Wakati fulani kule nchini Marekani kulitokea malumbano makali baina ya kampuni za Brother na Smith Corona zenye nguvu na ushindani mkali. Kampuni hizo zinajishughulisha na utengenezaji wa bidhaa zinazofanana zikiwamo mashine za kuchapa (typewriters), vichapishi (keyboards) za kompyuta, viyoyozi na vifaa lukuki vya kielektroniki.
Chimbuko la malumbano hayo lilikuwa ni ukiukwaji wa sheria inayokataza mrundikano wa bidhaa zisizo na ubora na zinazozidi wingi usiozingatia mikingo (limitations levels) katika soko. Sheria hii inayofahamika kama Anti-Dumping Law ilionekana kuvunjwa na kampuni zote mbili.
Kampuni ya Smith Corona ilituhumiwa kutengeneza kashfa hiyo ya kibiashara ili kusaka uwezekano wa kuimaliza kampuni ya Brother iliyokuwa tishio kubwa kwake. Smith Corona ilizichanga kizembe karata zake na kuibuka na hoja nyepesi ya utaifa wa kampuni. Smith Corona iliasisiwa nchini Marekani na hata makao yake ya kidunia yapo huko huko huko Marekani, wakati Brother iliasisiwa nje ya Marekani na kuanzisha tawi lake nchini humo.
Fikra za wakurugenzi na wamiliki wa Smith Corona zilidhani kuwa kwa kutumia karata ya uzalendo, tume ya ushindani wa kibiashara ingewahurumia wao na kuwaadhibu washindani wao (Brother) ambao ni wageni wa kutoka nje ya Marekani.
Smith Brother walivitumia vyema vyombo vya habari na kujipamba mbele ya Wamarekani kuwa wao ni wazalendo na hivyo wanatakiwa walindwe na kuhurumiwa kwa sababu wao ni ‘wahapa hapa’. Baada ya Tume ya ushindani ya Marekani kusikiliza shauri hilo, iliamua kuwa Brother haikuwa na kosa lolote na badala yake Smith Corona ndio iliyoonekana na makosa na hivyo ikawajibishwa.
Pamoja na kuwa Smith Corona walikuwa ni ‘wazalendo’ lakini walipigwa mweleka na ‘wageni’ kiushindani halisi sokoni na katika shauri mbele ya chombo cha kibiashara. Hapo kukapatikana somo moja kubwa katika ulimwengu wa kampuni hasa za kimataifa ya kwamba; suala la msingi si kuwa kampuni ya kizalendo bali ni kuwa kampuni inayoshindana katika soko kwa mujibu wa viwango na sheria.
Moja ya changamoto kubwa zinazokabili biashara nyingi katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, ni ushindani mkali kutoka kwa kampuni kubwa kutoka mataifa yaliyoimarika kiviwanda. Kampuni ninazozigusia hapa ni zile zinazoendesha uzalishaji ndani ya nchi mbalimbali duniani, huku zikiwa na makao yake makuu katika nchi mama.
Ni vema kufahamu kuwa Kiswahili kinachanganya maneno mawili ya Kiingereza – multinational companies na international companies – kwa kuyaweka kwenye neno moja tulilolizoea, yaani kampuni za kimataifa. Ipo tofauti ya kimantiki.
Tunaposema ‘multinationals’ tunamaanisha kampuni ambazo zimefungua matawi katika nchi mbalimbali zikifanya uzalishaji kamili wa bidhaa katika nchi hizo wakati ‘internationals’ ni kampuni zinazozalisha bidhaa katika nchi moja na kisha kuzisafirisha kwenda mataifa mbalimbali. Kwa hapa Tanzania tuna changamoto kubwa kwani kampuni ambazo ni ‘multinationals’ ni chache mno na hata kuwapo kwake hakuna nguvu kubwa kimataifa. Ingawa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na hamasa kubwa kwa kampuni za hapa nchini kujitanua na kuanza kuwa ‘internationals’ pale tunaposhuhudia zikisafirisha bidhaa kwenda mataifa jirani na nchi za Magharibi na Marekani.
Hii ni tofauti na jirani zetu Wakenya ambao misuli yao kibiashara imetanuka na wana kampuni za ‘multinationals’ na zinazoonesha nguvu ya kibiashara na kweli zinatamba. Upo mfano mzuri wa benki yao ya Kenya Commercial Bank (KCB Tanzania) iliyopenya hadi nchi kadhaa za Afrika; wakati huo huo sisi tunajikongoja na benki zetu za Kitanzania ambazo hata soko la ndani ya nchi ni changamoto kubwa mno.
