…Yaaendelea kuwahoji wafanyabiashara
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo kuchunguza wafanyabiashara wa kigeni maeneo ya Kariakoo imefikia asilimia 50 ya uchunguzi wake na imeahidi kukabidhi ripoti hiyo Machi 2 kama ilivyoagizwa.
Februari 2 Waziri Jafo aliunda Kamati ya watu 15 kuchunguza wafanyabiashara wa kigeni eneo la Kariakoo inayoongozwa na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Lwoga
Aliunda Kamati hiyo baada ya agizo la Rais Samia alitoa agizo hilo Januari 30, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya chakula cha mchana alichokiandaa kwa ajili ya washiriki wa shughuli ya uokoaji wa kuporomoka kwa jengo Kariakoo.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Edda Lwoga ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE).
Alisema baada tu ya uteuzi walianza rasmi kazi ya kuwahoji wafanyabiashara wa makundi mbalimbali kama machinga, wauza vifaa vya umeme, vifaa vya magari, vipodozi na biashara zingine.
“Hata leo hapa tuko na wafanyabiashara wa Kariakoo tunaendelea kuhojiana nao kupata taarifa zaidi kuhusu changamoto ya wafanyabiashara wa kigeni ili tuweze kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kuondoa changamoto hii,” alisema Profesa Lwoga.

“Tuliagizwa tutoe ripoti yetu ndani ya siku 30 na kwa hatua ya asilimia 50 tuliyofikia tunaimani tutaikamilisha na kuikabidhi kwa mamlaka ndani ya muda huo tuliopewa,” alisema Profesa Lwoga.
Alisema mbali na kukutana na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wametoa namba ya simu ya bure ambayo mwananchi yeyote anaweza kupiga na kutoa maoni yao.
“Tunapokea maoni kwa njia mbalimbali ili tutakapotoa ripoti iwe imegusa maeneo mbalimbali kwa hiyo mwananchi popote alipo Tanzania atoe maoni kwa hiyo tunaomba watu watupe maoni yao,” alisema
Alitaja namba ambazo wananchi wanaweza kupiga bure na kutoa maoni yao kuwa ni namba 080011616 na namba whatsap ambayo mwananchi anaweza kutuma ujumbe ni 0738 816113.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Conrad Millinga kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu alisema lengo la kamati hiyo ni kuona kwamba biashara zinazofanyika nchini zinawanufaisha zaidi watanzania.
“Wageni wanakaribishwa kufanyabiashara nchini, huwezi kukataa wafanyabiashara wa kigeni lakini tunataka wakija wafanye biashara zao kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi zilizopo wasifanye holela tu,” alisema
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severini Mushi aliwaomba wafanyabiashara kuitumia kikamilifu fursa hiyo waliyoipata kutoka serikalini kutoa maoni yao ili changamoto hiyo iweze kupatiwa ufumbuzi.
“Njooni mtoe ushirikiano kwa kamati ambayo imetembelea wafanyabiashara mbalimbali na tukitoa ushirikiano wa kutosha kwa kamati hii tutaiwezesha kumaliza kazi yake kwa wakati na kutoa ripoti yake kwa Waziri,” alisema.

Mjumbe mwingine kutoka kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA), Ted Sikuluwasha alisema mbali na kukutana na wafanyabiashara, kamati itafanya mahojiano na baadhi ya taasisi za serikali kuhusu changamoto hiyo.
Alisema kamati hiyo itafanyakazi zake kwa umakini mkubwa na kuishauri serikali namna bora ya kuondoa changemoto hiyo ili kuweka ushindani ulio sawa wa biashara baina ya wageni na wale watanzania.
“Tunapambana kuikamikilisha hii kazi kwa wakati lakini lazima tuzifikie pande zote ili tuweze kushauri vizuri kwenye ripoti tutakayoandaa, tumefikia asilimia 50 na tunaamini Machi 2 tutakabidhi ripoti,” alisema