Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA), kuwaondoa wapangaji ambao hawalipi kodi ya nyumba, hususani watumishi wa taasisi za serikali.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso ametoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma eneo la Temeke.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mradi huo, Kakoso amesema TBA wanapaswa kuwachukulia hatua watumishi waliopanga katika nyumba zao kwa kuowaondoa pasipo kuwaonea huruma.
“Watumishi wa serikali walipe kodi wasikae bure. Waziri nenda kawasaidie TBA kuwaondoa wapangaji sugu wasiolipa kodi. Tunataka TBA ijitegemee isitegemee ruzuku kutoka kwa serikali, ” alisema Kakoso.
Mbali na kutoa agizo hilo, Kakoso aliitaka TBA kuajiri watumishi zaidi ili waweze kufanya kazi kwa weredi kwa sababu taasisi hiyo ina upungufu ya watumishi zaidi ya 500.
Pia, aliiagiza TBA kujiendesha kibiashara, wawe na vyanzo vya mapato vitakavyokuwa endelevu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya maagizo hayo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema wameyapokea maelekezo na wanakwenda kuyafanyia kazi.
Kuhusu watumishi kulipa kodi ya nyumba, Profesa Mbarawa aliwataka Watanzania kuwa na tabia ya kulipa kodi kwa wakati ili kupeusha usumbufu wa kuondolewa.
Alisema kwa sasa TBA wanaandaa mfumo wa smart lock utakaowazuia wapangaji sugu kukwepa kulipa kodi ya nyumba.
“Kwenye nyumba hizi na zingine zote nchini tunakwenda kuweka mfumo wa smart lock. Kama mtu hujalipa kodi huingii ndani,” alisema Profesa Mbarawa.
Naye Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro, alisema mradi huo unajengwa wa gharama ya Sh.bilioni 19.4 ambpao kwa sasa umefikia 15 na utatekelezwa kwa miaka miwili.
Mtendaji Mkuu Kondoro ameongeza kuwa mradi huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo mabadiliko ya hali ya hewa hususani nyakati za mvua, wizi wa vifaa mbalimbali vya ujenzi hali inayosababisha kucheleweshwa kwa utekelezaji.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iko jijini Dar es Salaam ambapo inapokea taarifa na kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Taasisi za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.