakuta kampuni imejiandikisha hapa lakini ikashindwa kutumia benki ya hapa sababu benki haina uwezo wakatafuta njia nyingine nje ya nchi. Kwa hiyo, bado benki zetu hapa zikakosa, hivyo tulikuwa tunawataarifu ili waweze kujiandaa, wajue kwamba hiyo biashara ipo inakuja, waweze kuichangamkia na wasaidie. 

Lakini pia ukiangalia kwa sababu zilikuwa ni kampuni za nje, kwa mwezi kampuni inachukua fedha za Kimarekani dola milioni 600-800, kwa sababu ni za nje, hakuna kodi ya mapato yoyote inayolipwa hapa nchini.

Hiyo tukasema hapana, hapa lazima washiriki wa ndani, hata hao wa nje tuwalazimishe wajiandikishe hapa ili angalau Serikali na nchi tupate haya mapato tuliyokuwa hatuyapati. Mbali ya kodi za mafuta ambazo zinatozwa yanapoingia, lakini pia tutapata kwenye mapato ya ndani (domestic revenue). Mfumo huu unakwenda kwenye kampuni za ndani ambazo zimeandikishwa nchini. 

Sababu kubwa ni hizo mbili, kwanza kuziwezesha kampuni za ndani kushiriki katika hii biashara ya kuleta mafuta, lakini pia kupata haya mapato kwenye mapato ya ndani kwa sababu zitakuwa ni kampuni za ndani.

JAMHURI: Kwanini mchakato huu ufanyike sasa? 

Mjinja: Wakala wa Serikali katika kusimamia hii, tumeanza kazi rasmi Januari 1 mwaka huu (2016). Kwa hiyo, mtu anapotuuliza ni kwa nini sasa, kwa sababu wakati ule ilikuwa kampuni binafsi ndiyo iliyokuwa inasimamia lakini sasa ni wakala wa Serikali ndiyo unaosimamia. Kwa hiyo, PBPA imepitishwa kwa sheria ya mwaka 2015 na rasmi kazi tumeanza mwaka huu kama nilivyosema hapo awali. 

JAMHURI: Unadhani kikao kilichofanyika kati ya PBPA na mabenki kitazaa matunda katika uwekezaji huu?

Mjinja: Nina uhakika kitazaa matunda, na ninajua yapo mabenki ambayo yanaweza kuwawezesha wafanyabiashara kutokana na kiwango kidogo kilichowekwa. Huo uhakika ninao.

Kwa sababu baadhi ya mabenki hapa nchini yapo katika mkondo wa kibiashara na benki nyingine nje ya nchi, najua bado kuna mabenki ambayo yataweza. Lakini huu si mwisho kwa sababu tupo sasa kwenye utaratibu wa kuchambua kampuni za ndani zitakazokuwa zinashindana katika kusambaza mafuta. Tumeshatoa hilo tangazo.

 

>>ITAENDELEA>>