Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko (ambae ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Hai) Mkuu wa Wilaya amezindua kampeni ya “Ubungo Usiku kama Mchana” ambapo katika wilaya hiyo kazi za uzalishaji na Shughuli za biashara zitafanyika usiku na mchana kwa siku zote.

Akizindua Kampeni hiyo mara baada ya kuzungumza na Viongozi mbalimbali wa serikali za mtaa na Kata pamoja na wafanyakazi kutoka Idara zinazotoa huduma katika jamii, Bomboko amesema kuwa Kampeni hiyo itaenda kuonesha taswira halisi ya wilaya ya Ubungo ambayo ni ya kimkakati na ni lango la jiji la Dar es Salaam.

“Ajenda hii tumeamua kuibeba kwa sababu Wilaya yetu ya Ubungo ni eneo la kimakakati na eneo ambalo ndio lango la
Jiji,” amesema.

Amesema kuwa wamehakikisha huduma zote muhimu zinaendelea kutolewa kwa saa 24, ikiwa ni pamoja na huduma za afya, maji na umeme upatikane kwa uhakika lakini pia kuwa na uhakika wa miundombinu kama barabara ziwe zinazofikika katika maeneo yote ya wilaya ya Ubungo.

“Lazima katika Barabara zetu na kuwe na taa zinazotoa mwanga ili ziweze kutafsiri kazi zinazofanywa usiku na mchana. Usiku ili uwe mchana ni lazima kuwe na mwanga watu wanapofanyia kazi,” amesisisitiza.

Amefafanua kuwa Wilaya hiyo wanamkakati wa kuhakikisha masoko, stendi na maeneo ya kimkakati na huduma za kijamii zinapatikana masaa 24 na zinafata uhakika wa mwanga wa kutosha katika maeneo yote.

Akizungunzia maandalizi ya kampeni ya Usiku kama Mchana, Bomboko amesema yameshakamilika kwa asilimia 80, ndio maana wameanza kutoa taarifa kwa umma, na asilimia zilizobaki wanaendelea kuimarisha miundombinu ili kufanikisha kampeni hiyo kwa saa zote 24.

Amesema kuwa masoko yaliyoainishwa ni Soko la Mahakama ya Ndizi, mabibo, Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli Mbezi, kituo cha daladala cha Mbezi mwisho na Soko la Kichinjia kuku la Shekilango, Manzese Baharesa, Sinza na Mlimani City.

Ameongeza kuwa maeneo hayo muhimu yanawafanya waweze kuangalia namna watu wanaweza kufanya biashara kwa masaa 24.

“Ulinzi na usalama lazima uimarishwe katika maeneo haya na tutahakikisha kunakuwa na mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na uhakika wa usalama wa mali zao na wafanyabiashara wenyewe,” amefafanua.