Katika nchi mama ambako kampuni inaasisiwa ndiko kunakokuwa kichwa cha kampuni na katika nchi ambako kampuni husika inajisambaza kunakuwa ni mikia. Kuwapo kwa dhana hii ya ‘head and tail’ ndiko kulikoibua mjadala mzito miongoni mwa wanataaluma wa sayansi ya biashara unaohusu utaifa wa kampuni za ‘multinationals’
Utaifa kuhusu kampuni hizo (multinationals) unaonekana kuwa na mantiki kubwa kutokana na tabia, hulka na mienendo inayooneshwa na kampuni husika. Idadi kubwa ya kampuni hizo (kama si zote) kimsingi hazina nia ya kulinda maslahi ya nchi zinakokwenda. Kuna nyingi zinazotiliwa shaka ikiwamo ya kupendelea kuchukua malighafi za kuzalishia kutoka mataifa mama, uonevu kwa kampuni za nyumbani na uhatarishi katika mambo ya usalama wa taifa.
Zipo kampuni zinazopewa ruzuku na serikali za nchi zao, nyingine huchukua mitaji kwenye benki za nchi mama na wamiliki kuwa katika nchi mama. Kitendo hiki husababisha kampuni hizo kujikuta zikilinda hata maslahi ya kisiasa ya nchi mama. Hiyo nayo ni hatari kwa sababu taifa husika huwa shakani.
Kampuni nyingi za ‘multinationals’ zina nguvu kubwa kiuchumi na zina faida mororo za kiuzalishaji. ‘Multinational’ inapoingia katika nchi husika ni rahisi kuzimaliza kiushindani kampuni za nyumbani na kuziacha hoi bin taaban. Ujanja mwingine unaotumiwa na kampuni za aina hiyo ni kuficha ama kuzuia teknolojia na ufundi wa kiugunduzi.
Kwa mfano, kampuni ya Coca-Cola yenye makao yake makuu kule Atlanta, Marekani ni ya kimataifa (mMultinational) ambayo imefanikiwa kushika masoko ya vinywaji katika mataifa mengi ulimwenguni. Kampuni hiyo ina bidhaa kuu ambayo ni soda ya Coca-Cola lakini hadi leo kanuni ya kutengeneza unga wa soda hiyo, imebaki kuwa ni siri ya wagunduzi.
Kimsing siri za kiugunduzi hazina makosa kisheria (na ni haki ya mgunduzi kubaki na siri hiyo kwa manufaa yake ya kimaslahi ama kibiashara), lakini zinapochanganyika na nguvu za kampuni hizo kibiashara mara zote zimekuwa ni mwiba mkali kwa kampuni ndogo za nyumbani zinazojikongoja.
Tunaweza kubashiri hilo tunapoangalia bidhaa zinazobuniwa katika mataifa haya machanga zikitaka kushindana na bidhaa zinazotengenezwa na kampuni za ‘multinationals’.
Tujikumbushe jambo. Baadhi yetu tutakuwa tunakumbuka soda maarufu sana zilizokuwa zinatengenezwa mkoani Tanga zikijulikana kama Vimto. Pamoja na kuwa soda hizo zilikuwa nzuri na fahari ya Kitanzania lakini zilishindwa kuhimili ushindani katika soko ambalo tangu wakati huo lilikuwa limetawaliwa na soda tulizozizoea za Pepsi na Coca-Cola. Hiyo ilisababisha Vimto kujikuta zikijifuta zenyewe.
Kwa haraka haraka mtu anaweza kudhani kuwa wateja wanaendelea kununua bidhaa za kampuni za kigeni (na kuacha za kizalendo) kwa sababu ya ama kukosa uzalendo au kuwa na mazoea na bidhaa hizo. Hata hivyo, upo ukweli uliofichika kwamba kampuni za ‘multinationals’ na hata za ‘internationals’ zina mbinu na uwezo mkubwa wa kimasoko ambao ni vigumu kufikiwa na kampuni zetu ambazo ama ni changa au ni kongwe lakini dhaifu.
Ni dhahiri kuwa mikia (uzalishaji unaofanyika katika nchi nje ya nchi mama) ya kampuni hizo imekuwa ni jinamizi linaloendelea kuua viwanda vingi vya mataifa machanga. Mbali ya hiyo, pia kampuni kubwa za ‘internationals’ zimekuwa zikiingiza bidhaa nyingi na kwa bei ndogo katika masoko yetu na kusababisha hali mbaya kwa bidhaa zetu za nyumbani.
Huwa ninajiuliza itakuwaje siku moja kampuni ya McDonald’s ikifungua tawi lake Tanzania? MacDonald’s ni kampuni inayouza vyakula vya aina nyingi na iliyosambaa katika nchi nyingi duniani. Je, utakuwa wapi usalama wa kampuni za nyumbani zinazotengeneza biskuti? Tutawasalimishaje mama ntilie wetu na wale wanaotengeneza vitafunwa mitaani?
Ikiwa kampuni kubwa na yenye nguvu kama Smith Corona ilitolewa kamasi na kampuni ya kigeni na kuomba kuhurumiwa na serikali ya nchi mama, je, si zaidi kwa kampuni za kizalendo zilizopo katika nchi hizi masikini kuhurumiwa na serikali za nchi zao? Tutafakari, tuendelee kujadili, tuone ni kwa namna gani wazalendo watasaidika!
0719 127 901, [email protected]