Vyombo vya uchunguzi vya Serikali vimeanza kufuatilia ujenzi wa nyumba tano zinazojengwa sehemu moja huko Salasala, Dar es Salaam, mali ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, John Minja.

Minja ametajwa kuendeleza eneo lake kwa kujenga mahekalu ya gharama kubwa ikilinganishwa na uwezo wa ofisa mwadamizi wa Serikali, imefahamika jijini Dar es Salaam.

Nyumba tano zimejengwa mahali hapo Mtaa wa Salasala, Mbezi Beach, Dar es Salaam, jambo linalozua maswali mengi kwa majirani zake huko Salasala.

Thamani ya nyumba zilizojengwa zinafananishwa na idadi kubwa ya nyumba za kigogo mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye ripoti za awali za uchunguzi zinaonesha ana nyumba 74.

Taarifa zinasema Minja anafanya ujenzi huo karibu na makazi yake ambapo magari ya Jeshi la Magereza hutumika katika ujenzi huo unaoendelea pamoja na watu wanaotajwa kuwa wanatumikia kifungo cha nje.

Imeelezwa kwamba wafungwa hao wa nje, wanatumika katika ujenzi wa mahekalu bila malipo, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Kwa mujibu wa taratibu za adhabu ya nje ya gereza, wafungwa wanaotumikia kifungo cha nje wanatakiwa kufanya kazi za kujitolea kwa saa zisizozidi nne, lakini kamishna huyo anawatumia kufanya kazi kwa zaidi ya saa nne kwa maslahi binafsi.

Aidha, mbali ya tuhuma hizo, anaelezwa kuwa ana mikakati ya kuhakikisha wakati wa kuachia madaraka yake hayo anafanikiwa kujimilikisha gari analolitumia hivi sasa ambalo lilinunuliwa miaka mitatu iliyopita.

“Tayari kunafanyika njama za yeye kuondoka na hilo gari analolitumia hivi sasa, hilo shangingi (Toyota Land Cruiser) lililonunuliwa likiwa jipya, na hivi ninavyokwambia ameshalifanyia matayarisho ili aweze kulimiliki, na kuna kigogo anamsaidia kufanikisha hilo,” anasema mtoa taarifa.

Pia katika eneo hilo la jirani na nyumbani kwake, anajenga ukumbi mkubwa wenye bwawa la kuogelea. Ujenzi wa ukumbi huo unaelezwa kugharimu kiasi Sh milioni 100 kwa mujibu wa wakadiriaji wa majengo (Quantity Surveyors) wa kampuni moja ambayo iliomba isitambulishwe kwa sasa.

“Bwawa hili ni la aina yake, na jengo hili ni la aina yake kwa sababu ya kuezekwa kwa kutumia ‘cherewa’. Ujenzi wa aina hii unagharimu. Ni wa kisasa kabisa,” anasema mkadiriaji huyo.

Kutokana na ujenzi huo wa mamilioni, baadhi ya watu wake wa karibu pamoja na majirani zake wameshangazwa na kasi na gharama hiyo. Vyanzo vya habari vya uhakika vililidokeza gazeti hili kuwapo na taarifa za kuchunguzwa kwa kigogo huyo kutokana na kufuru anayoifanya hivi sasa.

Kutokana na taarifa hizo, JAMHURI ilifika Salasala kufahamu ukweli wake, ambapo imeshuhudia ujenzi huo ukiendelea huku gari kubwa la mizigo aina ya Scania pamoja na gari ndogo (Land Rover) yakiwa eneo la ujenzi huo pamoja na askari wa Jeshi la Magereza.

Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya mafundi ambao walidokeza kuwa ujenzi huo umekuwa wa kasi kutokana na kupatikana kwa vifaa vya ujenzi na amri ya mwenye mali.

“Hapa tangu tuanze kujenga hatujawahi kusimama hata kidogo, kila kitu tunapata. Wewe mwenyewe si unaona haya mambo yalivyokuwa makubwa? Hapa ni kazi tu mpaka tukimaliza patakuwa panatisha hapa,” anasema mmoja wa mafundi ujenzi.

Hata hivyo, imeelezwa tayari kigogo huyo ameanza  kuchunguzwa ili  kuweza kubaini vyanzo vya mapato yake kutokana na kudaiwa kuwa na ukwasi mkubwa.

Habari za uhakika zinaeleza kuwa tayari timu ya uchunguzi imeweza kufika katika makazi yake na kushuhudia ujenzi unaoendelea ambako imeshtushwa na ujenzi huo.

“Yeye binafsi hajui kama tayari mambo yameharibika, vijana wameshafika site (eneo la ujenzi) na wamemaliza kazi yao, wameshangazwa na jamaa anavyoweza kufanya mambo makubwa haraka kiasi hicho, lakini tunaamini chochote kinaweza kutokea,” anasema mtoa taarifa.

Akizungumza na Mwandishi wa gazeti hili kwenye Viwanja vya Ikulu, mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamishna Minja hakutaka kufafanua kinachoendelea badala yake alitaka mwandishi azungumze na maofisa habari wa jeshi hilo.

Hata aliposisitiziwa ya kuwa ni suala linalomuhusu yeye binafsi, Kamishna Minja alisema: “Kwa sasa sina nafasi hivyo ni vyema kuwasiliana na kitengo cha habari na kama kuna siku nitapata fursa nitazungumza lakini si sasa.”