Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imesema kuwa hadi sasa Kampuni 50 zina nia ya kuwekeza vituo vya kujaza gesi asilia iliyogandamizwa (CNG) nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano Ewura, Titus Kaguo, katika mafunzo ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji kwa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA).
Amesema Ewura inatoa vibali vya ujenzi ili kuhakikisha Huduma za gesi asilia iliyoshindiliwa zinafuata sheria, Kanuni na viwango stahiki.
“Ewura inaendelea kuhamasisha Watanzania na wadau mbalimbali kuwekeza kwenye CNG ili kuimarisha upatikanaji wa huduma,” amesema Kaguo.
Aidha Kaguo amesema Ewura imepambana na tatizo la uchakachuaji mafuta ambapo umepungua kutoka asilimia 80 mwaka 2007 hadi asilimia 4 mwaka 2022.
“Septemba 2010, Ewura ilianzisha program ya kuweka vinasaba kwenye mafuta yaliyotumika nchini ili Kudhibiti ukwepaji kodi, uchakachuaji na kuweka mazingira ya ushindani wa haki,” amesema.
Vilevile, amesema Ewura inaendelea kusimamia na kutatua migogoro na malalamiko ya walaji wa huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka hiyo dhidi ya watoa Huduma.
“Kati ya Julai 2023 na Juni 2024, malalamiko 258 yaliyotatuliwa ambapo 83 (33%) yalikuwa ya Ankara, 47 (17%) maunganisho ya Huduma, 18 (7%) yalihusu bei, 23 (9%) yalihusu ubora wa huduma, 22 (9%) Trespass, 34 (13%) Huduma kwa wateja, 13(5%) fidia, 1 (1%) kuharibu kwa Mali, 10(4%) moto na 4(2%) usalama wa afya, Mali na Mazingira.
“Utatuzi wa migogoro na malalamiko umefanyika kwa watoa Huduma kuwajibika kuboresha Huduma zao,” amefafanua.