Mwanzoni mwa mwaka huu, uliibuka uhasama mkubwa uliohusisha pande mbili za dini ya Kiislamu na Kikristo mkoani hapa. Uhasama huu ulianza kama ‘mchicha’ kwa viongozi wa pande hizi mbili kuzuliana visa kutokana na nani au dini gani inastahili kupewa heshima ya kuchinja wanyama kwa ajili ya kitoweo.
Waislamu walisema wao ndiyo wanaostahili heshima hiyo, vivyo hivyo na Wakristo na wao wanastahili kuchinja wanyama. Wakati huo mambo hayakuwa barabara. Uhasama ulizidi mipaka hadi kusababisha maafa mkoani Geita, yaliyotokana na mapigano yaliyoibuka baina ya Waislamu na Wakristo katika mji wa Buseresere-Katoro. Maafa haya yalilaaniwa na watu wote wapenda amani nchini.
Baada ya mauaji ya kiongozi huyo wa dini ya Kikristo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda (pichani) alifika Mwanza na Geita kusaka suluhu na ‘mchawi’ wa mambo hayo! Akaagiza iundwe kamati maalumu itakayohusisha wajumbe wa pande zote mbili na ishughulikie suala hilo kwa haraka sana. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, ndiye aliyepewa jukumu hilo. Tayari ameshaunda kamati hiyo yenye wajumbe 20 kwa kuzingatia madhehebu ya dini ya Kikristo na jumuiya zote za dini ya Kiislamu.
Kimsingi, kamati hii ni muhimu kwa kusaka amani, upendo na utulivu katika mikoa hii ya Mwanza na Geita, iliyogubikwa na sintofahamu kuhusu waamini wa dini hizi na hata wasiokuwa na dini.
Idadi kubwa ya wakazi wa mikoa hiyo wana shauku ya kuona na kusikia kamati hii inarejesha amani na kuondoa uhasama uliosababisha umwagaji damu.
Kinachoangaziwa na kutarajiwa na watu wengi ni kwamba pamoja na Serikali kutoa hadidu za rejea kwa kamati hii, upo umuhimu mkubwa kuhakikisha wajumbe wa chombo husika wanakuwa makini na wanaondoa tofauti zao katika suala hilo. Nionavyo mimi, wajumbe wa kamati hii wasifanye kazi yao kwa kuangalia nani ni nani katika suala hilo la uchinjaji. Usiwepo udini katika kutafuta suluhu na maridhiano juu ya nani achinje!
Naamini Wislamu na Wakristo kwa imani zao, wote wanamwomba na kumwamini Mungu mmoja aliye mbinguni. Hivyo, hapana shaka kamati hii itakuwa msaada mkubwa katika kumwondoa mtu anayetishia amani kwa Watanzania.
Kamati hii kamwe isithubutu kwenda nje ya kazi zake. Ikiteleza na kuingia kwenye malumbano ya wenyewe kwa wenyewe kuna hatari kubwa ya kusababisha mauaji mengine ya kutisha kuliko yaliyotokea kule Geita. Hatuombi hayo yatokee.
Pinda aliagiza kuwa wakati Serikali ikitafuta suluhu ya mgogoro huo, kazi hiyo ya kuchinja wanyama iendelee kufanywa na Waislamu maana ndiyo mazoea ya tangu zamani.
Kinachotakiwa hapa ni viongozi hawa wa dini za Kiislamu na Kikristo pamoja na waumini wao kupanua mioyo yao kwa kuwa wavumilivu. Bila hivyo, viongozi hawa wataitumbukiza nchi yetu pabaya kama tunavyoona kule Nigeria, Somalia, Afghanistan na mataifa mengine ambako amani imetoweka!
Akiizindua kamati hii, Ndikilo aliwataka wajumbe husika kuzingatia na kuiheshimu kazi waliyopewa kwa dhamana ya usalama na maisha ya wananchi. Lakini pia, Ndikilo amewahi kukaririwa akisema kuwa kamwe Serikali haitaingilia kazi ya kamati hiyo, isipokuwa inahitaji kupata taarifa za utekelezwaji wa kazi husika.
Kutokana na umuhimu wa kamati hii, tunataka viashiria vyote vya mambo ya kijinga na ya kipumbavu vitakavyoonekana kufanywa na baadhi ya wajumbe wake, Serikali isisite kuwawajibisha. Hatutaki porojo kwa wakati huu nchi inapokuwa katika hali ya hatari. Sina uhakika kama kuna watu wenye malengo ya kuleta mapinduzi ya nchi hii kupitia dini fulani.
Lakini, kinachotakiwa ni Serikali kuchukua hatua kwa kudhibiti pale chokochoko za aina yoyote za kuvuruga amani ya nchi zinapojitokeza. Isisubiri mambo yaharibike ndipo ikimbilie kuunda tume au kamati kama hii.
Wahenga walisema, “Usipoziba ufa utajenga ukuta. Ngoja ngoja huumiza matumbo. Mdharau mwiba mguu huota tende. Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.”
Iwapo Serikali italala na kushindwa kuzifanyia kazi methali hizi kwa kudhibiti viashiria na chokochoko za mtu, kikundi au madhehebu moja la dini, ipo hatari nchi ikaingia kwenye machafuko na umwagaji mkubwa wa damu.
Katika kushughulikia mambo yanayohusu amani na maendeleo ya nchi, ulegelege wa aina yoyote kwa kila kiongozi hasa watawala, hautakiwi kabisa. Umakini unatakiwa muda wote wa kazi. Upuuzi na dharau ni sumu katika safari ya mafanikio.
Watawala wetu, wananchi na makundi yote ya kijamii lazima tushikamane kwa pamoja kulinda na kutetea ustawi wa nchi yetu.
Maendeleo ni kitu muhimu sana kwa nchi au mtu mmoja mmoja. Hakutakuwapo na maendeleo yoyote iwapo Serikali italala na kushindwa kutimiza wajibu wake kwa jamii.
Kwa maana hiyo, kamati hii ya kusaka suluhu ya nani achinje, ifanye kazi zake kwa umakini na ilete tija kwa wananchi, isitumie fedha za wananchi bure!
+255 (0) 777 068270